Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nimshukuru sana mzalendo namba moja nchini ambaye ni Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya kazi nzuri sana siku tatu zilizopita za kusimamia rasilimali za nchi yetu hii Tanzania. Niliwahi kusema hapa kwamba, Dkt. John Pombe Magufuli ni mzalendo namba moja, na uzalendo wake tunauona hapa kwa namna ambavyo anawatetea watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pongezi kwa Waheshimiwa Mawaziri wote wa Wizara hii, kwanza kwa Mheshimiwa Lukuvi, Naibu wake pamoja na Wasaidizi wao wote, kwa kweli Wizara hii ni ngumu lakini Mheshimiwa Lukuvi amefanya kazi nzuri sana kwa kipindi kifupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia umaskini uliopo katika Jimbo langu la Rufiji. Jimbo la Rufiji lina square kilometer 13,600 na eneo la Bonde la Mto Rufiji ambalo linafaa kwa ajili ya kilimo ni zaidi ya hekta 500,000. Kutokana na utapeli wa madalali na kutokana na wawekezaji matapeli ambao wameingia Rufiji, leo hii ukifika TIC hauwezi kupata eneo la uwekezaji Rufiji. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kuliangalia hili na kuangalia uwezekano wa kunyanganya maeneo yote ambayo wawekezaji matapeli wamechukua ardhi yetu ya Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaskini tulionao ni kwa sababu matapeli hawa wamehodhi maeneo haya na hawayafanyii shughuli yooyote. Leo hii Rufiji tusingekuwa maskini kwa sababu ardhi ndio utajiri wa hali ya juu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri sasa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali yetu ya Awamu ya Tano iweze kupambana na matapeli hawa. Yako maeneo yaliyochukuliwa na watu wa RUBADA, pia yako maeneo yaliyochukuliwa na watu wanaojifanya ni wawekezaji lakini siyo wawekezaji wa kweli. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri maeneo hayo uyarudishe ili sasa wale wawekezaji wanavyopita TIC waweze kuelekezwa na kufika Rufiji wapatiwe maeneo ya uwekezaji. Kwa sababu, maeneo tuliyonayo ni ya kutosha, ardhi ipo tupu, wananchi wanashindwa kushiriki kwenye shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namwomba Mheshimiwa Waziri, kama sio yeye au Waziri anayehusika, atakapofika hapa atupe taarifa ni kwa nini mwaka 2006 Serikali iliamua kuhamisha mifugo kutoka Bonde la Ihefu na kuleta mifugo katika Bonde la Mto Rufiji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tufahamu sababu ya kuhamisha mifugo Bonde la Ihefu. Tunafahamu kabisa kwamba uhamishwaji wa mifugo kutoka Bonde la Ihefu kupelekwa maeneo mbalimbali ya nchi ulitokana na uharibifu mkubwa wa Bonde la Ihefu. Sasa nataka nifahamu, je, Serikali ilidhamiria kuleta mifugo katika Bonde la Rufiji ili sasa na bonde hili liweze kuharibika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu hayo Mheshimiwa Waziri; kama sio yeye au Waziri yeyote anayehusika atakapofika hapa atupatie majibu haya, ili Warufiji waweze kufahamu kiini cha matatizo haya, kwa sababu wakulima leo hii wanashindwa kushiriki katika shughuli za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba Warufiji walikuwa na ndoto za kupatiwa kiwanda katika eneo la Muhoro pamoja na Chumbi. Mheshimiwa Waziri atakapofika hapa, naomba atuambie, je, ardhi ile ambayo ilitengwa kwa ajili ya mwekezaji, bado ipo? Je, mwekezaji huyu anaifanyia utaratibu gani ili sasa tuweze kupata majibu ya jambo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 3 Machi, 2017, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alifika Rufiji na katika maeneo aliyofika, alifika Ikwiriri na katika kauli alizowahi kuzitoa Mheshimiwa Rais aliwaambia Watanzania wa Rufiji, hususan Wenyeviti wa Vijiji kutouza maeneo yao. Aliwaambia wawe makini sana na madalali na matapeli wanaotaka kuchukua ardhi yetu pale Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 9 Septemba, 2016 Waziri Mkuu pia alifika Rufiji, lakini pia katika maeneo ambayo yana mgogoro mkubwa wa ardhi ni eneo letu la Kata ya Chumbi. Tarehe 4 Mei, 2017 Waziri wa Ardhi aliniandikia barua ya kutatua mgogoro wa ardhi pale Chumbi. Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Waziri hakuweza kufika Chumbi, lakini wananchi wa Kata ya Chumbi wanaamini labda mimi ndio nimemzuia Mheshimiwa Waziri kufika Kata ya Chumbi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa, atoe majibu, ni kwa nini hakufika katika Kata ya Chumbi ambako kuna mgogoro mkubwa wa ardhi? Miongoni mwa malalamiko ya wananchi ni kwamba, Mwenyekiti wa Kijiji ameuza ardhi ambayo ina ukubwa wa takriban zaidi ya ekari 2,400 kwa Sh. 9,700/= kwa ekari moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Mheshimiwa Rais alishatoa tamko la Wenyeviti wa Vijiji kutouza maeneo yao, naomba Mheshimiwa Waziri akifanya majumuisho, basi atupe majibu ya jambo hili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.