Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru umenipa nafasi nichangie mpango huu. Nimekuja na mipango mitatu, nimekuja na Mpango wa mwaka 2016/2017; 2017/2018 na 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Deni la Taifa. Kwenye Mpango wa 2016/2017 tuliambiwa ilipofika Oktoba, 2015, Deni la Taifa lilikuwa dola bilioni 19 ikilinganishwa na dola bilioni 18 za mwezi Oktoba, 2014. Tulipokuja Mpango 2017/2018, tukaambiwa Deni la Taifa limekua dola bilioni 18, ongezeko la asilimia 9.76. Sasa mwaka uliopita ilikuwa bilioni 19, mwaka unaofuata tunaambiwa ni bilioni 18, lakini kuna ongezeko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawakuishia hapo, wanasema ongezeko hili wanalinganisha na dola bilioni 16 za kipindi cha 2015. Kwenye mpango huu wa mwanzo wanasema Oktoba ilikuwa bilioni 19, kwenye mpango huu wa pili wanasema Oktoba ilikuwa bilioni 16. Sasa kwenye mpango huu mpya wanasema Deni la Taifa limefika bilioni 26 ukilinganisha na Dola bilioni 22 za mwaka 2016 Juni, lakini kwenye ripoti ya Juni tunaambiwa dola bilioni 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, moja ya tatizo tunalo hapa ni data hizi zinazoletwa na Wizara ya Fedha. Data ni za kwao haiwezekani tukawa na fatal mistakes za zaidi ya Dola bilioni tatu, jamani hatusomi documents hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini ninachotaka kusema, ukiangalia mipango yote mitatu kwa kweli, ni copy and paste. Ukipitia yote wamebadilisha language, kinachosemwa ni kile kile. Kwa hiyo, hapa tunapanga, lakini ni kwa sababu, ni Katiba lazima tupange, yanayokwenda kufanyika wao wanajua, Bunge lako haliyajui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema deni la Taifa linapanda. Sasa hivi linapanda kwa trilioni nne kwa mwaka kulingana na ripoti za BOT. Maana yake ni nini? Maana yake tumeamua, kama Serikali kwamba, kila kitu kinafanywa na Serikali, hatuwezi kuendelea! Halipo Taifa duniani ambalo kila kitu wanajenga kwa fedha zao. Kwangu hata ukikopa ni fedha zako sina shida, ukikopa bado ni fedha zako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe shahidi tumekwenda Moscow uwanja wa Moscow International unajengwa na mtu binafsi. Hivi humu ndani tunasema tutafanya PPP, ukitafuta miradi ya PPP haipo, Serikali hii haiamini katika private sector.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Bunge hili tukubaliane Waziri wa Fedha atuambie Serikali hii haikubaliani na private sector kwa sababu mipango yake Mheshimiwa Waziri mwanzo mpaka mwisho haongelei private sector. Kama tumerudi kwenye ujamaa tuambiane wote tujue, lakini haiwezekani tunaimba ujamaa halafu tunataka matokeo ya Kibepari, haiwezekani! Hakuna katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, soma mpango huu hakuna production. Hatuongelei kukuza tija, angalia kwenye kilimo, angalia mazao yote ya kilimo hakuna anayeongelea kukuza tija, maana nilitarajia wangesema mwaka huu tumezalisha tani fulani za mahindi, mwaka kesho ni tani fulani za mahindi, hakuna! Pamba hakuna, kahawa hakuna, tumbaku hakuna, korosho hakuna, sasa tunapanga nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunapanga vizuri sana, lakini mwisho wa siku ukiangalia mpango uliopita yale yale yamesemwa. Huku kwenye mipango yote wanasema wataweka fedha TIB, fedha hizo zisaidie ku-leverage kwenye miradi, toka wameanza kusema hawajaweka senti tano TIB. Naomba watusaidie mambo ambayo wanajua hawawezi kuyafanya wasiyaandike unless wanaamini Bunge halisomi documents hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda humu ndani utaona kabisa kwamba, kwa mfano leo tunaongelea bei ya mahindi. Naomba nikwambie bei ya mahindi kinachofanya bei imeshuka watu hawataki kusema, Zambia wameanzisha Commercial Farming, wamelima mahindi mengi sana sasa yanauzwa mpaka Somalia, kwa vyovyote hatuwezi ku- compete kwa sababu wao wanaongeza production, hatuongelei production, sisi tunahangaika kubanakubana, sasa mmegeuza ni uchumi wa kubana tu, leo tunaleta sheria hapa ya kubana! Hakuna anayeongelea kupanua! Hakuna. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaanzisha kiwanda cha pamba una marobota 240,000 kwa mwaka. Bangladesh kiwanda kimoja kinatumia marobota milioni tano, leo tunaongelea viwanda vya pamba kwa marobota 240,000, tunamdanganya nani hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwonea huruma sana Mheshimiwa Rais anahangaika, lakini wenzake hawamwambii ukweli, mtanisamehe. Leo Rais anakwenda kuwaambia viwanda ndio vizalishe sukari, lakini tumesema hapa siku zote hakuna aliyetuelewa kwenye hili Bunge, lakini kwa sababu Rais amesema viwanda vitazalisha sasa.