Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuzungumza. Nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati kwa taarifa nzuri sana waliyowasilisha lakini pia bila kumsahau dada yangu Mheshimiwa Anne Kilango Malecela kwa hotuba yake nzuri sana ambayo ameimalizia hivi punde. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuipongeza sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri sana ambayo imefanya. Kuna watu ambao wanakaa wanasema tangu uhuru hatujafanya chochote, siwezi kuwakatalia kwa sababu wengi ni watoto wa miaka ya 80 na 90. Sisi ambao tumezaliwa tukiwa tunapita katika Mto Rufiji tukivuka kwa pantoni na sasa hivi tunapita katika Daraja la Mkapa katika Mto Rufiji tunajua wapi tulikotoka na kazi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niipongeze Wizara ya Miundombinu kwa kazi kubwa sana inayoifanya katika kupanua bandari zetu. Katika taarifa na hata hivi karibuni mimi mwenyewe nimeshuhudia uzinduzi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja Bandari ya Mtwara. Kazi kubwa sana inafanyika kule kuhakikisha kwamba kule Mtwara tunaongeza Gati namba mbili ambalo litakuwa na urefu wa mita 300. Nina uhakika kabisa baada ya hapo korosho zetu na mizigo yetu ya Mtwara itakuwa inapita bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara - Newala - Masasi. Sasa hivi tayari mkandarasi yupo kazini, anajenga kipande cha Mtwara - Mivata zaidi ya kilometa 50. Niiombe Serikali yangu kile kipande kilichobaki basi mkandarasi mwingine sawa na ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alivyoahidi kwamba vipande vyote vilivyobaki vitatafutiwa wakandarasi, hivyo tutafutiwe wakandarasi kwa sababu sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kazi yetu kuunga mkono bajeti yetu ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba ile miradi yetu itekelezwe na wale ambao wanaikataa bajeti wasishangae katika maeneo yao kuona mpaka sasa hivi hakuna kinachofanyika kwa sababu hakuna bajeti waliyoipitisha kwa ajili ya miradi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niunge mkono ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge ambao unaendelea sasa hivi kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro na pia kutoka Morogoro hadi Makutupora. Pia suala la ujenzi wa viwanja vya ndege, naipongeza sana Serikali yangu na naipongeza sana kwa kulifufua Shirika letu la Ndege kwa kununua bombardier zile ambazo kwa kweli wote bila kujali vyama tunazipanda na tunazitumia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina changamoto moja tu ambayo nataka kuishauri Wizara ya Miundombinu, ndege zetu hizi zinalala au zina-park saa 10.00 au saa 11.00. Tatizo kubwa sana bombardier zinaweza kutua Uwanja wa Songwe, Kigoma, Mtwara, Bukoba na Songea lakini viwanja hivi vingi havina taa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Waziri wa Miundombinu ahakikishe kwamba viwanja hivi vinawekwa taa ili ndege zetu hizi ziweze kutumika kwa ufanisi zaidi. Tunaweza kwenda Mtwara hata saa 4.00 au saa 6.00 usiku kama uwanja una taa lakini unakuta ndege zinakimbizana na jua, jua likizama na zenyewe zina-park. Pia viwanja hivi tukiweka taa tunaongeza hata usalama kwa ndege ambazo zinapita katika anga za kimataifa kukiwa na matatizo ya kutaka kutua wawe na viwanja mbadala vya kuweza kutua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanja vyetu vingi vinakosa sifa ya kuweza kutua usiku kwa sababu ya ukosefu wa taa. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa katika bajeti inayokuja ahakikishe viwanja vyote ambavyo bombardier inatua basi viwekewe taa ikiwemo pamoja na Kiwanja cha Mtwara. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa naipokea, ni kweli hizo pesa Mheshimiwa Rais amesema lakini lazima nikumbushe kwa sababu viwanja vilivyo kwenye huo mpango ni vingi, kwa hiyo, Waswahili wanasema lazima kamba kila mtu anavutia kwake. Kwa hiyo, naikubali taarifa na mimi namsisitiza Waziri kwamba zile pesa zilizotengwa hizo taa ziwekwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na upande wa Wizara ya Nishati. Nataka nizungumzie deni la TANESCO. Deni la TANESCO ni la historia, tunalo kwa muda mrefu kwa sababu muda mrefu shirika letu lilitaka kubinafsishwa. Sasa yale madeni tukisema tuiachie TANESCO yenyewe iweze kuyalipa sidhani kama tunaitendea haki. Naishauri Serikali yangu ione uwezekano wa kuisaidia TANESCO kulipa yale madeni ili iweze kujikwamua na kuweza kutekeleza majukumu yake kwa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba TANESCO inadai taasisi za Serikali lakini na yenyewe inadaiwa na taasisi kubwa ambayo inaidai TANESCO ni TPDC. TPDC inashindwa kutekeleza miradi yake mingi kwa sababu inapeleka gesi TANESCO na TANESCO anashindwa kulipa na TPDC naye anachukua gesi kwa watu. Kwa hiyo, naomba TANESCO isaidiwe kama tunataka ikimbie, tukiiacha yenyewe itakwenda kila siku ikitambaa. Kwa hiyo, nataka tuiwezeshe TANESCO kwa yale madeni aidha Serikali iyachukue au tuwasaidie kuyalipa au tuwasaidie kukopa ili waweze kujiendesha kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka nichangie ni kwamba tuwe na gas master plan au mpango kabambe wa matumizi ya gesi kwa sababu sasa hivi kila mwekezaji anaweka kiwanda eneo ambalo analitaka yeye. Sidhani kama Serikali itakuwa na uwezo wa kumpelekea kila mtu gesi pale ambapo amejenga kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitenga maeneo maalumu, tukaonyesha mpango kabambe wetu kwamba bomba la gesi litapita katika maeneo haya na yeyote anayetaka kutumia gesi akaweke kiwanda chake katika maeneo hayo, nina uhakika kabisa kwamba ndani ya muda mfupi tutakuwa na uwezo wa kuwafikishia gesi katika viwanda hivyo. Bila kuwapa maelekezo kila mtu akajenga anapotaka mwenyewe, tutakuwa na gesi nyingi lakini tutashindwa kuitumia kwa sababu gharama ya kuwafikishia watu gesi itakuwa ni kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimalizie kwa kuiomba Wizara ya Miundombinu kuunganisha barabara ya kutoka Mtwara - Kilambo kwa kiwango cha lami kwa sababu barabara hii inatuunganisha na nchi majirani zetu Msumbiji. Ni Sera ya Taifa kwamba barabara za Kitaifa ziunganishwe kwa kiwango cha lami. Natambua kwamba tayari kwa upande wa Mtambaswala tumeunganisha lakini watu wengi zaidi wanatumia kivuko cha Kilambo kwa ajili ya kwenda Mozambique kwa sababu ndiyo njia fupi zaidi kuliko upande mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuiomba Serikali wakati wa bajeti mara nyingi hapa tumekuwa na utaratibu wa watu kukataa kila bajeti, lakini inapokuja wakati wa utekelezaji walewale walioikataa bajeti ndiyo wanakuwa wa kwanza kulalamika kwamba kwao haijapelekwa. Mheshimiwa Rais aliomba kula kwa wananchi na alikuwa na ahadi zake na Wabunge tuliomba kura kwa wananchi tulikuwa na ahadi zetu. Kwa hiyo, zile ahadi zetu tutakuja kuulizwa sisi 2020 tumetekeleza kwa kiasi gani.