Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa ya kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019, awali ya yote nitoe shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Rais kumaliza miaka miwili na nimshukuru kwa kuendelea kuniamini nipige filimbi ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake kwa mpango mzuri ambao ninauafiki. Kwa sababu sitaki kufanya kazi ya kuwasomea watu, kila Mbunge anapaswa kusoma, nitatoa ufafanuzi kidogo juu ya mambo ambayo watu wanayaelewa ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kukariri dhima ya mpango wa pili wa miaka mitano. Dhima ya mpango wa pili wa miaka mitano ni ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Rafiki yangu Mheshimiwa Ummy amezungumzia maendeleo ya watu ambayo yanajikita kwenye elimu, yanajikita kwenye afya, yanajikita kwenye kipato. Sasa mageuzi ya kiuchumi, huu mpango ambao nauunga mkono ni sehemu ya ule mpango mrefu wa miaka mitano ambayo naiunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda tunavyovilenga, nimesikia hoja watu hawajajua mpaka leo viwanda tunavyovijenga. Sitaki kuwasomea watu lakini kwa faida, viko viwanda vya makundi manne na vyote tumevishughulikia. Kundi la kwanza ni viwanda vinavyochakata mazao au malighafi ya wananchi, katika kuhamasisha ni jukumu la viongozi wote na wananchi wote, ninapopiga filimbi nawategemea na ninyi Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuhamasisha zile malighafi tuzijengee viwanda.

Kundi la pili ni viwanda ambavyo vinaajiri watu wengi. Yupo Mheshimiwa Mbunge ameniambia kwa nini usilete viwanda vya teknolojia ya juu, hapana! Watanzania wote hawawezi kuendesha mitambo ya teknolojia ya Juu, Watanzania wote hawawezi kuendesha LNG Plant, kwa hiyo, nitaendelea kutengeneza viwanda vinavyoajiri walio wengi ili kusudi wale wenzangu na mimi ambao waliishia darasa la saba na darasa la kumi waweze kutumika pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi la tatu ni viwanda ambavyo malighafi zake, bidhaa zinazozalishwa zinatumika sana. Katika kundi hili tumefanya vizuri sana katika viwanda ambavyo nilianzisha. Tuna uwezo uliosimikwa wa kuzalisha saruji tani milioni 10.8, tunatumia mahitaji yetu tani milioni
4.87 kwa hiyo tuna uwezo wa kuzalisha kuliko ambavyo tunahitaji kama nchi. Tuna mahitaji sasa ya kujenga viwanda vya tani milioni 10 Sinoma Tanga lakini kuna viwanda vinakuja Chalinze, Mamba na mwenzake Nyati wanaweka viwanda vya tani milioni tatu pale. Kwenye hiyo industry ya bidhaa zinazotumika sana tumefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi la nne ni kutumia malighafi ambazo tumepewa faida na Mwenyezi Mungu ya kipekee ndiyo inaangukia suala la viwanda vya mbolea inayotumia gesi. Niwaeleze Waheshimiwa Wabunge mmelizungumza, Ferrostaal ameshapewa clear line na Wizara ya Nishati kwamba atengeneze mbolea. HELM ya Mtwara na ninyi njooni mjadiliane tuko tayari mzalishe mbolea. Tunapojenga Bagamoyo Special Economic Zone viwanda 190 kiwanda kimojawapo kitakuwa cha kutengeneza mbolea. Kwa hiyo, hivyo ndivyo viwanda tunavyoshughulikia. Sasa uhamasishaji ni jukumu lako mimi nikiwa nimetangulia kusudi tujenge Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio tuliofanikiwa, tumepata mafanikio. Fanikio moja kila Mtanzania sasa anaimba viwanda. Nchi yote watu wanaimba viwanda na nilifikiria wakati huo nitoe dhana ya isiyokuwa. Unapozungumza Watanzania, kwa mfano viongozi tunazungumza Watanzania kuanzia ngazi ya kwanza ngazi ya juu, ndiyo maana mimi kiwanda kidogo hata vyerehani vinne naendelea kusema ni viwanda vidogo. Kwa hiyo, usijitambue wewe nafasi yako kwa sababu unazo, lazima tuwalee Watanzania wadogo mpaka wale Watanzania wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa faida ya yule aliyeuliza swali, viwanda vidogo sana vinaajiri mtu mmoja mpaka wanne na capital yake ni shilingi milioni tano. Cherehani industrial kinauzwa shilingi milioni 3.5 na kinaweza kukutengeneza kipato cha kukutosha wewe na familia yako. Vipo