Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kwa mwaka huu naomba niwatakie Waheshimiwa wote heri ya mwaka mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la Halmashauri na Uongozi kwenye halmashauri na kikubwa nitaomba, usikivu wa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, kwamba kama kuna changamoto kubwa ambazo taarifa ya Kamati imeziainisha, kukusanya mapato madogo, kutopeleka fedha za asilimia 10 na mengine. Changamoto kubwa tuliyonayo ni aina ya Wakurugenzi tulionao kwenye Halmashauri zetu. Uwezo na utendaji kazi wa Wakurugenzi wa nchi hii kwa sasa ni kikwazo kikubwa sana kwa maendeleo ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama utaamua kufanya assessment ya kupima performance ya Wakurugenzi wako ni sehemu kubwa ya watu wanaokuangusha wewe na wanaoingusha Serikali kwa sababu ya uwezo wao. Hii imetokana na namna walivyopatikana, kama ingekuwa Wakurugenzi walipatikana kwenye mfumo ule wa kawaida wa Watumishi wa Umma huu upungufu mwingine usingekuwepo leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo ambalo nataka niliseme kama kuna jambo ambalo nilifikiria ningeliona kwenye taarifa ya Kamati na hii ni challenge kwa Kamati ya LAAC kwamba Kamati ingekuja na mapendekezo ya kushauri Bunge, liishauri Serikali namna ya upatikanaji wa Wakurugenzi, Wakurugenzi walioteuliwa na Mheshimiwa Rais wengi uwezo wao wa ufanyaji kazi ni mdogo hauendani na majukumu yaliyopo kwenye Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukamhoji Mkurugenzi namna anavyofanya kazi wewe mwenyewe unajiuliza kwamba huyu hivi tangu lini amekuwa Mtumishi wa Umma. Huko kwenye Halmashauri kuna migogoro mikubwa kati ya Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa sababu Wakuu wa Idara wana-perform vizuri kuliko Wakurugenzi. Haya wote mnayashuhudia kama Waheshimiwa Wabunge mnashiriki kwenye vikao vya Halmashauri vya Madiwani kwenye Mabaraza kule wote mtakuwa mashahidi. Aina ya Wakurugenzi wetu ni wana-perform vibaya mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulitakiwa tuanzie hapa, siku moja nilipokuwa namsikia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anasema tutajenga viwanda 100 kwenye kila Mkoa nilikuwa najiuliza kwamba hao watu wenyewe wa kusimamia wako wapi. Yaani jambo moja ambalo lili-click kwenye kichwa changu hao watu wenyewe wa kusimamia wako wapi. Pale kwangu kuna watu wametaka kuja kuanzisha viwanda tangu mwaka jana mwezi wa Tisa mpaka leo kupewa ardhi tu ile watu watatu, wanataka kuja kuanzisha viwanda vya kuchakata muhogo mpaka leo watu watatu Mkurugenzi ukimuuliza anasema sijui kitu gani hakijakamilika najua ni kwa sababu ya performance uwezo walionao ni mdogo kweli. Hilo jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu suala la miradi ya maji hususani ile ya vijiji 10 kwenye kila Halmashauri pamoja na miradi ya umwagiliaji. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kama kuna jambo ambalo nchi hii Serikali imepata hasara kubwa ni kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji kwenye Halmashauri na nafikiri more than 70% ya ile miundombinu sasa haifanyi kazi. Kamati ilitakiwa ije na ripoti ituambie kila halmashauri ni halmashauri gani angalau imefikia 50% hakuna, angalau kama kuna miradi ilianzishwa vijiji 10 ya maji ambayo imeweza kuitekelezeka kwa asilimia 50 kwenye Halmashauri hakuna. Huu ni uthibitisho kwamba kuna fedha zimetumika vibaya na kuna fedha zililiwa vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la msingi sana kwenye Halmashauri na hili nilivyokuwa nalifikiria nikaona kwamba, kama kuna uwezekano labda wale Wakuu wa Idara ya Maji labda waondoke kuwa monitored na TAMISEMI ili wawe moja kwa moja kwenye Wizara ya Maji ama watoke Wizara ya Maji waende moja kwa moja TAMISEMI. Hapa naona kuna-contradiction namna mnavyofanya kazi, inawezekana namna ya upelekaji wa maagizo yanakwenda yanawachanga wale watu, kwamba Wizara ya Maji wanaweza kusema hivi TAMISEMI ikasema, ikapelekea kukawa na shida kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naamini kuna miradi mingi ya maji ilianzishwa tena kwa lengo jema na Serikali kule kwenye halmashauri miradi ile haifanyi kazi. Halafu hakuna continuation hakuna mwendelezo leo unaweza ukakuta limeanzishwa hili kesho lile halijakamilika linaenda