Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama hapa na kuchangia katika taarifa za Kamati hizi mbili. Labda niseme tu kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, vilevile nilikuwa kwenye Kamati Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia kuhusu Serikali za Mitaa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya LAAC kuna maeneo ambayo yamezungumzia kuhusiana na kukaimu kwa Wakuu wa Vitengo au Wakuu wa Idara kwa muda mrefu. Naungana na wale wanaosema kwamba hili ni tatizo, kwa sababu unakuta Mkuu wa Idara anakaimu nafasi zaidi ya miezi sita inafika mpaka miaka mitatu wakati mwingine. Hii inapunguza uwezo wa kujiamini kwa Mkuu wa Idara pia anakuwa hana mamlaka kamili ya kusimamia au kutoa amri na maelekezo katika baadhi ya mambo. Kwa hiyo, naishauri Serikali katika hili baadhi ya taratibu zifuatwe ili wanaokaimu wasikaimu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu wapo watu wengi ambao wanazo sifa za kuwa Watumishi au Wakuu wa Idara kamili lakini kwa muda mrefu wanakaimu, hivyo hilo naomba lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni ucheleweshwaji wa ruzuku kutoka Serikali Kuu. Nashauri kwamba hakuna haja ya kuchelewesha ruzuku kwa sababu Halmashauri hasa ukizingatia baada ya kunyang’anywa baadhi ya vyanzo vya mapato zimekuwa hazina fedha, Kwa hiyo ruzuku inayotoka Serikali Kuu ndiyo inayofanyiwa kazi na Halmashauri zetu hivyo isicheleweshwe ili Halmashauri zikamilishe miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni unyang’anywaji wa property tax na mabango ya biashara kwa Halmashauri zetu. Kwanza napenda niseme tu kwamba Serikali za Mitaa nazo ni Serikali, kwa sababu kwa ufahamu wangu najua kuna Central Government na Local Government, sasa hizi Serikali za Mitaa zina majukumu ya kutoa huduma na kutimiza wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi, sasa tumezinyang’anya property tax pia tumechukua na mabango ya biashara, yote yamekwenda TRA. Nashauri kwamba turudishe property tax, turudishe mabango ya biashara katika Halmashauri zetu ili ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi ya maendeleo kama vile vituo vya afya, kuna zahanati pia kuna miradi ya madarasa na mambo mengine kadha wa kadha ambayo kama tutazirudisha property tax na mabango ya biashara Serikali za Mitaa zitaweza kufanya kazi kwa ukamilifu na kuwapa huduma bora wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni matumizi mabaya ya fedha za umma ambapo katika Halmashauri inabidi zisimamiwe kikamilifu. Pamoja na kupeleka fedha bila ya kuzisimamia ipasavyo itakuwa ni sawa na kazi bure. Kama wataalam wanavyosema the power without control is nothing. Kwa hiyo, lazima tunavyopeleka pesa tuzisimamie. Tuhakikishe kwamba zinafanyiwa ukaguzi na wale ambao wanapata hati chafu na hati zenye mashaka nao wajieleze kwa nini wanapata hati hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia katika Serikali za Mitaa ni mikataba ya upimaji wa viwanja. Mara nyingi upimaji wa viwanja umekuwa unatumia fedha nyingi lakini haukamiliki kwa wakati. Sasa tutoe maelekezo kwa Wizara kwamba wahakikishe pale ambapo Halmashauri inataka kupima viwanja, viwanja vipimwe kwa wakati na wananchi wauziwe bei nafuu ili kila mmoja aweze kupata kiwanja na ajenge nyumba bora ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie sasa katika Kamati ya PAC. Katika Kamati ya PAC kuna taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo imeishia tarehe 30 Juni 2016, taarifa hii imeeleza upungufu mwingi. Miongoni mwa upungufu uliojitokeza ni utekelezaji wa miradi iliyofanyika bila ya tija na kusababisha hasara kwa Serikali. Pia kuna dosari zilizojitokeza katika usimamizi wa miradi, kutokuwepo