Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii nami kujadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019. Mapendekezo ya mpango ambayo tunayajadili leo hayana tofauti na mapendekezo tuliyopitisha mwaka jana, hakuna tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hauna tofauti kwa sababu tone yake ni ileile ya mwaka jana, ndiyo ambayo ipo katika kitabu hiki cha mwaka huu, ukikipitia chote kama kilivyo, kina tone inayofanana. Sasa changamoto yake ni nini? Changamoto ya mpango wote ni utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakwenda kwenye hoja ambazo zipo kwenye kitabu. Mimi leo najadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Serikali ya Awamu ya Tano ina sifa moja imejinasibu kama Serikali ya kubana matumizi, lakini kwenye kitabu hikihiki unarudi unakuta deni la Taifa limeongezeka toka dola milioni elfu 22 mpaka dola milioni elfu 26115.2 ambayo ni sawasawa na trilioni hamsini na tisa. Sasa wewe unasema umebana matumizi, deni limeongezeka, unawachanganya wananchi, kwa hiyo sasa ndiyo vitu tunavyokwenda kuvijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda kuuliza sababu za kungezeka kwa deni ni nini Mheshimiwa Waziri amekuja sababu za kuongezeka kwa deni la Taifa ni ujenzi wa reli ya standard gauge, SGR, Strategic Cities mradi wa Usafirishaji Dar es Salaam (DART), sasa the question ni nini? Mheshimiwa Rais anapozunguka huko mtaani anatueleza kwamba tutajenga reli kwa fedha zetu za ndani, unakuta kwenye kitabu, kitabu kinasema tofauti kwamba tutajenga reli kwa mkopo, tuelewe nini, yaani tuelewe nini, kinachoandikwa na kinachozungumzwa ni vitu wiwili tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni mambo lazima tukubali kuyarekebisha, yaani siasa siyo kupiga fiksi muda wote au siasa sio kutafuta kiki muda wote hamna, wakati mwingine wananchi wanahitaji kuelewa ukweli. Tuwaeleze tu ukweli, tutajenga reli kwa mkopo, tutakopa kiasi hiki zitalipwa na wananchi, unapata sifa kwa sababu wananchi wanachotaka ni miradi ya maendeleo, sasa unawaambia tutajenga, kitabu kimeandikwa na ushahidi wetu unaotumaliza ni hiki kitabu. Hilo nimelimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni matumizi ya fedha nje ya bajeti tulizozitenga. Tumekaa hapa zaidi ya miezi mitatu tunapitisha bajeti, tunapitisha vifungu na mwisho wa siku kuna kitu kinaitwa Appropriation Bill, Sheria ya Matumizi ya Fedha. Ile sheria inatufunga kwamba tutumie kulingana na kile ambacho tumekipanga humu ndani. Sasa unakwenda kwenye kitabu unakuta sasa kuna miradi mipya tu kwamba miradi ya ujenzi wa bwawa wa mitambo ya kufua umeme Stiegler’s Gorge siyo jambo baya wala sikatai, lakini unarudi Sheria ya Bajeti inataka nini? Ukiangalia kifungu cha 43 cha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 inataka Serikali inapotaka kuongeza bajeti ije hapa. Ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Chato sio kosa, ni nia njema ile, lakini usipofuata sheria...

T A A R I F A . . .

