Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE.RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata fursa hii ya kuchangia. Awali ya yote kwanza niunge mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mpango wa maendeleo, na nishauri kwamba Serikali ijitahidi kuzingatia yale ambayo yatakuwa yanaweza kusaidia kuboresha Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilitaka nizungumzie suala la makusanyo ya Halmashauri, kama ambavyo Mpango unaonesha, kwamba una lengo la kukusanya shilingi bilioni 847.7 kwa mwaka 2018/2019. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napata mashaka sana kuhusu Mpango huu wa Serikali kama kweli unaweza kutekelezeka, kwa sababu mwaka 2017/2018 malengo yetu ni kukusanya shilingi bilioni 687.3, lakini bahati mbaya vyanzo vyote vingi vya Halmashauli vile vikubwa vimechukuliwa. Maeneo ya Halmashauri za Wilaya, ushuru wa mazao umechukuliwa kwa kiwango kikubwa na kwa bahati mbaya mkuu wetu wa nchi anapopita anawashauri wananchi kwamba kuanzia asubuhi mpaka jioni wasafirishe tani moja moja mpaka jioni, watakuwa wamekwisha kamilisha lengo la kusafirisha tani moja moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba Halmashauri za Wilaya ukusanyaji wa mapato kupitia kwenye mazao utakuwa mdogo sana, lakini kwenye Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji ukusanyaji wa proper tax, ukusanyaji wa kodi za matangazo kwa maana ya posters na billboards utakuwa umeshuka kwa sababu tayari kodi hizi zinakusanywa na TRA. Sasa napata mashaka ni namna gani tutaweza kufikia lengo la hii shilingi bilioni 847.7 kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu basi atuoneshe mpango mkakati wa kuhakikisha tunafikia malengo ya kupata hii shilingi bilioni 847.7 katika halmashauli zetu ili tuweze kufikia malengo ya mapato ya ndani ya nchi yetu tunayo tarajia. Vilevile katika eneo hili la halmashauri utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2017/2018 uko katika kiwango cha chini sana katika Halmashauri zetu nyingi. Miradi mingi ya maendeleo fedha hazijaja, sasa nilikuwa naomba wakati Mheshimiwa Waziri atakapojibu atusaidie ni kwa namna gani watazisaidia Halmashauri ili zitekeleze miradi yake ya maendeleo kwa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akatuambia katika mpango wake, nini malengo yake hasa kuhusu Halmashauri, malengo ya ukweli kabisa kuhusu Halmashauri na dhamira ya Serikali hasa kuhusu Halmashauri. Kwamba dhamira ni kuzifanya Halmashauri ziwepo ama dhamira ni kuziua Halmashauri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima haya mambo yawekwe bayana ili tuelewe maana inavyoonekana Serikali ya Awamu ya Tano dhamira yake kubwa ni kuziua Halmashauri. Unapoondoa uwezo wa Halmashauri kukusanya maana yake unazifanya zisiwe na mapato. Na kama unazinyima mapato, maana yake unazinyima uwezo wa kujiendesha. Leo Halmashauri nyingine hazina uwezo wa kulipa hata posho za Madiwani, sasa zitajiendesha namna gani? Ni vizuri Serikali ituoneshe kiukweli kabisa kwamba dhamira yenu hasa nini? Dhamira yenu kwamba Halmashauri ziwepo kama ilivyokuwa mpango wa awamu, dhamira ni kuziuwa Halmashauri? Ili kama ni kuziua Halmashauri tuondokane na Halmashauri, tuachane na mzigo wa kuwa na Madiwani ambao hawana kazi, kuwa na Wakurugenzi ambao hawana kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana maana leo katika halmashauri zetu utakuta wanao-dictate mipango ya Halmashauri sasa wanakuwa ni Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa kwa sababu power ya Halmashauri imeondoka kwa sababu hawana fedha hawana chochote na inaonekana dhamira ya Serikali Kuu ni kuziua Halmashauri. Kwa hiyo niombe, kama mpango bado ni kuziboresha Halmashauri basi turudi katika mpango wetu, tuonyenyeshe ambavyo tutaziboresha na kuzisitawisha halmashauri zetu ili ziweze kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika malengo tulikuwa tumejipangia kwamba angalau Halmashauri zetu nchini zijitegemee kuanzia kwa kiwango cha chini asilimia 35 mpaka asilimia 50, ili zimpunguzie Mheshimiwa Raisi na Serikali mzigo wa majukumu madogo madogo, yale ya chini na Serikali ijihusishe na majukumu makubwa kama ya reli na ndege, lakini mambo ya vituo vya afya, zahanati, shule za msingi yashughulikiwe na Halmashauri kwa kiwango cha kutosha. Mheshimiwa Waziri naomba sana uonyeshe jinsi ambavyo umepanga kujielekeza katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo mpango huu unaelekeza kwamba utapunguza umaskini wa wananchi utaendelea na jambo ambalo likizungumzwa mara kwa mara katika mipango yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri atuambie kama kweli mpango wa Serikali ni kupunguza umaskini wa Watanzania, na leo tunapata ujasiri wa kubomoa nyumba za wananchi bila huruma, nyumba ambazo wananchi wamejenga wengine kwa utaratibu, lakini tunazibomoa kwa kisingizio kwamba ziko katika hifadhi ya reli na hifadhi ya reli ni mita 30 kuna nyumba ambazo zipo nje ya mita 30, zimeishi katika maeneo hayo zaidi ya miaka 50, leo tunawabomolea wale wananchi hivi dhamira yetu ya kupunguza umaskini wa hao wananchi iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ambayo wananchi wana vibali vyote vya ujenzi, taratibu za kubadilisha matumizi ya maeneo hayo zimefanyika, lakini leo wananchi wale wanaambiwa walifika maeneo hayo baada ya mpango reli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefuatilia mpango wa ramani ya reli, hawana ramani ambayo imepitishwa na Wizara ya Ardhi, wananchi wana eneo ambalo limepitishwa na Wizara ya Ardhi na Serikali ni moja. Wizara ya Ardhi ni moja, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi yote ni Serikali, sasa inakuwaje leo watu waliopewa ruhusa na Wizara ya Ardhi wavunjiwe maeneo yao bila kulipwa fidia wakiambiwa kwamba wamevamia maeneo? Hivi inakuwaje eneo ambalo watu wamepewa kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi hii waambiwe wamevamia hayo maeneo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri kama ana dhamira ya kupunguza umaskini wa Watanzania awasaidie watu wanaovunjiwa nyumba zao wakati wametimiza masharti yote na wana hatimiliki za maeneo ambayo wanayomiliki ili wananchi wawe salama na wawe na mioyo yenye furaha yenye amani. Kama ni dhamira kufanya nchi iwe yenye utulivu basi tuwafanye wananchi wetu pia wawe na mioyo yenye utulivu na tuwasidie wananchi hawa ambao ni maskini ambao wamejenga hizi nyumba kwa hali ngumu sana, leo wanavunjiwa kirahisi kama vile hizo nyumba zimeanguka kutoka mbinguni. Naomba sana Serikali ilione hii kwa uzito wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mikopo ya elimu ya juu. Hotuba ya Kambi ya Upinzani imejaribu kuzungumzia suala la mikopo ya elimu ya juu. Ni vizuri Serikali ibainishe inaweza kukopesha wanafunzi wasome ama haiwezi? Ni vizuri tuweke bayana, kwa sababu kama tunahitaji kuwasaidia wanafunzi na wanafunzi hawa ni watoto wa maskini, maskini tunaowafahamu wana-qualify kukopeshwa lakini hawakopeshwi kwa sababu Serikali haina uwezo, inaonekana kuna ubaguzi kwa sababu kuna ambao wanakopeshwa na ambao hawakopeshwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuondoa hii hali ya ubaguzi ama tuondoe mikopo ama kama tunatoa mikopo tutoe mokopo kwa watu wanaostahili kupewa mikopo kama jukumu la Serikali ya nchi hii. Na kwa sababu ni kweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ilijitanabaisha kwamba wananchi wenye kuhitajiwa kukopa watakopeshwa wote bila mmoja kukosekana basi Serikali itimize wajibu wake huo vya kutosha ili wanafunzi wasikose haki yao ya msingi ya elimu ambayo ni haki ya Kikatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana katika Mpango huu Mheshimiwa Waziri atujibu ni wakati gani watamaliza tatizo la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu bila kuonesha aina yoyote ya ubaguzi kama inavyoendelea sasa hivi? (Makofi)

Kuhusu suala la utalii, hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni imeonesha jinsi ambavyo VAT kuwekwa katika utalii ilivyoathiri utalii katika nchi hii. Malengo yetu ni kuifanya nchi hii ishindane na nchi nyingine katika utalii, bahati nzuri nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii, tunategemea kwamba tungekuwa tuko katika hatua ya juu sana katika utalii. Ni vizuri pia Mheshimiwa Waziri akatueleza ni watalii kiasi gani ambao wameingia kipindi hiki ukilinganisha mwaka uliopita, na ni mpango gani uliopo katika Serikali hii kuingiza watalii zaidi kipindi cha mwaka 2018/2019? Tushindane na nchi ambazo zina vivutio kama vya kwetu, haiwezekani nchi ambazo hazina vivutio kuliko vya kwetu zitushinde katika kuingiza idadi kubwa ya watalii katika nchi hii. Kwa hiyo ni vizuri tuangalie sana mfumo wa kodi katika eneo la utalii ili itusaidie katika kuongeza idadi ya watalii katika nchi yetu na ukizingatia