Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kusimamia sekta ya kilimo hapa nchini. Pia niwashukuru sana viongozi wetu wakuu wa Serikali, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa uongozi wao wanaonipa ili kutekeleza majukumu yangu sawasawa. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniletea Msaidizi katika shughuli Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa naamini kwamba tutafanya kazi vizuri kwa matarajio ya waliotuteua na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa kuleta huu mpango ambao kwa kweli unatoa dira ya namna uchumi wa pamoja unavyoweza kwenda na tukafikia hilo lengo letu la kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe kutumia nafasi hii kuishukuru sana Kamati ya Kilimo, Mifugo, Maji na Uvuvi kwa sababu wamekuwa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu yetu. Wametushauri na tumesikiliza ushauri wao, wametuelekeza na tumetekeleza maelekezo yao. Pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia kwa namna moja au nyingine kuhusu mambo ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati yetu, ratiba ya Bunge iliyokuwa imetolewa ilikuwa tuanze kuwasilisha taarifa za Wizara tarehe 30 mwezi uliopita, lakini kwa unyeti wa jambo la mahindi, Kamati ilituita mapema zaidi tarehe 25 ili tujadili suala la mahindi kwa udharura. Wapo wananchi wana mahindi, hawawezi kuyauza kwa sababu ya bei kushuka na kwa hivyo wanashindwa kuingia katika cycle nyingine ya kilimo kwa sababu hawana fedha kwa ajili ya pembejeo na maandalizi ya mashamba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kutokana na mjadala katika Kamati, ndipo Serikali tulisikia na tukachukua pia hatua za kidharura tukaelekeza Wakala wetu wa Mazao (NFRA) waanze tena kwenda kununua katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa, tukajipiga piga pesa ikapatikana ya kuanzia na tunaendelea ku-mobilize funds ili waendelee kununua katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi wapo wameanza manunuzi katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma lakini pesa tena tulikuwa tunazungumza na Waziri wa Fedha nyingine imepatikana sasa wataanza pia kununua katika Mkoa wa Rukwa na baadae wataingia katika Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, hizi ni hatua ambazo tulizichukua kwa udharura ule ili kuhakikisha kwamba angalau fedha inaanza kupatikana kwa wananchi waweze kuingia katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tathmini tumebaini pia kwamba mahindi yaliyopo kwa wananchi ni mengi sana na watu kwenye maeneo haya wasipopata soko la uhakika wengine hiyo fedha ambayo inatolewa na Serikali kupitia Wakala wake inaweza isiwafikie kabisa. Kwa hiyo, Serikali imeamua kwamba itawaruhusu wafanyabiashara waweze kupeleka mazao nje ya nchi, hasa mahindi ili kutengeneza soko na kuchangamsha bei kwa wafanyabiashara na wakulima wa zao hili la mahindi hapa nchini. Tunaomba tu kwamba viongozi wote tushirikiane kuhakikisha kwamba taratibu za kawaida za uondoshaji wa mazao nje ya nchi zinafuatwa ili kulinda mipaka yetu na kulinda usalama wa chakula hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote nchini kuacha mara moja tabia ya kuzuia mazao kutoka katika mikoa yao kwenda mikoa mingine au kutoka katika wilaya zao kwenda wilaya zingine. Tanzania ni moja na tungependa bidhaa ziweze kusafiri kutoka sehemu moja ya nchi kwenda sehemu nyingine ya nchi bila vikwazo vyovyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia Wabunge wote wanaotoka maeneo yanayolima tumbaku kwa jinsi ambavyo wameshughulikia suala la ukosefu wa soko la zao hili kwa umakini na kuguswa sana. Serikali ilikwishaliona hili tatizo mapema la kwamba tumbaku imezalishwa zaidi ya mikataba iliyokuwepo na wanunuzi wetu wa kawaida wa hapa ndani, kwa hivyo tulianza mchakato wa kutafuta wanunuzi wa hii tumbaku ya ziada walioko ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada kubwa zimefanyika na mpaka hapa tunapozungumza sasa zipo kampuni za ndani ya hapa ya nchi walio tayari kununua hiyo tumbaku. Zipo kampuni pia ambazo zimeonyesha mwelekeo kutoka nje ya nchi ambao pia wapo tayari kununua hii tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie pia nafasi hii kuiagiza Bodi ya Tumbaku ifanye mazungumzo na makampuni yote yaliyo tayari kununua tumbaku hii ya ziada, ifikapo kesho mchana wawe wamekwishanipa taarifa ya kampuni gani inaunua wapi kiasi gani ili hii tumbaku iliyopo kwa wananchi isiendelee kuharibika kwa kutunzwa vibaya hasa ukizingatia kwamba sasa hivi tupo kwenye msimu wa mvua na inaweza kunyeshewa na kupoteza ubora wake.