kuanzishwa lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mradi pale ulijengwa na TAMISEMI tena lambo la kunyweshea mifugo, ulijengwa uligharimu karibu milioni mia mbili haujakamilika, haufanyi kazi tumeenda mwaka huu kwenye bajeti ya halmashauri unaenda kuanzishwa tena mradi mwingine ambapo hata huu wa kwanza haujakamilika. Sijui kama TAMISEMI wanajua, sijui hiyo Wizara yenyewe ya Mifugo inajua kwa sababu naona kama mambo yanajichanganya changanya tu. Hilo jambo lingine ambalo ni la msingi sana nilitaka nilizungumzie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu katika ukurasa wa 65 wa kitabu cha LAAC Kamati inaomba Bunge kuazimia kuunda Kamati Maalum ya Bunge itakayochunguza sababu na chanzo cha tatizo la miradi ya maji kutotekelezwa. Ndiyo hili nilikuwa nalisema kwamba, kama Bunge litaona inafaa naunga mkono hoja hii kwamba Bunge liunde Kamati ipitie kwenye kila Halmashauri, ikachunguze ni miradi mingapi ya maji ilianzishwa ile ya vijiji 10 pamoja na umwagiliaji iliyoanzishwa na TAMISEMI, tuone mingapi inafanya kazi na mingapi haifanyi kazi. Katika hii tutagundua madudu mengi kweli kweli kwa sababu Halmashauri nyingi hazijatekeleza vizuri hili suala. Kwa hiyo, naomba niunge mkono hili suala la kuunda Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Halmashauri kutokupewa pesa kwa wakati, wakati mwingine haya yote tunayasema kwamba Wakurugenzi hawafanyi kazi, uwezo wao mdogo ni kweli, lakini jambo lingine kwamba hizo fedha zenyewe za kufanyia kazi wanazipata wapi. Unakwenda kwenye halmashauri leo mwezi huu tupo karibu kwenye quarter ya tatu unakuta fedha za development kutoka kwenye Serikali Kuu labda wamepata asilimia 15, asilimia 20 unajiuliza sasa huyu Mkurugenzi hapa anafanya kazi gani kwa sababu upatikanaji wa fedha kutoka Serikali Kuu ni kikwazo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha bahati yupo hapa alieleze Bunge tatizo ni nini. Leo kwenye Halmashauri tunapitisha bajeti kwa ajili ya Mwaka wa Fedha 2018/2019, fedha za mwaka 2017/2018 hazipo, fedha za maendeleo hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalokwamisha maendeleo kwenye Halmashauri zetu ni Serikali Kuu kutopeleka fedha kwenye halmashauri zetu.

Jambo hili ni hatari linaua moja kwa moja Halmashauri ya Wilaya. Leo tunalaumu fedha za asilimia 10 haziendi, halmashauri inapewa maagizo ya kutumia fedha hizi za ndani kwenye kuajiri watumishi. Nimesikia hapa leo mmoja wa Waziri anajibu kwamba halmashauri itumie fedha za ndani kuajiri watumishi. Fedha hizi ambazo zingepaswa kupelekwa kule kwa vijana zile asilimia 10 kwa wanawake na walemavu, leo Waziri anakuja kusimama anatolea agizo waajiri watumishi

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo lingine ambalo linakwamisha ni suala la fedha kutoka Serikalini ziende kwenye halmashauri na jambo hili pia linapelekea halmashauri kuwa na mzigo mkubwa kwa sababu hata yale mapato yetu ya ndani ambayo asilimia 60 tumepanga kupeleka kwenye maendeleo, tunaondosha tunapeleka kwenye maeneo ambayo yalipaswa yagharamiwe na fedha za Serikali Kuu. Kwa hiyo, hili ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilimalizie ni kuhusu suala la Halmashauri kukosa mapato ya ndani kadri tulivyopanga. Unakuta tumepanga tukusanye labda milioni 300 kutoka kwenye mazao ya wakulima kwa mfano mbaazi. Halmashauri yetu sisi ambayo mbaazi ni chanzo kikubwa cha mapato tunashindwa kukusanya ule ushuru kwa sababu mbaazi imekosa soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna jambo ambalo lingine ni la msingi sana ni Serikali kujielekeza katika kutafuta masoko ya mazao ya wakulima kwa sababu mazao yakikosa soko halmashauri hazipati pesa za kujiendesha. Kwa hiyo, leo mbaazi inauzwa mpaka Sh.150, Sh.200 halmashauri hii itatoza ushuru wa shilingi ngapi kwa mkulima ili ipate mapato yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la Serikali kutafuta masoko sio jambo la blaa blaa linalohitaji majibu mepesi ni jambo la lazima kwa sababu Serikali ipo kwa ajili ya wananchi na wananchi lazima watafutiwe masoko na Serikali iwahudumie wananchi wake, lisiwe jambo sasa la kuja hapa fulani amesema hivi, hili Lindi hawataki, tunahitaji majibu ya kweli kwamba mtu akilima mbaazi zake apate soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.