Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kukubali ombi la Mheshimiwa Paresso ili aniachie dakika kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na maswali, yaani ni hivi, tunajadili hapa maswali yaulizwa Bungeni na Mheshimiwa Dkt. Mpango yupo na anajua swali gani likiulizwa karibu Bunge zima linasimama. Lakini unapokuja kuweka mipango ili Watanzania wengi wanufaike unatuletea mipango ya kujenga reli kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndiyo reflection ya Waheshimiwa Wabunge kwamba wao wanataka reli ya Dodoma? Ni reflection ya Watanzania kwamba wao wanataka kiwanja cha ndege cha Chato? Ni kweli ni matakwa ya Waheshimiwa Wabunge, wao wanataka bombardier? Kwa nini mnatufanyia namna hii? Kwa nini wakati Bunge watu wanauliza maswali katika mipango ya nchi hii huangalii ni nini watu wanataka ndani ya Tanzania, sisi ndio wawakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasimama wengi kwenye maji, lakini leo unatuletea mipango ya maji ya vijiji totototo, wakati Tanzania tuna mito, tuna maziwa, tuna kila kitu. Kwa nini usituletee maji ya bomba, mpango ambao utaonekana mnakwenda kutega sasa maji katika milima, katika mito ambayo tutakuwa na kilimo cha umwagiliaji na maji yatatiririka kila kijiji? Kwa nini mnakwenda kutuchokozea ardhi chini ili ituletee matetemeko ndani ya nchi ya Tanzania?

Kwani Mungu aliweka Mito hapa Tanzania alikosea nini? Naomba mipango inapokuja ndani ya maji usituletee mipango mingi ya visima. Tumia mito, maziwa ili tupate maji ya umwagiliaji na maji ya bomba salama na kunywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata umeme huo. Umeme wa maji nasikia ni rahisi. Huko nyuma katika vitabu nilisikia sana wana mipango, kwa mfano kule Mlimba kuna mto mkubwa kabisa ambako unakwenda kumwaga maji mpaka huko Kilombero, mpaka Rufiji, huko kwenye Stiegler’s, lakini kule mmekusahau kabisa. Mlisema mtazalisha umeme kwenye Mto Mpanga, leo katika mipango yenu hakuna kitu, mmedandia Stiegler’s Gorge. Nini? Tatizo liko wapi, kwa nini mnapanga mipango halafu mnaiachia njiani, kwa nini hammalizi? Kwa hiyo, mimi nilitegemea mipango iwe endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye gesi, Watanzania wote walijua sasa gesi imepatikana, tukasifiwa hapa kwamba gesi sasa ndiyo mkombozi wa Watanzania, kila mmoja alijua baada ya miaka fulani gesi…, sasa hivi mimi niko kwenye Kamati ya Nishati na Madini; gesi sasa hivi ni kitendawili, na wakati ule Mheshimiwa Mnyika alikuwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini alisema leteni mikataba ya gesi hapa Bungeni, mikataba mnayosema tofauti na mliyoingia kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo utakuta eti Serikali imedhamini Songas imekwenda kuchukua hela huko halafu Songas hawana chochote. Mitambo ya TPDC, mitambo ya TANESCO, lakini Songas kamuajiri tena huyo mbia Pan African Energy, halafu huyo huyo anaunasibu tena wa TPDC. Hela tumekopa Tanzania; kuna gesi hapa?; halafu Serikali ndiyo inakwenda kulipa ule mkopo. Ule mkopo hailipi Serikali, inalipa kwa Watanzania, wapigakura wetu. Nini ninyi? Haya mambo gani mnatuletea hapa? Hizi figisufigisu hapa za nini? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna matatizo makubwa ndani ya nchi yetu. Labda kama unashinikizwa, maana tumuonee huruma na huyu jamaa. Hapa unaambiwa hii nchi hakijachakuliwa Chama cha Mapinduzi, amechaguliwa mtu mmoja, alichukua fomu peke yake, kwa hiyo hata ukiwa Waziri ukibisha tu imekula kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa bwana, lakini Mheshimiwa Spika jana alisema tuseme tu tusiwe na wasiwasi, sasa wasi wasi wa nini Wabunge wa CCM, lakini na mimi mwenyewe si Mwenyekiti wangu kaniambia niseme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida za Watanzania kwa mfano kule Mlimba na maeneo mengine ni kuunganishwa barabara za mikoa na wilaya kwa sababu Watanzania wengi ni wakulima. Lakini leo Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie, katika mpango huu unaokuja, je, ni barabara ngapi nchini Tanzania zitakwenda kuanzishwa na kujengwa kwenye viwango vya lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasaidia nini? Inasaidia kwa sababu Watanzania wengi ni wakulima. Kwa hiyo, watapitisha mazao yao lakini itasaidia sana wanawake ambao wanajifungua katika mazingira magumu na Hospitali za Wilaya ziko mbali. Haki ya Mungu wanaokufa nchi hii ni vijijini. Kwa hiyo, barabara zitaokoa uchumi kwa wakulima, zitaokoa vifo vya akina mama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipata barabara inawezekana kabisa tutapunguza vifo vya akina mama kwa sababu sera ya Taifa kila kata kuwe kituo cha afya, kila kijiji zahanati. Hebu tuambie mpango madhubuti wa kutimiza sera ya Taifa kwamba kuna vijiji vingapi nchini Tanzania vina zahanati, kuna kata ngapi zina vituo vya afya na mpango wa Serikali ni nini katika kutatua haya matatizo. Hatuwezi kukubali wananchi wanakufa huko, hasa akina mama na watoto. Tunaomba uje na huo mpango ili utuambie tupunguze vifo, tuokoe akina mama na watoto na tuokoe wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu mimi nilitegemea uje na mpango, kwa kuwa tayari tuna vituo vya JKT na hii tunasema kwenye nchi ya viwanda, ungekuja na mpango hapa kwamba JKT itachukua vijana iwe darasa la saba, iwe vyuo vikuu, watakwenda kufanya huko stadi mbalimbali na kufundishwa uzalendo halafu wakitoka huko wanakuwa na package ya kuwakopesha kwenda kutengeneza viwanda. Mngechukua hata wataalam kutoka China, na hiyo ilikuwa Ilani ya CHADEMA, tulisema JKT itakuwa si tena mabunduki tu, kutakuwa na mpango maalum vijana kwenda huko kujifunza mafunzo mbalimbali ili kwenda kuokoa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkopo wa reli, mmechukua mkopo mnajenga reli mpaka Dodoma, lakini TAZARA mmeisahau. Tatizo ni nini? Hii TAZARA inapita hata Selous, watalii walikuwa wanatoka Dar es Salaam wanakwenda kwa treni mpaka Mlimba, au wengine wanapita kwa barabara mpaka Mlimba wanaingia Selous; lakini leo barabara hakuna, reli yenyewe haina uhakika. Tatizo liko wapi? Uje na mpango katika kukuza utalii kule Selous ili hawa watalii waje kwa barabara au waje kwa TAZARA ili tuone kwamba tunakuza uchumi wetu.

Mheshimwa Mwenyekiti, afya nimeshazungumza. Kwa ujumla naomba angalia hoja za Waheshimiwa Wabunge, angalia maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Unapokuja na mipango yako zikusanye ujue tatizo ni nini halafu ukija na mpango elekeza kule ambako Wabunge wengi wanaleta maswali Bungeni ili tutatue haya matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mengine ya bombardier na nini yatakuja tu, hivyo viwanja vya Chato, hii tumeshakula bogi umetuingizia huku mabilioni ya hela wakati wengine hata maji hatuna, umetuingizia huku mabilioni ya hela, unakopa wakati sisi hapa ulitakiwa ukope turudi vijijini kwetu tuwaambie tumekopa kwa sababu tunajenga barabara, tumekopa kwa sababu tunajenga vituo vya afya, tumekopa ili tujenge zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tungekuwa radhi kabisa kuiunga mkono Serikali kwa kukusanya kodi, tungefunga mikanda kwa sababu tunajua mpaka kufikia mwaka fulani matatizo ya maji litaisha, barabara pamoja na zahanati yataisha, lakini sasa hivi hatujui hiyo mikopo itamaliza tatizo gani. Sisi watu wa Mlimba hatuna shida ya ndege bombardier, hatuna shida ya kiwanja cha Chato lakini madeni hayo yanatupata wote, hiyo si tabia nzuri, acheni.