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutarajie tu kwamba zoezi hili litakwenda vizuri, wanunuzi watapatikana wataichukua hii tumbaku nasi tutajipanga vizuri sasa kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa soko hili la tumbaku kwa kuingiza wanunuzi wengi zaidi wa tumbaku kuliko tulionao hivi sasa. Kwa hiyo, mazungumzo yanaendelea na nchi mbalimbali ambazo zina interest ya kununua tumbaku yetu na Inshallah Mungu akitujaalia tutapata wanunuzi wengi zaidi katika msimu ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti ilizungumzia suala la upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Ni kweli hili limekuwa tatizo kwa wakulima wetu hapa nchini kwa miaka mingi. Pembejeo inafika mahali na hasa pale tulipokuwa na mfumo wa ruzuku, pembejeo ya ruzuku inafika kwenye eneo msimu umekwisha mbolea na mbegu ndio zinafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, sasa hivi tunafanya mpango hapa nchini kupitia wizara yetu ambapo tutahakikisha kwamba mbolea inakuwepo maeneo yote wakati wote. Hili tunalifanya kupitia huu utaratibu wa uagizaji wambolea kwa pamoja, mbolea itakuwa inaendelea kuagizwa bila kujali msimu wa kilimo ili kuhakikisha kwamba ipo madukani muda wote na mwananchi akiihitaji anakwenda ananunua anafanya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la kuamini kwamba kilimo ama pembejeo zinahitajika wakati wa mvua peke yake sio sahihi, kwa sababu wapo pia wananchi ambao wanafanya kilimo cha umwagiliaji, kwa hiyo, wao hawasubiri msimu ule mvua, wanaendelea na kilimo chao muda wote. Kwa hiyo, sasa tumeanzisha huu utaratibu ambao utakuwa unatuhakikisha kwamba madukani iko mbolea na inayohimilika kwa maana ya bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la bei limekuwa ni tatizo au changamoto kwa wakulima wetu kwamba wengi wamekuwa hawawezi kumudu bei ya mbolea hizi. Sasa tulichokifanya tumeanzisha huo utaratibu ambao unatuhakikishia kushuka kwa bei ya hizi mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tena kutumia fursa hii kuwakumbusha wadau wote wahakikishe kwamba bei elekezi kwa aina mbili za mbolea tulizoanza nazo katika mfumo huu yaani mbolea ya kupandia DAP na mbolea ya kukuzia Urea bei elekezi zinazingatiwa kwenye maeneo yote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatahadharishe wafanyabiashara ambao hawataki uaminifu, wanaoendelea kuuza bei elekezi katika maduka ya jumla ya Mikoani na Wilayani kwamba jambo hilo ni kuvunja sheria, kwa sababu wao katika maduka ya jumla wanatakiwa wauze kwa bei chini ya bei elekezi ili bei elekezi imfikie mwananchi kijijini ambaye ananunua mbolea na kwenda shambani. Bei elekezi siyo katika maduka ya jumla isipokuwa bei elekezi ni ya wakulima anayenunua na kwenda shambani. Kwa hivyo, viongozi wote wa mikoa simamieni hili jambo, viongozi wote wa wilaya wasimamie hili jambo ili wananchi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge na tumeona ni vema na sisi tulitolee maoni ni kuhusu uboreshaji wa lililokuwa Shirika letu la Usagaji la Taifa (National Milling Corporation). Niseme tu kwamba sasa hivi iliyokuwa NMC iko chini ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na bodi hii imekwishaanza kazi. Ilianzishwa mwaka 2009 lakini utekelezaji wa majukumu yake umeanza mwaka 2013 na sasa hivi wanasaga na kununua mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasaga mahindi katika kinu cha Iringa na katika msimu huu mwanzo walikwisha nunua tani 2,300 za mahindi lakini sasa hivi wamepata pesa, mkopo kutoka Shirika letu la Hifadhi ya Taifa (NSSF) shilingi bilioni 8.9 na tumewaelekeza kwamba waendelee na ununuzi wa mahindi katika maeneo haya ambayo yana uzalishaji mkubwa ili kuondoa hiyo stress ya bei katika soko la mahindi. Pia wanafanya jitihada za ku-possess mali zao zote ambazo wamepewa kwa mujibu wa sheria ili waweze sasa kufanya biashara kama ambavyo inatarajiwa kutoka kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisigongewe kengele ya pili, naomba nikome hapo. Nisisitize tu kwamba ni ruhusa sasa kusafirisha mahindi kwenda nje ya nchi na taratibu tu za kawaida zifuatwe, pia ifikapo kesho mchana suala la tumbaku ya ziada liwe limekwishapata suluhu kwa maana ya kwamba mnunuzi gani ananunua kiasi gani, wapi niwe nimekwishafahamishwa ili keshokutwa kama ni ununuzi kuanza uanze mara moja bila kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninaomba nimjibu Mzee wangu, Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa tulizalisha kwa utoshelevu wa asilimia 123. Kama ulivyosikia katika maelezo yangu sasa hivi yapo maeneo yenye ziada nchini, kule bei ziko chini, wananchi wanalalamika hawana pa kuuza mahindi kiasi kwamba tumefikia turuhusu watu kupeleka mahindi nje ya nchi. Lakini yapo maeneo na kwa tathmini yetu, mikoa kama 11 itakuwa na utoshelevu wa chini ya kiwango na kwa hiyo tunaendelea kuwaomba wafanyabiashara nchini wachukue mahindi kule ambapo yapo ya ziada wapeleke kwenye maeneo haya ambayo hayana utoshelevu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitumie tu tena nafasi hii labda kulisemea hili, kwamba wafanyabiashara nchini na wakala zetu za Serikali wanaonunua watachukua mahindi maeneo haya yenye ziada na kwenda kuyauza kwenye maeneo ambayo yana upungufu ikiwamo pia Jimbo lake la Mpwapwa.