Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba nianze kwa kukushukuru wewe na Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama na kutoa mchango wangu katika sekta ambayo, ili kuendelea katika mambo manane, ardhi ndiyo ya kwanza; bila kuwa na ardhi hatuwezi kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kwa sababu nne (4) zifuatazo:-

Kwanza, kitabu cha hotuba kimeandaliwa vizuri sana, maneno machache, takwimu kwa wingi.

Pili, Mheshimiwa Waziri William Lukuvi, Naibu Waziri Mheshimiwa Angelina Mabula, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na timu yake, wanafanya kazi nzuri sana ya (kupigiwa mfano). Ni ukweli usiopingika kuwa, watendaji walio wengi wa Wizara ya Ardhi wamebadilika, hongereni sana, ongezeni bidii zaidi ili muwakomboe Watanzania hasa wanawake.

Tatu, mipango ya kusikiliza kero za wananchi; naunga mkono kwa sasa, Wizara imeweka mipango mizuri ya kutatua kero za wananchi kupitia Mabaraza ya Ardhi, Mahakama za Ardhi, Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Mikoa na Halmashauri za Wilaya.

Nne, Hati zilizofutwa/kurudishwa kwa wananchi; naunga mkono kwa sababu Serikali imefuta baadhi ya hati ambazo zilimilikiwa na watu wachache kwa muda mrefu bila kuendelezwa na kurudishwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri ninayo mambo ya kuishauri Serikali katika, sehemu chache nilizochagua kuzitilia mkazo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, mpangilio wa Matumizi ya Ardhi, Wanawake na kumiliki Ardhi, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata fursa, katika umiliki wa ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Kijiji ya 1979 kifungu cha (4-5). Katika kutoa nafasi ya umiliki wa ardhi kwa akinamama bado taratibu za kimila hazitoi fursa kwa wanawake hasa wa vijijini kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, Serikali itazame upya taratibu za kimila kwa kuzifanyia marekebisho ili kutoa fursa kwa akinamama kumiliki ardhi. Ningependa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha Hotuba yake atuambie na wanawake wasikie kwamba, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha taratibu za kimila ambazo ni kandamizi zinazowanyima wanawake fursa ya kumiliki ardhi sambamba na wanaume zinaondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, migogoro ya wakulima na wafugaji, hifadhi na wananchi; pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya kutatua migogoro ya ardhi, bado tatizo ni kubwa. Ushauri wangu, Serikali itafute fedha ya kupima ardhi yote ya Tanzania. Ni muhimu sasa Serikali Kuu itafute fedha hata kwa njia ya mkopo kwa ajili ya kupima ardhi yote ya Tanzania na kupanga matumizi bora ya ardhi. Kila eneo lipangiwe matumizi yake ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya Watanzania wengi. (Suala la kupima ardhi lisiachwe kwa Halmashauri iwe ni ajenda ya Kitaifa).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, utoaji wa Hati za Viwanja; pamoja na kazi nzuri ya utoaji wa hati kwa wakati, bado wananchi wanaotumia ardhi karibu asilima 80 hawana hati miliki. Mfano; katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali iliahidi kutoa hati miliki za ardhi 400,000 lakini hadi kufikia tarehe15 Mei, 2017, Serikali ilikuwa imetoa hatimiliki 33,979 tu, sawa na asilimia 8.5 ya lengo zima (ukurasa 18). Kiwango hiki ni kidogo sana ukilinganisha na uhitaji wa hatimiliki hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, Serikali iweke mipango itakayohakikisha wananchi wote wanaotumia ardhi wanapata hati miliki. Matokeo ya mipango hii ni kwamba, viwanja vya wananchi vitawaletea tija kwa kutumia hati zao kufikia fursa za kiuchumi. Pia Serikali itapata mapato ya uhakika; sasa wananchi watakuwa wanalipia kwa mujibu wa sheria (kodi ya kila mwaka). Swali langu, je, Serikali imejipangaje kwa mwaka 2017/2018, kuhakikisha lengo la utoaji wa hati miliki ili kuendana na kasi ya ongezeko la idadi ya watu na mifugo inafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, Mipango Miji; pamoja na kuipongeza Serikali kwa kuhakikisha Miji na Majiji yanapangwa. Naomba niishauri Serikali, kuhakikisha Miji yote inakuwa na master plan ili kuondoa tatizo la kuwa miji holela ambayo haikupangwa halafu baadaye tunapotaka kujenga miundo mbinu tunalazimika kuhamisha wananchi waliojenga kabla ya miji kupimwa na kusababisha hasara kwa Serikali, kulipa fidia pia ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme na zinapotokea ajali za moto tunashindwa kuwafikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, Ujenzi wa Nyumba unaofanywa na National Housing na Kampuni ya Watumishi Housing: Pamoja na kulipongeza Shirika la Nyumba na Kampuni ya Watumishi Housing kwa kujenga nyumba na kuwakopesha wananchi. Swali langu ni kwamba, je Mashirika haya yana mkakati gani wa kujenga nyumba za bei nafuu zaidi ambazo wananchi wengi hasa watumishi wa umma wa kipato cha chini wataweza kumudu kununua? Ujenzi wa nyumba za milioni 40 bado hii ni gharama kubwa sana kwa Watanzania ambao bado ni maskini hasa wale wanaoishi vijijini na wafanyakazi wenye kipato cha chini hasa wanawake ambao ndio walezi wa familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Mabaraza ya ardhi na Nyumba ya Wilaya bado hayapo kwenye wilaya nyingi. Kwa hiyo, wananchi wengi wanakosa haki zao kutokana na mabaraza haya kutokuwepo. Pia utengenezwe utaratibu wa kuendesha kesi ambao ni rahisi kwa wananchi kuweza kuandika maandiko juu ya matatizo hayo. Nauliza, Serikali ina mpango gani kuhakikisha mabaraza haya yanakuwepo katika kila Halmashauri/Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, Kodi ya majengo kwa sasa inakusanywa na TRA, Serikali iweke utaratibu mzuri wa TRA kuwafikia wananchi au kushuka kwa wananchi ili kukusanya kodi hizi na aidha, Serikali ifanye tathmini kwa kiasi gani imeweza kukusanya mapato yanayotokana na kodi ya majengo ili kuona kama kuna mafanikio mara baada ya kazi hii kukabidhiwa TRA badala ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nane ni kuhusu mashine za kufyatua matofali. Pamoja na shukrani nyingi kwa Shirika la Nyumba la Taifa chini ya Mkurugenzi Ndugu Mchechu, kutoa mikopo ya mashine za kufyatua matofali kwa vikundi vya vijana katika Halmashauri. Je, Shirika la Nyumba la Taifa limejipangaje kwa mwaka 2017/2018 kuhakikisha kuwa mikopo ya mashine za kufyatua matofali inatolewa kwa vikundi vya akinamama ili kuweza kujipatia kipato na kujenga nyumba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.