viwanda vidogo vinaajiri watu watano mpaka 49 na mtaji wake ni shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 200. Hivi ndiyo vile viwanda vya kuchakata nyanya, viwanda vya pilipili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vya kati vinaajiri watu 50 mpaka 99, vinaanzia shilingi milioni 200 mpaka shilingi milioni 800. Kuna viwanda vikubwa milioni 800 na vinaajiri watu 100 na kwenda zaidi. Hiyo ndiyo naihubiri kwa Watanzania walio wengi. Nikienda kwa wale wenye nazo; kiwanda kidogo wanasema ni shilingi bilioni mbili lakini tunahimiza viwanda vidogo na ukisoma Mpango wa Mheshimiwa Mpango anakuambia SIDO itapewa kipaumbele cha kuongoza katika ujenzi wa viwanda, kwa sababu tunatambua kwamba wananchi walio wengi wataweza kupata faida kwa kushiriki katika kuchakata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze Waheshimiwa Wabunge katika ujenzi wa viwanda sekta inayoongoza ni ya uchakataji (manufacturing) wanaita mediating sector, tunataka tuwalee Watanzania watoke katika uchuuzi wawekeze katika kuchakata katika kutengeneza viwanda. Pale ulipo, uangalie zile factor zinazokuwezesha uweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ule mpango wa pili wa miaka mitano nafasi ya sekta binafsi ndiyo mhimili kwa hiyo msitegemee Serikali ihamasishe, sekta binafsi ihamasishe, ni jukumu lenu ni jukumu langu na sekta binafsi ndiyo itafanya hayo mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala ambalo kuna watu wamedokeza nawaheshimu sana rafiki zangu, nitawapiga taratibu. Watu wanasema kwamba Serikali haina mahusiano mazuri na sekta binafsi. Hamna taarifa, Serikali inakutana na sekta binafsi na jana wanaosikiliza taarifa za kiingereza katika kipindi cha This Week In Perspective wamesema wenyewe watu wa Tanzania Private Sector waliokuwa pale kwamba mahusiano ni mazuri sana mpaka Mheshimiwa Rais anawaita wafanyabiashara anazungumza nao. Ila ni kwamba kuna paradigm shift, mambo yamebadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza viwanda ili moja; tutengeneze ajira, tunatengeneza ajira, mbili; tuzalishe bidhaa zenye ubora kusudi tuweze kutosheleza mahitaji ya Watanzania na kuuza nje. Lakini tunatengeneza uchumi wa viwanda na viwanda ku-broaden ile tax base. Mwisho yote haya mawili ukiyatengeneza utakwenda vizuri. Lakini mwisho lazima umuone Mzee wa mpango uweze kumpa chochote. Kilicho cha Yesu mpe Yesu na cha Kaisari mpe Kaisari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie masuala maalum. Limezungumzwa suala la Mchuchuma na Liganga. Amezungumza Mheshimiwa Mpango, Mchuchuma na Liganga naisimamia mimi na ni suala la muda. Ile sheria mliyoibadilisha Bungeni ya kuhusu rasilimali zetu tupate kiasi gani inahusu Mchuchuma na Liganga. Nikishamaliza mambo yangu, mwekezaji tayari ana pesa ya fidia anaanza na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la EPZA watu wanasema tunatumia utaratibu ambao hautumiki dunia nyingine, ndiyo! Mambo mengi tunayofanya Tanzania hayatumiki sehemu nyingine, kama la kuwakoromea wale watu wa makinikia, Marais wachache wanaweza kuwakoromea, kwa hiyo, kuna mambo ni ya kwetu kwetu tu! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika kwenye EPZA, tumekubaliana na wawekezaji wa Bagamoyo waje walipe fidia tutengeneze ile Bagamoyo Special Economic Zone. Bagamoyo Sepcial Economic Zone Januari inaanza na nitatengeneza viwanda 190 kwa kuanzia. Tutaharakisha viwanda hivi mwaka 2020 viwe vimeanza. Mwaka 2020 kuna shughuli lazima nihakikishe kwamba viwanda vile vipo ili kusudi niweze kuonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee. Suala lingine specific la uhusiano kati ya sekta ya kilimo na viwanda. Waheshimiwa Wabunge, Serikali (mimi ndiyo napiga filimbi) lakini siwezi kufanya kazi bila kilimo, bila mifugo, bila TAMISEMI, bila miundombinu na miundombinu wezeshi ndiyo maana nahitaji umeme, nahitaji maji, nahitaji reli, nahitaji barabara. Ukijumlisha hayo ndiyo yanaitwa uchumi wa viwanda halafu mimi nakuja najenga viwanda.