kwa nyaraka za malipo kwa baadhi ya taasisi na Wizara na Mashirika ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna upungufu wa kutokuzingatiwa kwa Sheria za Manunuzi ipasavyo, dosari katika usimamizi wa mikataba na ufanisi mdogo wa mabenki ya umma ukilinganisha na mabenki binafsi pia kuna kutokuzingatiwa kwa Sheria ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kulizungumzia ni taarifa ya kwamba hadi Juni 30, 2015 kuna Maazimio nane tu ambayo ni sawa na asilimia 64.2 kati ya maazimio 14 ambayo ndio yametekelezwa, lakini kuna mengine Sita ambayo ni sawa na asilimia 35.8 haya bado hayajatekelezwa. Nafikiri ipo haja Serikali kuhakikisha maazimio haya yanatekelezwa yale ambayo yamebaki ili kuweza kuisimamia Serikali, Bunge linapotoa maelekezo kutokana na maelezo ya taarifa za Kamati, basi maelekezo yale yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ipo taarifa kwamba Serikali kutokulipa kwa wakati madeni ambayo imechukua au imekopa kutoka katika Mifuko ya Jamii. LAPF wanaidai Serikali shilingi bilioni 243.43, WCF inaidai Serikali shilingi bilioni 26.6, PPF inaidai Serikali shilingi bilioni 139.5, PSPF inaidai Serikali bilioni 623. 93, NSSF inaidai Serikali bilioni 519.05, NHIF inaidai Serikali bilioni 43.8 jumla ya madeni haya yote ni takribani trilioni 1.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa Mifuko ya Kijamii ambayo jana tu tumepitisha sheria hapa kwamba iunganishwe kwa pamoja, lakini sasa kama fedha hizi hazitalipwa au zitakaa kama deni kwa Serikali kwa muda mrefu, hii Mifuko itajiendeshaje? Matokeo yake ndio tunaposababisha watumishi wanapostaafu kukaa kwa muda mrefu wakisubiri mafao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niishauri Serikali katika hili, haraka iwezekanavyo ilipe madeni haya ya Mifuko ya Jamii, au kupitia kikao hiki Serikali ituambie baada ya jana kupitisha sheria ya kuunganisha Mifuko hii ya kijamii hadi lini Serikali itakuwa imelipa deni hili la shilingi trilioni 1.59. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naliona ni kutoanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Fund) nao pia Serikali ituambie, kwa sababu hii ilikuwa ni katika mapendekezo na maazimio ya Bunge letu ni lini Serikali itaanzisha hii Public Investment Fund.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni hali ya kifedha ya Mfuko wa PSPF kutoimarika ipasavyo. Hii nafikiri kwa upeo wangu ni ile kutokana na kuikopesha Serikali na Serikali kutolipa kwa wakati. Kwa hiyo nashauri Serikali ilipe madeni haya kwa wakati. Kingine pia ni usimamizi duni wa mikataba katika Wizara na Mashirika ya Umma. Mikataba yetu imekuwa na matatizo mengi na yote hii ni kwamba tuonawapa mamlaka na tunaowapa dhamana wanaona labda kwa sababu si mali yao, siyo taasisi zao binafsi ndiyo maana hawasimamii ipasavyo. Naishauri Serikali pale mtu anapofanya uzembe katika Idara yake au katika Wizara yake kama kuna mkataba mbovu mtu huyo awajibishwe moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ninalotaka kulizungumzia ni kutokukamilika kwa uzingatiaji wa Mfumo wa Kihasibu (IPSAS) accrual basis, hili ni tatizo, kwa sababu kama tunashindwa kusimamia mifumo na kuikamilisha tutasababisha ufisadi mwingi katika Halmashauri zetu. Ni bora hii mifumo tuisimamie lakini mifumo hii pia tuhakikishe inakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumzia ni baadhi ya Taasisi za Umma kutofuata Sheria za Manunuzi, ndiyo maana katika taasisi zetu za umma kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za Serikali. Kwa mfano hata katika ununuzi wa samani tu kwa sababu hatusimamii vizuri, kwa sababu hatufuati Sheria za Manunuzi matokeo yake imekuwa kila mwaka tunabadilisha samani au