kwamba Mlima Kilimanjaro ni moja wapo wa vitega uchumi muhimu sana katika nchi yetu, ni vizuri tuone jinsi ambavyo tunaweza kuutumia ule mlima kutuingizia mapato ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka pia niongelee suala la mfumo wa kodi. Mheshimiwa Waziri kwenye mpango wake ameonyesha kwamba angalau wananchi wameonesha ku- comply kulipa kodi, ameonesha kuwa wananchi wengi wameingia kwenye mfumo wa EFD machine. Ni kweli, sasa ni wakati wa mpango wetu Mheshimiwa Waziri uoneshe namna gani tunaangalia upya sera ya kodi na mfumo wa kodi ili sera hii ya kodi na mfumo wa kodi ifanye kodi ilipike kwa wafanyabiashara vizuri zaidi. Kwa sababu kodi ikilipika vizuri maana yake ni kwamba watu wengi watakuwa wanafanya biashara na uchumi wetu utapanuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi tulionayo sasa hivi hailipiki ndiyo maana watu wengi inabidi waingie kwenye mfumo wa rushwa ili wakwepe kulipa kodi. Kwa hiyo, watu wengi wanakwepa kodi kwa sababu ya viwango vya kodi kuwa vikubwa pamoja na mfumo wa kodi kuwa mgumu. Kwa hiyo tuangalie kwa kiwango cha kutosha mfumo wetu wa kodi ili kodi yetu ya nchi hii ilipike na wafanyabiashara wapate nafuu katika kufanya biashara zao. Ili wasifunge biashara zao kama ambavyo wanafunga sasa, ili wasigombane na TRA kama wanavyogombana na TRA sasa, tuwafanye watu wa-comply kulipa kodi wenyewe na Mheshimiwa Waziri unafahamu kodi nzuri ni ile inayolipika. Sasa kama kodi hailipiki maana yeke hiyo kodi inapoteza ule uzuri wake, naomba Mheshimiwa Waziri hilo lifanyiwe kazi kiasi cha kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la viwanda. Suala la viwanda katika nchi hii tunalolizungumza ni jambo bora; ni jambo la msingi kuifanya nchi hii kuwa ya viwanda. Hata hivyo tunazungumzia viwanda vya vyerehani vitatu, vinne, vitano ndivyo tunavyovipigia kelele, lakini kuna viwanda vimebinafsishwa katika nchi hii, tumeendelea kusema viwanda vile virudishwe kwa watu ambao wana uwezo wa kuviendesha, lakini havirejeshwi mpaka sasa hivi. Watu wamekalia viwanda vimekuwa magofu halafu tunaendelea kupiga kelele viwanda vidodo vidogo. Sawa, hata hivyo ni viwanda, lakini hivi viwanda vikubwa lazima vifanyiwe kazi, virejeshwe katika uendeshaji. Viwanda havifanyi kazi, vimekufa na vilikuwa viwanda vyetu vya kodi ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama waliopewa wameshindwa kuviendesha wavirejeshe kwa wanaoweza kuviendesha. Kilimanjaro viwanda vingi vimelala kwa sababu tu watu wamevichukua na haviendeshwi. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri utusaidie katika mpango wako, nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba viwanda vilivyobinafsishwa vinarejeshwa kwa watu wanye uweza kuviendesha kama wale waliokuwa wamepewa wameshindwa kuviendesha ili vifanye kazi viongeze ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho nataka kuongea katika siku ya leo ni suala la sekta binafsi. Serikali inakuwa kama inajinadi kwamba ina dhamira ya kusaidia sekta binafsi lakini katika uhalisia tunaonekana hatuna dhamira ya kusidia sekta binafsi. Leo tunavyozungumza sekta binafsi haikopesheki, benki haziwezi kukopesha sekta binafsi, na watu wengi wa sekta binafsi wanafunga biashara zao kama hotuba ya Kambi ya Upinzani ilivyosema. Hatujafanya tathimini ya kutosha ni kwa nini watu binafsi wafunge biashara zao? Hatujafanya utafiti wa kutosha ni kwa nini leo benki haziwezi kukopesha sekta binafsi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujafanya utafiti wa kutosha ni kwanini benki zishindwe kukopesha. Mheshimiwa Waziri ni lazima mpango wako utuoneshe ni namna gani mmejipanga kuhakikisha kwamba mnasaidia sekta binafsi na mnazisaidia benki zikopeshe sekta binafsi. Hatuna sababu ya kujenga ugomvi na benki zetu, hatuna sababu ya kujenga ugomvi na sekta binafsi kwa sababu sekta abinafsi ndiyo chachu muhimu sana yakuinua uchumi wetu. Huko nyuma Serikali ilishajitoa kufanya biashara, leo Serikali mnakuja sana katika kufanya biashara. Sasa wakati mnakuja kwa kasi isaidieni sekta binafsi kwa sababu ndiyo inayoinua uchumi katika dunia hii. Mheshimiwa Waziri mpango wa Serikali utusaidie sekta binafsi ili sekta hizo binafsi zisaidie malengo ya Serikali ya kufikia uchumi wa viwanda, malengo ya Serikali ya kuinua uchumi wa nchi hii, malengo ya Serikali ya kuondoa umaskini wa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante sana.