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ni vizuri nimweleze kabisa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, mimi sipingani na kutenga fedha ya bilioni mbili ipo kwenye bajeti. Hiyo ilikuwepo na ndio maana hakuna mtu anayejadili, lakini sisi tunachojadili ile bilioni 39, ambayo iko nje na kinyume cha bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunajadili. Ni mambo mema Sheria ya Bajeti kifungu cha 43(1) ya mwaka 2015 inaruhusu Serikali kuomba nyongeza ya bajeti na inawekewa mkazo na Sheria ya Fedha za Umma, kifungu namba 18(3) na cha (4) ya mwaka 2000; vyote hivyo inataka Serikali inapotaka kufanya jambo kwa mfano unataka labda kuli-allocate ama kuongeza jambo lingine jipya ambalo halikuwepo kwenye bajeti unaleta ndani ya Bunge. Sasa mambo mengi hapa ndani yanayofanyika sasahivi na Serikali hayajapitishwa na hili Bunge, hayajapitishwa na tumekaa humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoeleza ni nini? Leo unayafanya haya in good faith unasema unatumia kwa nia njema, lakini kesho atakuja Rais mwingine, Mheshimiwa Mpango utakamatwa kwa kutumia madaraka yake vibaya huo ndio ukweli. Kwa sababu hapa Mheshimiwa Simbachawene juzi alijiuzulu kwa sababu tu aliingia mkataba wa TANZANITE, lakini kwenye maelezo yake alisema kabisa ametumwa juu, lakini leo amewajibika yeye. Kumbukeni watu wanaowatuma wana kinga, wao hatuwafungi, wala hatutawakamata. Kesho nakueleza ukweli sio lazima atoke Upinzani huyo Rais, atakwambia nani alikupa mamlaka ya kuidhinisha fedha za Stiegler’s Gorge, nani alikupa mamlaka ya kupitisha fedha nanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachotaka sisi hapa, tunataka tu Serikali ifuate utaratibu, kwani tatizo liko wapi? Ni jambo jema, ni kwa nia njema tunakutakia mema na tunakuonea huruma wewe kwa sababu baadaye mimi nitakuwa shahidi kwamba ulikuwa unakataa ushauri ndani ya Bunge na nitataka, hiyo kamati ya uchunguzi utakapokuwa unaenda ndani mimi nitakuja kutoa ushahidi kwa sababu tulishauri, kwa sababu tunayajua haya, sheria zipo na uzuri wa hii nchi ni kwamba sheria zipo, unless otherwise, leo Sheria ya Manunuzi iko likizo yaani iko likizo kabisa hakuna mahali inapotumika yaani mambo yanajitokeza tokeza tu huko, unashangaa tu kitu kimefanyika, baadaye procedure ndio zinafuata, yaani unaanza ku-take action halafu baadaye unafuata procedure. Haya yote yataundiwa Kamati ya Uchunguzi na tawala zinazokuja, miaka minane au mitatu sio mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili nataka tu nimwambie Mheshimiwa Waziri. This is politics, politics lazima ujue namna ya kui-handle, kwa sababu politics ina repercussion, utabaki peke yako na hakuna mtu atakayekuja kukuangalia muda huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukijadili hapa issue ya maji, maji ni kero kwa nchi nzima. Unapitia Mpango hapa unakuta imeandikwa sijui visima kumi na tano; Mpiji, issue za Halmashauri tu, hizi ni issue ndogondogo kabisa. Sera ya Maji inazungumzaje, sera ya maji inataka Mtanzania akichota maji mbali ni mita mia nne, lakini sasa hivi uhalisia ni upi? Wananchi wanapata shida, ukija ukisoma takwimu za Wizara watakwambia maji mijini wanapata kwa aslimia zaidi ya themanini; maji vijijini zaidi ya asilimia sitini na tano, lakini je hali halisi maji yanapatikana? Kauli mbiu ya Serikali inasema tumtue mama ndoo kichwani, ndoo hiyo imetuliwa, tuwe wakweli, ndoo imetuliwa? Jibu unakuta kwamba haijatuliwa na kila mmoja anatafuta mahali pa kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni mambo tunayohoji ya msingi kwa nia njema tu, tengenezeni bajeti ambayo inatekelezeka. Sasa haya yote haya ndio mambo ambayo tumekuwa tukiwaeleza humu ndani na nafikiri Waziri wa Maji aliyekuwepo anajua haya mambo, nini