kila mwaka rasilimali au vyombo vya Serikali vimekuwa havina ubora unaostahili na tunaagiza vyombo vipya, tukijua ni matumizi makubwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumzia ni dosari katika mkataba wa Mlimani City na Mlimani Holdings Limited. Katika taarifa iliyosomwa hapa na Mwenyekiti wetu Mama Naghenjwa Livingstone Kaboyoka ameeleza upungufu mwingi sana katika Mkataba huu. Nami niungane na mchangiaji aliyesema kwamba, takribani miaka 17 sasa imepita, ubadhirifu unaendelea, miradi haikamiliki lakini watu walikuwa wako kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama inafika mahali wanaingia mkataba mbovu kama huu, tutegemee nini? Kwa sababu katika Vyuo ndiko wanapotoka wasomi ambao ndiyo wanaokuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, wanakuwa Makamishna, lakini leo hapohapo ndipo pana ubadhirifu na kumeingiwa mkataba mbovu. Sijawahi kuona katika mradi kama huu mkubwa kwamba eti Mwekezaji anatakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 inatakiwa Mwekezaji aoneshe mtaji wa namna gani anaweza kuendesha ule mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi wa Mlimani City Mwekezaji ameonesha Dola za Kimarekani 75 ambazo ni sawasawa na shilingi 150,000 lakini mkataba huo ukaingiwa. Sasa huu siyo wizi wa mchana kweupe? Bahati mbaya haya yametokea Serikali iko kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC kama nilivyosema, tumeanza kupigia kelele haya tangu mwaka jana na tukawaita baadhi ya Maafisa wa Chuo Kikuu vilevile tukatoa taarifa kwamba mkataba wa Mlimani City una upungufu, tulikitegemea tangu
kipindi hicho angalau wangefanya marekebisho. Hadi leo hii nazungumza hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwamba katika mradi au mkataba wa Mlimani City pamoja na Mlimani Holdings bado Serikali inatakiwa kufanya kazi kubwa katika hili na kupitia Bunge hili tutoe maelekezo kwamba waliohusika na mkataba ule Serikali iwachukulie hatua za kisheria haraka na mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumza ni ukiukwaji wa malipo ya land rent ambapo UDSM ilitakiwa ipate asilimia 10 ya pango kwa mapato ghafi, badala yake UDSM inalipwa baada ya kutoa gharama, wao wanalipwa asilimia 10 wakati walitakiwa walipwe kabla ya kutoa gharama. Kwa hiyo, ukiuangalia kwa undani mkataba huu wa Mlimani City na Mlimani Holdings pana uchafu mkubwa umejificha hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza CAG kwa kuibua uchafu na ubadhirifu katika mkataba ule, lakini kama CAG ndio jicho letu Wabunge anatuletea taarifa na Serikali haichukui hatua, itafika mahali tutamchosha CAG. Serikali imwezeshe kwa kumpa bajeti anayotaka kwa asilimia 100 lakini yale anayotuletea tusioneane haya, Waswahili wanasema ukicheka na nyani utavuna mabua. Kupitia Bunge hili nataka waliohusika wote katika mkataba ule wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe ni funzo na fundisho kwa wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi wa Dege Kigamboni au Dege Eco Village, kuna taarifa kwa kweli zinatia kichefuchefu, kuambiwa kwamba kuna kiwanja Kigamboni kinachoweza kufikia milioni 800 cha makazi ya kawaida. Hili naona halitakiwi kufumbiwa macho. Katika hili kwa kutokana na muda ni kwamba mkataba wa NSSF wana asilimia 45 ya hisa na hawa AHER au Azimio Holdings…

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, naomba umalizie sentensi yako.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Nimalizie kwa kusema kwamba mkataba wa Dege Eco unatakiwa ufanyiwe kazi lakini vilevile pia kupitia Bunge hili, taarifa ya mabaya yote yaliyoibuliwa katika taarifa ya PAC na LAAC Bunge lako lichukue hatua za kinidhamu na lichukue hatua za kisheria. Ahsante.