Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia taarifa za kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Msajili wa Hazina aliyetumbuliwa Ndugu Lawrence Mafuru kwa kazi kubwa aliyokuwa akitushauri mpaka sasa hivi tumeona kuna mabadiliko makubwa sana. Toka kupata faida ya shilingi milioni 443 mpaka tulipata milioni 885.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi pia kupuuza mchango wa mzee wetu ambaye ni msajili wa sasa hivi, tunamshukuru pia. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru sana Wanasheria wetu wanafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba wanatushauri na tunafanya vizuri kuishauri taasisi pamoja na taasisi zinazokuja kwenye vikao vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze na madeni ya Serikali. Ukijaribu kuangalia kwenye taasisi mbalimbali ambazo tumeweza kuziita na kuzikagua tumekuta Serikali inadaiwa fedha nyingi sana. Baadhi ya mashirika mbalimbali yameweza kutoa huduma, lakini Serikali imeshindwa kulipa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiyataja mashirika mbalimbali ambayo yanaidai Serikali ukianza na Mamlaka ya Kuchimba Visima inaidai Serikali karibu bilioni 2.7; ukija Mamlaka ya Maji DUWASA Dodoma hapa inadai Serikali bilioni mbili; ukija SUMA JKT wanaidai Serikali bilioni 5.8; ukija MSD wanaidai Serikali bilioni 144.9; Haya yote ni madeni ambayo Serikali inadaiwa, lakini wananchi wa kawaida wanapokuwa wanadaiwa hata Sh.10,000 wanapigwa penalty na wanakatiwa huduma katika maeneo yao, lakini Serikali imekuwa ikidaiwa na haijali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni madeni ya muda mrefu, si madeni ya siku moja wala ya mwaka mmoja. Haya ni madeni ambayo mengine yana miaka mitano, mengine miaka mitatu, Serikali haitaki kabisa kuhakikisha kwamba, inalipa haya madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhumuni la kuanzisha mashirika haya tulitaka yatoe tija kwenye nchi hii, lakini pia, yaajiri watu wengi, lakini mashirika mbalimbali sasahivi yako katika hali mbaya na yanataka kufa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu na Shirika la Ndege (ATCL). Shirika hili la Ndege ATCL ndani ya miaka mitatu limeendeshwa kwa hasara kubwa kabisa. Shirika hili mwaka 2014/2015, liliendeshwa kwa hasara, lakini matumizi yake kila mwaka yanazidi kuongezeka. Mwaka 2014/2015, walitumia karibu 94,359,000,000/=; lakini mwaka 2015/2016, walitumia bilioni 109.2; na mwaka 2016/2017 wakatumia bilioni 13.7. Fedha hizi ambazo zinatumika tofauti na mapato ambayo yanapatikana ni hatari kabisa kwa mashirika mbalimbali na shirika hili linataka kufa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata maswali mengi sana kwamba, sasa hivi tunaona Serikali inajumua ndege nyingine, maana si kununua ni kujumua; inajumua ndege nyingine kwa ajili ya kuhakikisha kwamba shirika hili linakuwa na ndege nyingi. Sasa nafikiria wamefanya utafiti gani wakati shirika linaendeshwa kwa hasara, halafu Serikali inakwenda kuwekeza fedha nyingi za Watanzania kwenda kununua ndege. Ni namna gani wamefanya utafiti ili shirika hili liweze kuleta tija kwenye nchi hii. Kwa hiyo, hali si nzuri. Shirika linaendeshwa kwa hasara na linaendelea kutumia fedha nyingi kupita kiasi ambacho kinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna shirika lingine, kuna TANTRADE, shirika hili pia limeendeshwa kwa hasara miaka mitatu mfululizo. Shirika hili mwaka 2013/2014, lilitumia fedha milioni 397. 9; lakini mwaka 2014/2015, lilitumia milioni 614.6; na mwaka 2015/2016, likatumia milioni 838.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi haya ambayo yanatofautiana na mapato linayopata shirika hili yamesababisha hasara kubwa kwenye shirika na mtaji wa uwekezaji kwenye shirika hili umeshuka kwa asilimia toka 32.7 hadi 16.5, ni hatari sana. Ni kwamba, mpaka sasa hivi usimamizi wa mashirika haya umeonekana kwamba Wakurugenzi pamoja na bodi ambazo zinachaguliwa zimeshindwa kusimamia mashirika haya na Serikali isipochukua hatua mashirika haya yanakwenda kufa na kupotea kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo lingine, nataka kuzungumzia pia, kuhusiana na sheria mbalimbali ambazo zinaendesha mashirika yetu. Kwa mfano, Sheria ya Manunuzi; ukiangalia MSD sasa hivi Sheria ya Manunuzi inaathiri sana shirika hili. Sheria ya Manunuzi inafika mahali MSD ili waweze kupata dawa wanatumia miezi mitatu kutangaza zabuni, lakini pia inasababisha dawa zichelewe kufika nchini, zaidi ya miezi tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni jambo la kuangalia sana kwamba. Hivyo, ni muhimu Serikali ikajaribu kuangalia Sheria hizi za Manunuzi zimekuwa ni tatizo katika mashirika haya na yanashindwa kuendelea na kufanya vizuri kwa sababu ya sheria kandamizi ambazo zipo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu shughuli mbalimbali ambazo zinafanyika kwenye mashirika haya. Ukijaribu kuangalia mashirika mbalimbali katika nchi hii hayana bodi. Ukiangalia Shirika la MSD Bodi yake sasa hivi imekwisha muda wake karibu mwaka mzima umepita, lakini mpaka sasa hivi hakuna jambo lolote ambalo linaendelea kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, bodi hizi zinateuliwa upya na kuhakikisha kwamba, zinafanya kazi kwa kusaidia mashirika haya ili yaweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.