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, twende kwenye records tumesema, waongezeeni maeneo walime. Ilovo waliomba maeneo wakanyimwa, Ilovo wameenda Zambia leo ni number two kwa sugar production in Africa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ardhi tunayo ni over regulations ni over regulations. Humu ndani Waziri anaongelea kodi tu, haongelei kukuza biashara, anaongelea kukusanya kodi peke yake, tunakusanya kodi kwa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mabenki yanakufa, mabenki yote yana-record less profit hata mabenki makubwa. Uchumi unaofanya vizuri unaangalia mambo haya mawili, performance ya banking industry na performance ya stock exchange. Go to Dar es Salaam turn over ya Stock Exchange Dar-es-Salaam imeshuka kutoka bilioni 20 mpaka bilioni mbili na no one is talking about 85 percent, Waziri wa Fedha hasemi wala sidhani kama ana interest na sioni yeyote mwenye interest na hili jambo, ni nini hii? Jamani hii nchi ni yetu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaombeni, haiwezekani viwanja vya ndege tujenge kwa pesa, reli kwa pesa zetu, umeme kwa pesa zetu, barabara kwa pesa zetu, hivi sisi ni nani? Dunia yote imeenda kwenye private sector, the whole world! China kuna toll road, Malaysia kuna toll road, kokote unakokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni mambo mawili, moja; tunaleta hapa sheria ambayo humu ndani hawajasema ya kuleta NASACO, unajua kwa sababu gani, tunaongelea Tanzania tuna-manage ma-container 600,000 Singapore wana-manage ma-container milioni 34. Badala ya kuongelea kuongeza mzigo, tuongeze ma-container yatoke laki sita yaende milioni nne hadi milioni tano, tunafikiria ku-regulate hayo, kulinda hizo hizo laki sita zetu, ni nini hii? Hakuna anayewaza kuongeza biashara, kuongeza production, hakuna! Soma mwanzo mpaka mwisho hatuongelei kukuza biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda kwenye mabenki kila kitu kimeshuka, everything. Naomba nikupe data mbili au tatu. Personal landing mwaka 2015 ilikuwa asilimia 25.5, leo ni asilimia nane. Trade 2015 ilifika asilimia
24.6 leo ni asilimia tisa. Manufacturing it was 30 percent, leo ni asilimia tatu. Hakuna anayesema, tunaona mambo ni mazuri, ukisema tutaanza kupewa majina. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo hayako sahihi kwa sababu moja tu, ukiangalia sababu yetu ni moja tu, mpango wetu wa mwaka huu ndiyo wa mwaka jana, ndiyo wa mwaka juzi na ndiyo wa mwaka unaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Bunge lako tuamue, tuiombe Serikali iseme sasa inataka ujamaa twende kwenye ujamaa per se, kama ni ubepari au uchumi wa soko tuende kwenye uchumi wa soko per se, short of that ukivichanganya hatuwezi kwenda kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nataka kusemea suala la Kigoma, REA. Alisema jana Mheshimiwa Obama, kinachoendelea REA leo kwa watu wa Kigoma ni dhambi. Kigoma tumepata mkandarasi amepewa kazi, ni Kigoma na Katavi, anataka kuanza CRB inakuja inasema huyu hafai. Hivi CRB Mikoa yote hamkuona umuhimu wa kuangalia procurement, mnaangalia kwa ajili ya Mkoa mmoja na kwenye Sheria ya Procurement CRB inakujaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu tunazijua, aliyekuwa anataka kazi ya Kigoma na Katavi ndiye Mwenyekiti wa CRB, ni conflict of interest na Mawaziri leo, Waziri Kamani hawezi kuamua ana kigugumizi, Waziri Mbarawa hawezi kuamua ana kigugumizi kwa sababu wote tunazijua. Watu wa Kigoma mnatuweka wapi, kwani sisi siyo Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unfortunate, hivi sisi ni nani? Nataka kusema suala la REA na suala la Kigoma kwenye REA III naombeni mfanye maamuzi. Kama suala labda kumpa huyo ambaye najua ni mpendwa ambaye yuko CRB, mpeni tufanye kazi, yule maskini mwenzetu ambaye alifanya REA II leo hamwoni wa maana mnyang’anyeni basi mpeni mnayemtaka ili twende watu wa Kigoma wasipate hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini mipango yetu kwa kweli ni ya mwaka jana ndiyo ya mwaka juzi. Sielewi maana yake ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.