Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mahindi ni zao la chakula na uzalishaji wake umepanda kutokana na mwamko wa wakulima kutokana na hamasa kubwa iliyotolewa na Serikali. Pamoja na yote hayo ukulima wa mahindi leo hii ni kama adhabu kwani hakuna soko la mahindi, bei yake ni ya chini, gunia moja ni kati ya shilingi 25,000 mpaka shilingi 30,000. Je, kwa bei hiyo mkulima atamudu kununua pembejeo, mbolea, mbegu, dawa na gharama nyingine za kuendesha kilimo?

Mheshimimwa Mwenyekiti, mkulima ataendeshaje shughuli nyingine za maisha huku tukijua kuwa zao la mahindi kwa mkulima ndiyo zao la chakula na biashara. Akiugua anategemea auze mahindi, watoto kwenda shule auze mahindi, kujenga nyumba auze mahindi na kulipa michango auze mahindi. Hivyo, unapofungia mahindi yasipelekwe nje huoni kuwa ni kuwatesa wakulima wakati Serikali hainunui mahindi? Hivi Serikali inataka wakulima warudi kwenye jembe la mkono au kilimo kwa ajili ya familia tu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kilimo hakuna viwanda. Wafanyakazi wa viwandani wanahitaji kula, viwanda vinahitaji malighafi inayotokana na kilimo. Hata bidhaa itakayozalishwa viwandani lazima soko la kwanza liwe wananchi wenyewe. Je, watanunuaje bidhaa kama hawana fedha kwa sababu Serikali imewafanya wawe maskini kwa kutonunua mazao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, itakuwa ni vizuri wananchi wote wanaolima wahamie kulima korosho? Wakulima waache kulima mzao ya chakula wote wahamie migodini kuchimba madini? Wananchi wa Tanzania wataweza kununua chakula nje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo akumbuke maneno yafuatayo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, alisema:-

1. Mkulima asinyanyaswe.

2. Mkulima asipangiwe bei ya mazao yake hukumsaidia kulima.

3. Hata kama utanunua debe moja la mahindi kwa ng’ombe watatu ni sawa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais huyu anajua shida ya wakulima cha ajabu Waziri wake anakwenda kinyume na bosi wake. Kwa hali hiyo viongozi tumuelewe Mheshimiwa Rais wetu, tusimchonganishe na wananchi (wakulima).

Mheshimiwa Mwenyekiti, zuio la kuuza nje lina tafsiri kama ifuatavyo:-

(i) Unapomzuia mkulima asiuze mazao yake (mahindi) nje wakati na wewe hununui maana yake ni kumpangia bei wakati hukumsaidia kulima.

(ii) Unaposema wafanyabiashara wakanunue mahindi na kupeleka mikoa isiyo na chakula, je, huyo mfanyabiashara umempatia fedha za kwenda kununua hayo mahindi kiasi kwamba uwe na uhuru wa kumpangia bei ya kwenda kununua hayo mahindi? Je, hao wafanyabiashara utawatafutia soko zuri la kurudisha gharama zao ili wapate faida?

(iii) Unaposema kuuza chakula nje kwa maana ya mahindi/mchele mpaka wa-process wauze unga na mchele. Je, wakulima hao wameandaliwa kuwa na uwezo huo kwa sasa?

(iv) Unaposema wakulima hao kuuza nje wa-process wauze unga/mchele, je, wakulima wetu wamefikia kiwango hicho? Je, ni kila sehemu kwa sasa kumefikiwa na umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ni uungwana sana ukiaminiwa na Rais tenda haki kwa watu wake na ukiona ngoma ni nzito siyo vibaya kuachia ngazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya, nashauri kuwe na mpango wa kumalizia maboma ya majengo ya zahanati na vituo vya afya ambavyo tayari wananchi wametoa nguvu kujenga maboma hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango haujaonesha kununua magari ya wagonjwa kwa vituo vya afya ambavyo bado. Mfano, Kituo cha Afya Milepa na Laela katika Jimbo la Kwela - Sumbawanga Vijijini havina magari ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umeme, Mpango ueleze juhudi za makusudi kuhakikisha kila kijiji/kitongoji kinapata umeme. Mfano, Jimbo la Kwela lipo nyuma halijapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara, naishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa Daraja la Mto Momba. Naomba baada ya daraja kukamilika ianze ujenzi wa barabara ya Kasansa - Kilyamatundu - Kamsamba - Mlowo kwa kiwango cha lami.