Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Uongozi mzima wa Wizara. Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo Wizara hii ni miongoni mwa Wizara chache sana zinazochapa kazi hasa chini ya uongozi wa Mheshimiwa William Lukuvi, pamoja na Naibu Waziri, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie hotuba hii katika maeneo yafuatayo:-

Migogoro ya Ardhi, kila kona ya nchi utasikia migogoro hii. Nipongeze tena jitihada zinazofanywa na Wizara katika kutatua migogoro mfano ni upimaji wa maeneo ya wafugaji na wakulima katika Mkoa wa Morogoro. Bila shaka mfano huu utakwenda maeneo yote nchini mfano katika Jimbo langu la Kilindi lenye nusu wakulima na nusu wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mfumo huu pia uelekezwe huku kwa sababu migogoro inaongezeka kila siku. Suluhu ni kupima tu. Wizara imeelekeza Halmashauri zitenge fedha kwa ajili ya kupima, lakini ni ukweli usiofichika bado Halmashauri zetu hazina uwezo wa kupima kwani baadhi ya Wilaya zina maeneo makubwa sana mfano wilaya yangu ina vijiji 102, vitongoji 650, hivi itachukua miaka mingapi kupima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Migogoro ya Ardhi, (mpaka kati ya Kilindi na Kiteto). Mimi binafsi nichukue fursa hii nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu; Waziri wa Ardhi; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ambao walifika mpakani na kujionea mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 30 ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza Wizara kupitia wapimaji kupitia GN 65 ya mwaka 1961 inayotenganisha Mkoa wa Tanga na Arusha kwa sasa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada zake wapimaji walifika na kufanya kazi kubwa ya kubainisha mpaka huu, gharama za fedha za umma zimetumika kwa watumishi hawa lakini cha kusikitisha ni kuona zoezi hili limesimama alama (Beacons) hazijawekwa, wananchi wanataka wapate majibu ya Wizara hii, tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekwishatambua wapi mpaka wao upo kwa mujibu wa taarifa ya wapimaji ambapo, mimi, Mkuu wa Wilaya na Mkoa wa Tanga tunazo, nadhani zoezi hili ni vema lingekamilishwa ili wananchi wa wilaya hizi mbili, (Kiteto na Kilindi) ambao wanaishi kwa hali ya wasiwasi na kutofanya shughuli za kilimo na mifugo wanachoomba kupata suluhu ya kudumu ambayo ni kuweka alama za kudumu (Beacons).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kauli ya Wizara juu ya jambo hili ambalo linabeba mustakabali wa maisha ya wananchi wa Kilindi na Kiteto, kutowaona wapimaji kumalizia zoezi hili kunatoa picha isiyoleta matumaini. Wananchi wana imani kubwa na Mheshimiwa Waziri kwani utendaji wake bila shaka umemletea sifa kila kona ya nchi hii, ni imani yangu hatapata kigugumizi katika hili ili kuleta haki kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.