Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na nimshukuru sana Mungu kwa kunijaalia afya njema ya kuongea hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze haraka katika mchango wangu kwenye taarifa hii au na hotuba hii iliyoletwa mbele yetu ya Waziri wa Fedha na Mipango. Nijielekeze moja kwa moja kwenye ukurasa wake huu wa 29.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kukuza uchumi wa viwanda ni lazima kabisa ujielekeze katika mpango huu moja kwa moja. Kwa bahati nzuri sana Mheshimiwa Mpango ameandika vizuri sana hapa kwamba kuna miradi ya vielelezo na miradi ambayo itatausaidia Tanzania kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Sasa basi ninaomba kutokana na mpango huu ambao ameandika hapa kwenye suala hili la gesi na naomba nijielekeze kabisa katika suala la gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gesi; ameandika vizuri hapa kwamba Serikali inataka kujielekeza katika kujenga mtambo wa kusindika gesi ya kimiminika. Sasa basi ni kweli kwamba miradi hii iko mingi na nimetaja huu mmoja ili walau Waziri Mpango anielewe. Leo hii gesi Mnazi Bay imezalishwa vya kutosha. Lakini ukiangalia wataalam wanatuambia gesi pale inazalishwa na inaweza kutumika kwa kipindi cha miaka 70. Ukiangalia matumizi ya gesi pale hayafiki asilimia 25 mpaka 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji aliyewekeza gesi pale amewekeza kwa bilioni za pesa za kutosha. Sasa ukiangalia gesi inayotumika sio ya kutosha na kwa kuwa sisi tuna gesi na tunataka sasa kutengeneza na kuisadia Tanzania kwenda kwenye uchumi huu na Mwenyezi Mungu ametujaalia kupata gesi, naomba mpango huu basi kadri ulivyoandikwa hapa ujielekeze kutumia gesi ili walau gesi hii ambayo Mungu ametupatia isaidie basi kwenda kwenye viwanda hivi vilivyoanzishwa sasa katika eneo lote la viwanda na Serikali iweke basi mazingira wezeshi ya kujengwa kwa viwanda maeneo yale ambayo bomba la gesi linapita, kwa kufanya hivi tutasaidia uchumi upande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi utapanda kwa sababu ukiangalia katika bajeti ya Serikali ya mwaka uliopita, Serikali inaagiza mafuta kwenye bajeti yake zaidi ya robo inatumia kwa kuagiza mafuta nje. Kwa kuwa nishati ya mafuta inaagizwa kwa kutumia fedha za walipa kodi, nimshauri Mheshimiwa Mpango na wachumi wengine waone namna gani ya kufanya kitaalam ili walau gesi hii iweze kuendesha mitambo, tukaachana au tukapunguza kiwango cha matumizi ya mafuta, tukatumia gesi kwa sababu gesi imechimbwa pale na gesi hii ni bure tunaweza kutumia tunavyopenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ikitokea leo Serikali inaamua hata wenyewe tu kwa magari ya Serikali ikaondoa mfumo wa kutumia petroli kwenye magari tukatumia gesi ambayo imo imezalishwa pale, Tanzania tutasogea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Serikali nayo ikiamua kutumia wachumi wetu kushauri na wataalam tulionao nchini wakajenga sheli za kutumia gesi, magari yetu na magari mengine ya Serikali yakabadilisha huo mfumo ikawekwa sheli nyingine Dar es Salaam, ikawekwa sheli
nyingine Arusha, tukawekewa sheli nyingine huko Kigoma, mtandao wa gesi ukaundwa katika nchi yetu, hii nchi ya Tanzania hii itasonga mbele kwa sababu tuna gesi asilia na wataalam wametuambia gesi yetu ni pure yaani haihitaji zaidi kubadilishwa na kitu chochote. Tunapata, tunaweka kwenye matumizi na tunaweza kujengewa uwezo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ukiangalia leo hii TPDC uwezo wao wa kuuza gesi ni mdogo sana, ni mdogo kwa sababu tunaona kabisa wale wawekezaji walioko kule wanaidai Serikali pesa kubwa sana na kwa sababu pesa hii ni nyingi zaidi ya dola milioni 20 na ukiangalia uwezo wao wa kutumia siyo mkubwa na TANESCO ni shirika letu la Kitanzania linalojiendesha kwa hasara. Kama Serikali itaamua kuweka mpango huu vizuri, na mimi leo nimeamua kuelekeza mchango wangu katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuisaidia sana Tanzania kwenye sekta ile ya madini, nimuombe tena kupitia Bunge hili achungulie tena hili eneo la gesi kwa sababu eneo la gesi mimi siamini kama gesi hii inashindwa kutusaidia Watanzania. Nina wasiwasi na gesi hii ambayo kimsingi haitumiki ipasavyo. Kwa nini nasema haitumiki ipasavyo? Ni kwa sababu gesi tunayo, haitumiki ipasavyo na haiuziki. Kwa bahati nzuri sisi Kamati tumepata bahati ya kutembelea kule na tunaona jinsi ambayo rasilimali hii ya gesi haitumiki vizuri.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kujielekeza katika eneo hili la gesi ili walau gesi basi isaidie mitambo mingi ambayo inasubiriwa saa hizi. Ukiangalia Mheshimiwa Rais siku moja nimemsikia katika vyombo vya habari ametembelea maeneo ya Lindi na Mtwara, kuna kiwanda kikubwa pale cha Dangote, hebu angalia kwa nini mpaka sasa hivi hakijapelekewa gesi ili gesi itumike basi, maana kiwanda kile kikifanya kazi ya kuzalisha saruji bei ya saruji inashuka Mikoani na uchumi wa Tanzania unapanda kwa sababu saruji kule imeshafanyika kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona mchango wangu niuelekeze hapo kwa sababu ninafahamu vizuri matumizi ya gesi ambayo kwa kweli kwa sasa hayatumiwi inavyotakiwa. Pamoja na haya nataka nielezee jambo lingine dogo tu. Katika mpango huu, umeeleza jinsi ambavyo mikopo na jinsi ambayo mikopo chechefu inavyoleta shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana, sasa hivi kuna shida katika maeneo ya mikopo yetu katika mabenki, Mheshimiwa Mpango elekeza sasa namna rahisi ya kusaidia wananchi ili wasiende kupigwa huko katika suala la mikopo, wanapata uchungu kupewa riba ya juu sana. Sasa naomba Mpango huu basi tunapoenda mwaka huu wa 2018/2019 usaidie eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliamua kuyasema haya na huu ndiyo mchango wangu kwa leo. Ahsante sana.