Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami ili niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mezani. Pia nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii. Moja kwa moja naunga mkono hotuba ya Upinzani iliyowasilishwa kabla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa maendeleo huu utatekelezwa na Watumishi wa Umma, utatekelezwa na wananchi kwa ujumla. Ili Watumishi wa Umma waweze kutekeleza huu mpango wanahitaji kwanza kupata stahili zao zile wanazostahili, kama ni posho, kama ni mishahara, kama ni kupandishwa vyeo ili wawe na morali ya kuweza kufanya kazi kwa kujituma. Vilevile wanahitaji kupata refresher courses za kuwajengea uwezo wa kuweza kufanya kazi zao kwa utaalaam zaidi na hapa linakuja suala la mafunzo kwa ajili ya in service ambayo kwa muda mrefu yamesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watumishi wa umma wanahitaji kutiwa moyo wajue kwamba wanafanya kazi zao, wanaweza kufanya maamuzi bila kuogopa kutumbuliwa. Vinginevyo tutakuwa na utumishi wa umma wenye hofu ambao hauwezi kufanya kazi kwa kujituma na kwa ukamilifu kwa hofu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watumishi wa umma kama hawapati zile stahili zao kwa wakati tutarudi kule tulikokuwa zamani kwenda kufuga kuku – kukimbilia kufuga kuku, kukimbilia kuangalia ng’ombe kazi zinaachwa kufanyika ofisini. Kwa hiyo ni jambo muhimu sana kuangalia suala la Watumishi wa Umma ambao kwa kweli kwa muda sasa hawako vizuri na huo ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengine ambao watatekeleza huu mpango ni wananchi wenyewe na wananchi wanahitaji amani, wanahitaji utulivu. Kuna hawa watu wasiojulikana ambao sasa hivi wamekuwa ni tishio kwetu. Ni lazima Serikali iingilie kati kuwahakikishia wananchi wake usalama wao. Nilikuwa Mkuranga juzi na katika kikao nilikuwa na wananchi tunafanya kikao, wanaogopa hata hizi bodaboda saa 11 hawawezi tena kwenda kwenye maeneo yao wanayoishi kwa sababu ya hofu. Kwa hiyo, tunahitaji Serikali itoe kauli ya kuwahakikishia wananchi usalama wao ili waweze kufanya kazi zao vizuri, kwa sababu bila kuwa na uhakika na usalama hata shughuli za kiuchumi hazitafanyika kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Serikali za Mitaa na Local Government inayo historia. Tulipopata uhuru tulikuwa na Local Government ambayo ilikuwa na nguvu sana, lakini Serikali ya wakati huo ikaona kwamba pengine ni ku- centralize, tuka-centralize Serikali, tukaua Local Government lakini hatukufanikiwa. Serikali ikarudisha tena Local Government kwa sababu Tanzania ni nchi kubwa sana, ina kilometa za mraba 945,000 ni kubwa sana haiwezekani ikatawaliwa kutoka Serikali kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo sasa matokeo ambayo yamekuwa yanaendelea kutokea sasa hivi inaelekea kuziua Serikali za Mitaa na kuzipunguzia nguvu za kuendesha shughuli, wakati tunajua wazi kabisa kwamba Serikali za Mitaa ndiyo kwenye huduma za afya, ndiyo kwenye barabara, ndiyo kwenye elimu na maji. Kama Serikali za Mitaa hazitapewa uwezo wa kutosha, uwezo kwa maana ya rasilimali watu na uwezo kwa namna ya rasilimali fedha, huu mpango ambao tunauleta hauwezi kufanikiwa kwa sababu utekelezaji uko kwenye Serikali za Mitaa na ndiyo kwenye wananchi. Ina maana basi huu mpango hautafanikiwa na maendeleo tunayotaka kuleta Tanzania ya viwanda haitaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu kwanza mwaka huu ilipangwa bajeti kama (approximately) ya bilioni 12, lakini iliyotoka ilikuwa ni bilioni moja tu na point ambayo ni about 11 percent. Sasa kwa mtindo huu, sijui kama kweli huko tunakokwenda Serikali hii itafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwenye Local Government kama nilivyokwishasema awali na wengine pia wameshachangia, tumenyang’anya Local Government property tax, tumewanyang’anya ushuru wa mabango, ruzuku haiji kwa wakati sasa hiyo Local Government ambayo tunataka ifanye kazi itafanyaje kazi kama haipati resources?