Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza mimi mkubwa kuliko Mheshimiwa Bashe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi angalau dakika tatu hizi, ili niweze kuchangia. Naenda moja kwa moja kumgusa mkulima ambaye asilimia 90 ya Wanarukwa ni wakulima wa zao la mahindi. Nimekuwa nikilalamika sana hapa kuhusiana na zao hili la mahindi kwamba sisi wakulima wa Rukwa asilimia kubwa tunalotegemea ni zao letu la mahindi kama zao la biashara. Nasikitika sana leo hii Sumbawanga kama alivyosema Mheshimiwa Malocha, gunia la mahindi ni shilingi 21,000 kwa mara ya kwanza kwa miaka 15 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niliwahi kulisema na Mheshimiwa Waziri hapa akatoa kauli kwamba tumefuta, sasa tunafungua milango ya kwenda kuuza mahindi kokote kule mkulima anapotaka. Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Waziri akaweka kikwazo kingine cha kutaka kibali. Hivi kuna mkulima gani anaweza kutoka Sumbawanga kuja kufuata kibali Dodoma? Hapo tulikuwa tunakaribisha rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inanisikitisha sana, huwezi kuruhusu mazao yaende nje halafu tuweke kikwazo kingine. Mkulima hawezi kuhimili vikwazo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha sana mbolea leo Sumbawanga hakuna; na ikiwepo ni mbolea ya magendo na leo hii toka jana kuna foleni kubwa sana ya kununua mbolea. Mbolea Urea leo hii imefika shilingi 65,000 mpaka shilingi 70,000. Huyu mkulima tunamweka katika fungu gani? Kwanza kabisa anabanwa kwenye mbolea, pili anabanwa kwenye kuuza. Sasa afanye biashara gani? Halafu kubwa ninachosikitika mimi sijui Mawaziri wetu wanafikiria nini? Bahati mbaya tunapochangia, wao wanacheka, mimi hii kitu huwa naumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu kwa nini havichukuliwi kuwa serious? Leo hii Mkenya anatoka hapa anakwenda kununua mahindi Zambia, anayapitisha kwenye barabara yetu, kwa magari yetu, anakwenda kuuza kwao, anatuacha sisi Tanzania tunakosa soko la kuuza mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, WFP badala ya kununua mahindi Tanzania na baada ya kukosa kibali cha kusafirisha mahindi kwenda nje, wameenda kununua mahindi Zambia, wameleta hapa, yako hapa Dodoma, yanasubiri kwenda maeneo mengine, sisi tumeshindwa kuwauzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, ifike wakati sasa Serikali ikae chini iliangalie jambo hili. Sisi tunao wajibu wa kuwawakilisha wakulima wetu, tuna wajibu wa kuwawakilisha wananchi wetu, lakini zao kubwa ambalo sisi tunalotegemea ni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima huyu anahitaji akivuna mazao yake auze ili aweze kununua bati, auze ili aweze kumsomesha mwanafunzi. Tumesema kila siku hapa lakini Serikali haitusikii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba leo Mheshimiwa Waziri, tunaanza kuvuna mazao mwezi wa tano na sita, lisije likatokea jambo lingine hapa ukatuambia unafunga tena mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hape kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)