Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii adhimu kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya leo tumekutana hivi wote katika dhima nzuri kabisa ya kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2018/2019. Pia nitoe pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa chini ya Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli pamoja na timu yake nzima kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kufanya na sisi tukiendelea kuisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, nitoe pongezi kwa wenzetu walioaminiwa, walioaminiwa wapya lakini na wale ambao wameendelea kuaminiwa na Rais kwa uteuzi wa kushika nafasi za Mawaziri, Naibu wa Mawaziri lakini pia nawapongeza na wale ambao walibaki, tutaendelea kusimamia Serikali huku kwenye ukumbi huu wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi kwa Wizara ya Mipango na Fedha kwa Mapendekezo haya mazuri chini ya Mheshimiwa Dokta Mpango kama jina lako lilivyo lakini pamoja na pacha wangu Mheshimiwa Dokta Ashatu na Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, kimsingi hotuba yenu ya Mapendekezo ya Mpango imekaa vizuri tatizo kubwa ambalo tumekuwa nalo ni kwenye utekelezaji. Kama ambavyo wameainisha kwenye hotuba yao wamechukua maoni kutoka kwenye jamii, taasisi za Kiserikali, Kamati ya Bunge ya Bajeti ambayo hiyo unaipata kwenye hotuba yake ukurasa wa nne paragraph ya saba lakini pia wameileta kwenye Bunge ili waweze kuchukua maoni.

Mheshimiwa Spika, tunawaomba sana kwamba uchukuaji wa maoni haya uwe wa ukweli. Tumeanza juzi tunakwenda kumaliza Jumatatu siku tano nzima Waheshimiwa Wabunge hawa kila mmoja kwa nafasi yake anatoa pale alipoona panafaa. Tukitoka kapa kwa maana ya uchukuaji wa haya maoni, kwa kweli tutakuwa tunapoteza maana nzima ya sisi kukaa na kujadili Mapendekezo haya ili yaje kuboresha mpango na bajeti siku za mbele. Tunawasihi sana wachukue maoni yetu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nataka niseme kwamba pamoja na uzuri wa Mapendekezo na tunatarajia Mpango utakuwa mzuri baada ya kuchukua input zetu, ni lazima tuweke mikakati madhubuti na inayotekelezeka ya kuhakikisha utekelezaji wa Mpango huu unakwenda. Tutachukua maoni lakini utekelezaji unakwendaje? Tuna mikakati gani inayotekelezeka ya kuhakikisha Mpango huu wa Maendeleo na Bajeti ya 2018/2019 utakuwa dhahiri, utakuwa realized kwa Taifa na utakuwa realized kwenye uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye maoni na ushauri wangu katika kuboresha Mapendekezo haya ambayo mmeyaleta mbele ya Bunge hili. Nia ni nzuri na nia ni kwamba tunakwenda kujenga, kuimarisha na kuendelea kukuza uchumi imara, uchumi endelevu, uchumi ambao tunataka tufike mahali tunasema sustainable growing economy na sisi tumepanga mpaka 2025 tuwe katika kiwango cha uchumi wa kati, ni lazima tuone tunakwendaje vizuri ili tufike huko kwenye hazima yetu.

Mheshimiwa Spika,Dhana ambayo tunakwenda nayo ni ya uchumi wa viwanda. Uchumi wa viwanda maana yake tunahitaji kufanya mapinduzi ya viwanda. Tumeyasikia mapinduzi ya viwanda yamefanyika kwenye Mataifa mengine mbalimbali na hatimaye kweli wamefikia uchumi wa viwanda.

Mheshimwa Mwenyekiti, nia na madhumuni hapa ni kwenda kuongeza uzalishaji. Tumesikia wenzetu wamechangia kwamba mahali ambapo tunategemea sisi kukusanya au kupata mapato ya nchi ni kwenye vyanzo labda vilevile, tunahangaika na tax base ambayo kila siku inakuwa ni ileile, unakamua ng’ombe ambaye tayari labda hajaweza kuzalisha zaidi. Sisi dhamira yetu lazima twende kuzalisha zaidi tupate surplus ambayo mwisho wa siku tunaweza kuweka akiba na nyingine ikatusaidia kuongeza kipato kwa kuuza huduma na bidhaa ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema na kwenye maandiko haya yote yako vizuri kabisa kwamba tunataka kuweka viwanda ambavyo vitalishwa na rasilimali zinazozalishwa Tanzania. Ni sahihi kabisa, tungeweza kuzungumzia kila eneo na products zao wanazozalisha. Mfano kule kwetu Kondoa tunaweza kuweka kiwanda cha edible oils, kuna karanga, ufuta, alizeti kwa wingi kabisa na hii inaweza ikawa Kondoa lakini vilevile ikakamata Ukanda mzima wa Kati. Dodoma yote inazalisha alizeti vizuri kabisa, Singida majirani zetu wanazalisha alizeti, karanga, ufuta, tunapiga kiwanda kimoja cha kiwango kikubwa ambacho ni double refinery.