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba Local Government inafanya kazi kwa niaba ya Serikali kwa sababu Serikali kuu imekasimu madaraka kwa Local Government. Kwa hiyo kama Serikali ya Mitaa inafanya kazi, inafanya kazi kwa niaba ya Serikali, kama Serikali ya Mitaa ikishindwa ina maana Serikali Kuu na yenyewe imeshindwa. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuimarisha Serikali za Mitaa ziweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye rasilimali watu tunahitaji kwa ajili ya huu mpango kufanikiwa. Katika mpango ule wa mwaka 2016/2017 - 2020/2026 wa mwaka jana ambao uliwasilishwa kulikuwa na taaluma ambazo ziliainishwa, kulikuwa na Wahandisi, watu wa construction, watu wa agriculture na yalitolewa malengo. Kwa mfano, katika agriculture na zingine lengo lilikuwa ikifika mwaka 2025 wataalam 145,000 wanategemewa kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika mpango wa sasa hivi kuna maeneo kwenye training kuna taaluma mbalimbali ambazo watu wanakwenda kusomeshwa. Swali langu ni kwamba tumeweka target hiyo ya 2025 na intervention 2015/2016 kwa mfano kwenye agriculture tulitegemea tuwe na wataalam 4,475, sasa napenda kujua, tukifananisha lengo lile la 2025 na tulivyoanza 2015/2016 kwa kuainisha kada zile ambazo zinatakiwa kufikiwa, je, tumekwenda vipi mpaka sasa hivi huu mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia Wabunge tuweze kufuatilia utendaji kazi wa Serikali katika kufikia yale malengo ambayo yameainishwa. Kwa hiyo, nitapenda sana kujua Serikali imefikia wapi katika kuainisha hayo malengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kila siku kilimo ni uti wa mgongo na sio uti wa mgongo tu, kilimo ndiyo kitatoa malighafi kwa ajili ya uchumi wa viwanda. Nimeangalia katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri, ameainisha tu activities ambazo zinatakiwa kufanywa kwa ajili ya kilimo lakini sijaona mahali popote ambapo ameainisha kwa mfano, watalaam wa kilimo hasa Maafisa Ugani ambao ndiyo wanaokwenda kuwasaidia wakulima katika uzalishaji, sijaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata katika sikumbuki ukurasa wa hii ripoti ya sasa hivi ambapo imeainishwa taaluma mbalimbali nimeona watu wa VETA, sijui watu wa mambo ya hoteli, sijaona popote wameainishwa Maafisa Ugani ambao ni muhimu sana kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuweza kulima vizuri na kwa kitaalam waweze kupata mazao ya kutosha. Kwa hiyo, ningependa kujua ni kwa namna gani Maafisa Ugani watapanga ili tuweze kupata Maafisa Ugani wa kuweza kwenda kusaidia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Serikali tuwe na Maafisa Ugani wa kutosha kama ambavyo tulivyo na Madaktari kwa ratio tunasema kila Daktari mmoja anatakiwa kutibu wagonjwa 10,000. Tuwe na ratio pia kwa ajili ya Maafisa Ugani kwa ajili ya wakulima kusudi Afisa Ugani aweze kuwafahamu wakulima wake kwa umakini na shida zao, wawezeshwe kwa kupewa hata pikipiki waweze kuwafikia wakulima, ndiyo tutaweza kuleta kweli mapinduzi ya kilimo katika nchi hii. Bila hivyo itakuwa ni kuzungumza hapa kila siku, tutaondoka, mambo yatabaki hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la mikopo ya wanafunzi. Kama tunavyojua sasa hivi wanafunzi wengi hawajapata mikopo. Naishauri Serikali iangalie tena upya hii Sera na utekelezaji wa mikopo. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu, kwanza na-declare interest kwamba mimi ni mmojawapo walioanzisha Bodi ya Mikopo, sababu ilikuwa ni kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)