Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuzipongeza Kamati zote kwa kazi nzuri ya kutoa taarifa ya utekelezaji kuhusu kilimo, mifugo na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa, nchi yetu ilishiriki katika Azimio la Abuja la tarehe 30 Novemba hadi tarehe Disemba Mosi, 2006. Katika Azimio la Abuja kulikuwa na makubaliano kuwa nchi zitenge angalau asilimia 15 ya bajeti za nchi zao katika kilimo. Sisi Tanzania bado tupo chini katika kufikia azimio hilo kuhusu kilimo. Kama ilivyobainisha Taarifa ya Utekelezaji ya Kamati, ukurasa wa sita na saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo nchi za Rwanda, Botswana, Nigeria, Malawi, Zambia na Burkina Faso wameweza kutenga bajeti zao za kilimo zaidi ya asilimia 15 ya bajeti zao. Wenzetu Rwanda wameenda mbali zaidi kwa kutenga asilimia 18.8 ya bajeti yake kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inaingia katika uchumi wa viwanda na viwanda hivi vinahitaji malighafi itokane na mazao ya kilimo. Je, kwa bajeti ambayo haifiki asilimia 10 tutaweza kufikia huo uchumi wa kati wa viwanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli napenda kuishawishi Serikali kuona umuhimu wa kuongeza bajeti ili kuleta ufanisi katika kilimo na kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo cha umwagiliaji ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazoweza kuleta mapinduzi ya kijani. Suala la utegemezi wa mvua haliwezi kutuvusha kwa jinsi tunavyotaka mapinduzi ya kilimo kwa haraka. Tumeona jinsi mvua zilivyoleta maafa na
mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini. Iwapo ungekuwepo utaratibu wa kitaalam wa kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua yangeweza kutumika kwa umwagiliaji na hatimaye yangeleta tija. Naishauri Serikali yangu sikivu na Tukufu kuona unafanyika utaratibu wa kuhifadhi maji ya mvua ili yaweze kutumika kipindi cha baadaye na hata ikiwezekana katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utoaji miche ya mikorosho katika Mikoa ya Kanda ya Kati, Dodoma na Singida. Naipongeza Serikali kwa kutoa miche ya korosho. Nashauri ufanyike uhamasishaji wa kutosha kabla ya kipindi cha mvua, ili wananchi waweze kuandaa mashamba ya kupanda miche hiyo. Nashauri miche ya mikorosho itolewe mapema ili wananchi waweze kupata tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.