Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika mpango huu uliowasilishwa na Serikali hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, napenda kushauri Serikali inapoleta mipango hasa kwenye miradi mikubwa, isiwe na miradi mikubwa mingi ambayo itagharimu fedha nyingi tena za mkopo, lakini matokeo yake inachukua muda mrefu. Ni vizuri mkawa na miradi michache, hata kama mtakopa lakini angalau iwe michache mwisho wa siku iweze kuwa na ufanisi. Kama ambavyo mmefanya hapa, kuna miradi mingi lakini ukiangalia hata mipango ya miaka miwili nyuma iliyopiata hivyo vivyo, mmekuwa na miradi mingi sana ambayo hata leo ukifanyia tathmini nafikiri hakuna hata mmoja ambao tayari umeshaanza kuonesha matokeo, lakini tena mmekopa maana yake mnaendelea kuendeleza Deni la Taifa.

Kwa hiyo, ushauri wangu ni bora muwe na miradi michache yenye matokeo ya haraka lakini itakayotumia fedha kidogo au hata kama ni nyingi lakini kwa ukopaji ambao utakuwa si wa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nichangie katika Sekta ya Utalii. Pato la Taifa asilimia 17.2 inachangiwa na Sekta ya Utalii. Maana yake ni kwamba asilimia 25 ya fedha za kigeni inatokana na utalii. Lakini ukiangalia hapo kwenye mpango ambao umewasilishwa na Serikali hamjatilia mkazo wa kutosha wa namna gani sekta hii ya utalii ambayo inaingiza kiwango kikubwa cha Pato la Taifa inawezeshwa ili kuhakikisha utalii huu ambao unaingizia fedha za kigeni nchi hii uweze kuendelea kwa kiwango kikubwa. Mfano, umesema hapa Mheshimiwa Waziri, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato yanayotokana na utalii. Maana yake ni kwamba mmekuwa mkizoea kuendeleza kuongeza kodi kwenye sekta ya utalii au kwa watu ambao wanafanya biashara ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tuliwashauri hapa wakati tunapitisha bajeti kwamba mfute baadhi ya kodi zilizopo kwenye utalii, hamkufuta, wenzetu wa Kenya wakafuta, sisi hapa tukaongeza. Maana yake ni kwamba unaendelea kufanya sekta ya utalii ni ghali sana hapa nchini, mwisho wa siku mzungu au mtalii yeyote atachagua kwenda kwenye eneo ambalo ni rahisi na ataona vile vitu ambavyo anavitaka, kwa hiyo mkiwa mnashauriwa, Waziri mpokee ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu anayewekeza kwenye hoteli za kitalii analipa kodi 46. Mheshimiwa Waziri ni vizuri sana muwe na kodi chache ili watu wengi waingie kwenye kuwekeza kwenye utalii ili tuendelee kupata wageni maana yake utalii utakuwa ni rahisi. Tulimshauri sana Mheshimiwa Profesa Maghembe kipindi hicho lakini hakusikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi nyingine ni ya TALA license, unalipa dola 2,000 kwa magari matatu. Uwe na magari 100 unalipa dola 2,000. Ni kwa nini msifanye kodi hii ikalipwa kwa gari? Ukilipa kwa gari maana yake utawa- encourage watu wengi wawe na magari, utalii utakua, ushindani utakuwa mkubwa, biashara itakua. Unalipa dola 2,000, magari 100; wale Leopard Tours Arusha, makampuni makubwa wana magari 100 mpaka 200 lakini analipa dola 2,000. Kijana wa Kitanzania aliyepambana amepata hela ana magari matatu analipa dola 2,000, hii ni nini Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeishauri Serikali, tulimshauri sana Mheshimiwa Maghembe hapa hakusikia akaendelea kushukilia msimamo huo, nafikiri ni vizuri muangalie hilo. Lakini sekta hii ya utalii pia imeajiri vijana wengi ambao walikosa ajira lakini wameji-engage huku. Kwa hiyo, tunategemea kwamba jinsi ambavyo utalii utaongeza Pato la Taifa ndivyo ambavyo wawekezaji wataingia kwenye sekta hii, ndivyo ambavyo pia vijana wetu wengi watapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano mliingia kwa nguvu kubwa sana mkasema nchi hii ni nchi ya viwanda, Tanzania ya viwanda. Lakini siku hizi wimbo huu umeanza kupotea, sijui mnaendeleaje, hausemwi kwa nguvu ile ambayo mlianza nayo mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matamko ya kutafuta kiki za kisiasa. Mheshimiwa Waziri jana wamezindua, wanasema kila mkoa utajenga viwanda 100, maana yake mikoa 26 tunategemea kuwa na viwanda 2,600. Sasa hivi viwanda mnavyotamka, kwanza mtupe tafsiri yake, kwa sababu akija Waziri wa Viwanda anasema vyerehani vitatu kiwanda, akija mwingine anasema viwanda ni viwanda, mtupe tafsiri sahihi ya viwanda ni nini ili siku tunapowafanyia tathmini ya hivyo viwanda ambavyo mmekuwa mkiwaambia Watanzania tujue ni viwanda kweli au si viwanda. Kwa hiyo msitafute kutafuta cheap kiki za kisiasa kuwanufaisha Watanzania wakati sio sawasawa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)