kimemtoa pale sasa hivi? Sasa haya yote ndiyo haya tunayoyazungumza watu wanataka maji, hawataki stori za kwenye vitabu, hizi tumeshachoka nazo. Kwa hiyo sasa hayo ni mambo yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Sekta binafsi, Serikali imeijadili kidogo sana yaani ka-paragraph kamoja tu, lakini ukweli Sekta binafsi imeporomoka. Mabenki yanapata hasara, mzunguko wa fedha umeshuka, mikopo chechefu imeongezeka, watu wanashindwa kulipa madeni, Serikali haijajadili mpango wa namna ya kuiwezesha Sekta binafsi ili iweze kuwa imara, inakuja na sheria, sasa hivi kila siku wanaleta sheria, sasa hivi wanaleta Sheria ya NASACO, yaani kila kitu unataka Serikali ifanye biashara na Serikali yenyewe. Hiyo principle ya wapi, duniani ilishashindwa, kama unafuata policy ya China hawaendi namna hiyo na namna China walivyobadilisha uchumi wao sio kwa staili tunayokwenda nayo, hii ni staili ya kutuvuruga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya yote hatutaki kuyasema lakini ni kwenye vitabu, leo unazungumza ili uchumi ukue ni lazima watu wakose hela, hiyo siyo interpretation sahihi. Kufanya biashara na sekta binafsi sio chanzo cha ubadhirifu wa fedha, kunatakiwa kuwe na namna ya ku- handle wale watu, kuna namna ya kufanya nao kazi na tueleze tu ukweli watu wanahitaji ajira wote tumekuwa tukijadili hapa kuna tatizo kubwa sana la ajira nchini, lakini ajira sio lazima ajiriwe na Serikali; mtu hata akiajiriwa benki pale CRDB anasema nimeshapata ajira yangu; mtu akiajiriwa pale na Mohamed Dewj anasema mimi nimepata ajira; mtu akiajiriwa na Coca Cola anasema mimi nimepata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo nenda kwenye hayo Makampuni yote Coca Cola wamepunguza wafanyakazi, ukienda Mabenki wanapunguza wafanyakazi, lakini yote hapa bado Serikali haijaja na mpango makini wa kuhakikisha kwamba sasa tuna-revamp sekta binafsi iweze kusaidia kwenye uchumi wetu. Sasa haya yote tunajaribu kumwelimisha lakini anakuwa mgumu wa kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimweleze Mheshimiwa Waziri this is politics na ndio iko hivihivi, utakuwa hapo utaondoka, utawala uliopo uko leo, kesho utaondoka, ndiyo maisha yanavyokwenda, tusikilizane, tuelimishane ili tuweze kuelewa wapi tunapotaka kuelekea, kwa sababu tunataka uchumi imara. Sasa hizi sera mnazokuja nazo hizi na NASACO kila siku tunapitisha sheria mpya sisi tunawaangalia tu, zinafukuza wawekezaji, lakini haziruhusu mazingira ya watu kurudi nchini kuwekeza ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya yote ni masuala ya kiuchumi ambayo tunayakwepa kwa sababu na bahati mbaya nchi yetu tunataka nchi ya kijamaa halafu tunataka matunda ya kibepari, haiwezekani! Ni biashara ambayo haipo yaani na hicho ndicho ambacho mimi nakiona kwamba tuko wajamaa lakini tunataka matunda ya kibepari, biashara hiyo haipo.

Sasa Mheshimiwa Waziri lazima akubali na nasoma hotuba yao, tumekwenda tumefuata mpango wake kwa umakini sana na uzuri kitu kimoja tu Mheshimiwa Mpango ndiye yeye aliyeandaa mpango alikuwa Katibu Mkuu wa Mipango, makosa yote anayoyakosoa ya Serikali ya nyuma yeye ndiye aliyeyafanya. Kwa hiyo, akifitisha fito au kufanya nini ni yeye ndiye mwenye haya makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifurahia sana Mheshimiwa Rais alivyomweka Mheshimiwa Mpango pale, nikajua sasa huyu aliyetengeneza mpango sasa atausimamia vizuri. Eeh, bwana eee, kila kitu hamna kitu, biashara hakuna, yaani mambo yanafanyika chini ya standard. Bahati mbaya sana wanataka sifa, yaani kakitu kadogo wanataka wasifiwe, tulieni mambo yanajifanya yenyewe, tekeleza wajibu wako, watu watakupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nashukuru sana. Nafikiri elimu imemwingia, atayafanyia kazi. Ahsante sana.