Inaweza kulisha na kuongeza tija katika ukanda wote wa edible oils. Lengo kama ambavyo mmeliainisha ikiwa ni kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa kwenye maeneo yetu na kukuza mnyororo wa thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe na kuzidi kushauri Wizara katika kuboresha haya Mapendekezo. Mapinduzi ya viwanda yatafanikiwa pale tutakapofanikisha mapinduzi ya kilimo. Tunazungumzia malighafi zilizoko pale lakini bila ya mapinduzi ya kilimo haya mapinduzi ya viwanda yatakuwa ni hadithi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeendelea kuweka jihada katika kuhakikisha tunapata mbegu bora, kuhakikisha tunaweza kupeleka pembejeo kwa wakati, mikakati mingi sana ipo, lakini jambo moja kubwa ambalo nataka kuliwekea uzito leo hapa ni suala la kilimo cha umwagiliaji. Hiki kilimo cha mvua hata upeleke mbegu za namna gani, uwe na pembejeo za namna gani bila ku-engage kwenye large scale farming ambayo itakuwa inategemea irrigation tutakwama tu kupata mapinduzi ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nisisitize sana eneo kubwa ambalo lazima tuliwekee mipango ni hili la irrigation ambalo tumekuwa tukilizungumzia mara nyingi. Wizara ya Maji na Umwagiaji ukiangalia bajeti yake kwenye upande wa irrigation ni ndogo sana. Hapa tunahitaji tuwekeze heavily kwenye infrastructure za irrigation, iwe kupitia mabwawa, kupita kwenye utaratibu wa matone (drip irrigation) au na mifumo mingine ya mito, mifereji na kadhalika lakini bila irrigation large scale farming itashindikana.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia large scale farming ndiyo italeta mapinduzi ya kilimo, tunazungumzia wakulima wakubwa lakini pamoja na hawa wadogo, wakitumia kilimo cha umwagiliaji tija yake ni kubwa, una uhakika wa yield. Tusipofanya hivyo tutakuwa tunakabiliwa na changamoto ya tabia nchi kila mara na hatimaye uhakika na usalama wa chakula na uzalishaji usiwepo, hata hivyo viwanda ambavyo tunataka malighafi tunazolima wenyewe ziende kulisha kwenye viwanda ikashindikana.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Mheshimiwa Dokta Mpango na pacha wangu Dkt. Ashatu, na nawasihi sana ushauri huu wa kui-nvest heavily kwenye scheme na infrastructure ya irrigation ni jambo ambalo tukiweka hapo mkazo litatuondoa na tutafikia kwenye mapinduzi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwenye kufanikiwa mapinduzi ya viwanda nimezungumzia mapinduzi ya kilimo lakini vilevile tujiwekeze na tujikite kwenye kuzalisha wataalam wa ufundi. Amezungumza ndugu yangu hapa Mheshimiwa Maige, siku za nyuma nimewahi kuzungumza tulivyokuwa tunajadili Mpango 2016/2017 na 2017/2018 kwenye Bunge hilihili kuhusiana na polytechnics, kuzalisha wataalam kwa ajili ya kwenda kuviendesha na kuviendeleza viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia uchumi wa viwanda, wako wapi hao wataalam ambao wanakwenda kuwa wabunifu na kuvikuza viwanda hivyo kama kila mmoja anataka afanye kazi ya white colour. Vyuo vilivyokuwepo awali, Chuo cha Ardhi amezungumzia mzee hapa Dar Technical vile ambavyo products zilizokuwa zikitoka kule zinatoka kwenda kufanya kazi ya ufundi. Managers ni wengine, watakuwepo mainjinia watapata degree na kadhalika lakini wanaokwenda kuendesha viwanda vile tunawazalishia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwekeze kwenye polytechnics, vyuo vikuu vya ufundi, vya ufundi wa kati ma- artisan hawa, technicians wa FTC lakini pia na vyuo vikuu vya ufundi ambavyo wenzetu maarufu wanaviita polytechnics ili viweze kwenda kuzalisha wataalam watakavyovikuza na kuviendeleza viwanda hivyo. Haya ambayo nimeyaongea ya polytechnics lakini ya irrigation nadhani tukiyazingatia yatatusaidia sana kwenda kuleta tija kwenye Mpango huu ambao tutakuja kuujadili mwakani. Jambo lingine na la mwisho, huko mwanzo nimezungumzia kuongeza uzalishaji mwisho wa siku ina-ripple effect kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine na la mwisho nataka kuzungumzia kuhusu na dhana nzima ya uwezeshaji wananchi kiuchumi. Sitagusa milioni 50 za kwenye Ilani kwa sababu nadhani huko siko tunakotaka kwenda, lakini basi tujikite kwenye kuwezesha infrastructure muhimu, kutengeneza mazingira mazuri ya micro-financing ambapo wale wananchi wa kawaida wataweza kupata angalau nguvu kidogo ya uchumi liquidity ikaongezeka kupitia sijui SACCOS, kuimarisha mifumo ya VICOBA, micro-finances nyingine, kujenga na kuimarisha mazingira haya ili angalau mwananchi wa kawaida aweze kunufaika na mikopo au upatikanaji wa mitaji yenye masharti na gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira ya kawaida, yule mfanyabiashara pale Kondoa kijijini au mjini au mkulima ni ngumu sana ku-access financing kupitia financial institutions tulizonazo. Ni lazima tutengeneze miundombinu mizuri kabisa, tujenge mazingira ya kuwafikia hawa watu wa chini wakope kidogo kidogo ili waweze kujiinua kiuchumi wao wenyewe mmoja mmoja na hatimaye jamii nzima ya maeneo halisia na hatimaye Taifa kwa ujumla. Tutakuwa tumepiga uchumi jumla na tumepiga micro- economy, mwisho wa siku Taifa linakwenda mbele na kwa kazi kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.