Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Serikali kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kutoa pongezi kwa Waziri pamoja na Mawaziri wote kwa sababu mpango ni shughuli shirikishi, wamefanya kazi kubwa katika kuandaa dira hii ambayo sasa tunaichangia ili tuweze kuiimarisha zaidi, iweze kutupeleka kule tunakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa ambayo inaendelea mpaka sasa. Mradi wa reli kwa kiwango cha standard gauge ni kazi kubwa, kuimarisha pia Shirika letu la Ndege ni kazi kubwa, kuendelea kuisimamia na kuimarisha sekta ya madini nayo ni kazi kubwa inayohitaji pongezi kubwa sana kwa Serikali, kuimarisha sekta ya usafirishaji pia ni kazi kubwa sana kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, pia kusimamia nidhamu kazini na kuendeleza ujenzi wa viwanja mbalimbali vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti nianze kwa kusema tu kwamba tunaingia katika utaratibu wa utekelezaji wa bajeti wa mwaka 2017/2018 ambao tumeshauanza, lakini pia tunazungumzia mpango kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka unakuja. Lipo jambo ambalo tunapaswa pia tuliulize na Serikali iendelee kulifanyia kazi kutokana na utekelezaji hafifu wa bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma mpango katika ukurasa wa 20 inaonesha kwamba katika mwaka wa fedha 2016/2017 ni asilimia 55 tu ya fedha ya miradi ya maendeleo zilizokwenda kwenye miradi yetu. Hii inaleta picha ifuatayo:

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunapaswa kuongeza upya vyanzo vyetu vya mapato, lakini inawezekana pia kuna mahali ambapo tunazo sheria zinazotukwaza katika usimamizi wa fedha lakini tunahitaji kuongeza juhudi kubwa katika kusimamia na kudhibiti matumizi na mapato ya Serikali. Naikumbusha Serikali kwamba katika bajeti ya 2016/2017 ilikuwa ime-allocate fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Baadhi ya fedha bado hazijafika katika miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali iweke msisitizo mkubwa katika mpango huu kwa kuhakikisha kwanza tunakwenda kuimarisha au kutatua kero za wananchi kwa ile miradi ambayo inagusa huduma za jamii, hususani maji, umeme na afya. Haya ni mambo ambayo napenda Serikali yangu iyape kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuikumbusha Serikali kwamba bado ina kazi ya kuendelea kusambaza fedha za miradi ambayo iliahidiwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Katika mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Mji wangu ilitengewa fedha shilingi milioni 599 kwa ajili ya uchimbaji wa mifereji na usambazaji wa maji ya bomba, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi tunavyozungumza fedha hizo hazijafika katika Halmashauri ya Mji wa Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inachelewaesha kuanza kwa mradi lakini inaongeza kero kwa wananchi kwa sababu tayari wameshachimba mifereji na sasa wanasubiri fedha. Nimezungumza na Waziri wa Maji amesema kwamba fedha hizo tayari ameshazi-approve kutoka Wizarani lakini zimekwama Hazina. Namwomba Mheshimiwa Mpango ahakikishe fedha hizi zinakwenda haraka kwa sababu mvua zikinyesha mifereji ambayo walichimba wananchi kwa njia ya kujitolea itaziba, hatimaye tutaanza tena kupigizana kelele na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na suala la maji kuna suala la umeme, kila Mbunge anayetoka Kanda ya Kusini lazima azungumze kuhusiana na suala la umeme. Tuna kero kubwa sana katika eneo hili tumezungumza mara nyingi na Waziri, tumezungumza mara nyingi na Watendaji wa TANESCO. Ukweli ni kwamba hali ya umeme katika Mikoa ya Kusini ni mbaya sana na ubaya zaidi kwamba ni kipindi sasa cha takribani miaka miwili ahadi ambazo tumekuwa tukipewa ili kuondoa tatizo la umeme hazikamiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Naibu Waziri amezungumza kwamba mwisho itakuwa mwezi wa Disemba tatizo la umeme litakuwa limekwisha. Tunaomba Waziri wa Fedha, tunaomba Waziri wa Nishati ahakikishe kwamba tatizo hili kweli linakwisha kwa sababu wananchi wanashindwa kufanya biashara, wananchi wanashindwa kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa sababu tatizo la umeme ni kubwa sana. Kitu kikubwa kinachowaumiza wananchi wa Mikoa ya Kusini ni kwamba Kusini ni chanzo cha gesi ambayo pia inatumika huku katika miji mingine kwa ajili ya kusambazia umeme, kwa nini tuna shida kubwa kwa kiwango hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa napitia mpango, sioni mahali ambapo kuna mpango wa kuimarisha au kufufua viwanda vyetu vya korosho. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza, binafsi nimemwandikia barua Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na pia nimepeleka barua Wizarani kwake na kumkabidhi Katibu, tunaomba maelezo ya kina kwa nini Kiwanda cha Korosho cha Masasi hakifufuliwi? Nani kapewa kiwanda kile na mamlaka gani imemfanya akifanye kuwa ghala la kuhifadhia korosho badala ya kuleta mitambo na kubangua korosho. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inalitatua na inalishughulikia kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niseme kidogo katika suala la kilimo, tunashukuru Serikali watu wa Kusini tukizungumzia kilimo tunazungumzia korosho, tunaishukuru sana Serikali kwa hatua iliyofikia, korosho inauzwa vizuri lakini zipo changamoto ambazo tungependa Serikali iziangalie. Kwa mfano, tumepata changamoto kubwa ya uhaba wa pembejeo katika mwaka wa fedha uliopita lakini ninaposoma mpango huu sioni mahali ambapo Mheshimiwa Mpango ameonesha usambazaji wa pembejeo aina ya sulphur utakavyokuwa kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019. Tunaomba eneo hilo liingizwe ili tuweze kuona namna gani sasa Serikali inawasaidia wakulima wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo eneo lingine ambalo ningependa kuikumbusha Serikali, tunayo miradi ya barabara ambayo inaendelea na mengine inaendelea kwa taratibu mno, tunayo barabara yetu ya kutoka Nanganga kuelekea Nachingwea – Masasi, barabara hii hatuoni kazi inayofanyika kwa kweli, tungeomba Serikali iongeze juhudi na kutoa fedha za zakutosha barabara hii ikamilike ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ya kutokea Mtwara inakwenda Tandahimba, inakwenda Newala, inakuja Masasi nayo hii hatuoni Serikali kama ina kasi kubwa ya kutaka kuimaliza tunajua kazi imeanza, tunaomba Serikali iongeze fedha za kutosha katika mwaka wa fedha ujao na mwaka wa fedha huu ili tuweze kukamilisha barabara hizi kwa ufanisi zaidi na kwa haraka ziweze kupitika tuwe tumetekeleza tuliyowaahidi wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wetu kuna eneo la kufunganisha maendeleo ya watu na shughuli za kiuchumi. Nataka niseme kidogo katika eneo la elimu, mwaka wa kwanza nilichangia na jambo hili nililisema halikuwepo katika mpango mpaka last version, mwaka wa pili nilichangia tena na mwaka wa tatu huu nachangia. Hakuna nchi inayoweza kuendelea duniani katika sekta ya elimu bila ya kufikiria namna ya kuendeleza sekta ya elimu isiyo rasmi, elimu nje ya mfumo rasmi. Jambo hili nalieleza mara nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo matamko yanatolewa na viongozi wetu, kwa mfano mtoto akishapata mimba haruhusiwi tena kusoma, tunajiuliza mtoto yule anatakiwa aende wapi? Wapo watoto ambao wanashindwa kumaliza elimu ya Sekondari kwa sababu mbalimbali zikiwemo za utoro, umaskini uliotopea na mambo kadha wa kadha. Wapo ambao pia wameacha kusoma shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na wingi wa wanafunzi tulionao katika elimu rasmi watu ambao wanahitaji elimu walio nje ya mfumo wa elimu rasmi ni wengi zaidi. Nataka nikupe tu mfano mdogo, kwamba katika sensa ya watu iliyofanyika mwaka 2012 watu milioni 5.5 sawa na asilimia 22.4 ya Watanzania walionekana hawajui kusoma na kuandika. Ukisoma ripoti ya UNESCO ya mwaka 2014 inaonyesha kwamba tatizo hili linaendelea siku hadi siku...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)