Kwa hiyo, wanaosubiri milingoti ya viwanda ukiona reli inajengwa, viwanda vinakuja. Ukiona mabomba ya maji viwanda vinakuja, ukiona umeme unavutwa viwanda vinakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo mahusiano. Serikali ihakikishe upatikanaji wa soko la mazao. Hapa ndipo kuna kazi. Nimei-position kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri, nai-position Wizara yangu. Wizara yangu imepewa mandate mpya ya kuhakikisha tunatafuta masoko ya mazao, yawe kilimo, yawe wapi ni kazi yangu mpya katika hii awamu mpya kuhakikisha ninapata soko la mazao na nitatoa mwongozo zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda vya kuchakata mazao nimelizungumzia katika zile sekta tatu, watu wanauliza mbona nyama haijazungumzwa? Katika mazao ya wananchi mifugo ni mazao ya wananchi ndiyo viwanda category number one. Viwanda vya mbolea vya Ferrostaal na HELM nimevizungumzia ni kiasi cha kusubiri vinakuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamasishaji nimezungumza ni jukumu la sisi wote. Viwanda vilivyokufa tunavifufua na hakuna mjadala. Atakayeshindwa ampe mwenzake na tunahakikisha suala hilo tunalifikiria. Ukisoma Vision 2020 inaelezea kwa nini tulishindwa lakini ukisoma Mpango wa Pili unakueleza kwa nini hatutashindwa. Import substitution come export promotion ni mojawapo ya hatua nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sekta ya sukari na nizungumze kuhusu Mheshimiwa Mchengerwa. Wale wawekezaji wako watatu siku zao zimehesabiwa, hatutaki watu kuatamia maeneo ya ardhi. Tutashirikiana Wizara ya Ardhi na ile ya Kilimo kuhakikisha kwamba tunazalisha sukari ya kutosha. Watu wa SADC wametusaidia kupata uwezo wa kuzalisha sukari bila kuingiliwa. Tanzania tuna uwezo wa kuzalisha tani milioni mbili kwa mwaka kwa kutumia mabonde yetu yote yaliyopo. Mheshimiwa Rais alipokuwa Kagera ametoa ultimatum kwa wenye viwanda waongeze uzalishaji na hilo mimi nalisimamia. Kwa hiyo, msiwe na wasiwasi tutazalisha sukari lakini uzuri wa sukari uzalishaji wa sukari unatengeneza ajira nyingi. Kwa hiyo, Kigoma kwetu kule nitapeleka viwanda viwili kusudi watu wa Kigoma badala ya kwenda mbali mkate miwa kwenu na mambo yawanyokee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utendaji wa Wizara nimeshazungumzia naipanga upya, lakini jukumu la SIDO kwenye mpango ndiyo inatangulia na niwaambie naanza na Mkoa wa Geita, Katavi, Simiyu, kote huko naweka ma- shade mpya. Kwa hiyo, nataka kuwaonesha tunatengeneza shade, dada tulia na Kagera nitaweka, tunatengeneza shade ambazo mtu unachakata unakwenda pale, ma-shade ninayokujanayo ni mapya, unapewa shade, unafundishwa na namna ya kuchakata, ukihitimu unatoka na kitu chako. Ni miaka miwili, mwaka wa tatu mtaona wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitambue mchango wa Mheshimiwa Saada. Na mimi nitazungumza na counterpart wangu wa Zanzibar namna ya kuweza kuchakata ile karafuu kuiongezea ubora. Napenda kutumia fursa hii kuwaambia kwamba watumie wataalam wangu, SIDO tutaiongezea uwezo iweze kufanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie mchango wa Mheshimiwa Mbowe, aliyezungumza kwamba hatuna sera na kwamba tutengeneze sera moja, huwezi kutengeneza sera moja, sera zote zilizopo ni nzuri. Ile mnayoiita fast tracking ni kuharakisha na fast tracking strategy maana yake ni nini, ni kuondoa vikwazo. Tunayo hiyo na tunayo blue print ambayo ukisoma Easy of Doing Business tuko poorly ranked, sasa kwa sababu tuko poorly ranked tumejitambua sisi tukatengeneza blue print, ile blue print ndiyo inakwambia kasoro yako, usichelewe kutoa kibali, nenda kalipe kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale wanaposema tumepimwa vibaya hata kutolipa kodi wazungu wanatuona ni kasoro. Kwa hiyo, kama mnasema Easy of Doing Business tunarudi nyuma ni kwa sababu watu hawalipi kodi. Sasa huwezi kunihukumu Mwijage eti nimerudi nyuma kwenye Easy of Doing Business ni kwa sababu watu hawakulipa kodi. Hawa watu nitaendelea kuwabembeleza mimi kusudi walipe kodi niendelee kupata ranking nzuri. Kwa hiyo, mikakati iliyopo ni mizuri ila kama mtu anataka nije nimsomeshe, nimwelekeze taratibu, mikakati ile inatosha na niwahakikishie Tanzania sasa tuko kwenye viwanda, siyo kwamba tutajenga viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tutakwenda vizuri, Mpango uko vizuri.