Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo. Na mimi naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wao, lakini salamu za kipekee kwa Mheshimiwa Waziri, amefanya kazi kubwa sana katika Mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Mvomero. Mheshimiwa Waziri kazi uliyofanya Morogoro ni ya historia, migogoro ya ardhi imepungua, migogoro ya wakulima na wafugaji inaendelea kupungua. Tunaomba jicho lako la huruma liendelee kutusaidia wananchi wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nielekeze matatizo yafuatayo kwa sababu muda wenyewe ni mdogo. Mheshimiwa Waziri, suala la kwanza tuna mgogoro wa mipaka ya kiutawala kati ya Manispaa ya Morogoro na Wilaya ya Mvomero, huu mgogoro ni mkubwa sana, naomba sana utusaidie. Halmashauri ya Mvomero imeanzishwa kwa GN yake, Manispaa ina GN yake, lakini tunaomba sasa hivi Mheshimiwa Waziri, Ofisi yako, wataalam wako waje watoe tafsiri ya GN. Mgogoro unazidi kuendelea, mipaka inaingiliana na wananchi wa Mvomero wanakosa haki kwasabbau Manispaa wanaingilia eneo la Mvomero na wanaanza kugawa ardhi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kauli ya Serikali katika suala hili na tunaomba sana uje utusaidie Mkuu wa wilaya, wataalam wa Mvomero na wananchi pia tumeanza zoezi hili lakini halina mafanikio kwa sababu tunahitaji nguvu kubwa ya Serikali.

Mheshimiwa Waziri, jambo la pili ambalo ningependa sana kulizungumza kwa sababu ya muda nao unakwenda ni kuhusu ardhi kubwa. Mvomero kuna ardhi ambazo hazijaendelezwa, kuna ardhi inaitwa Katenda Group hawa wana heka 12,500 tangu mwaka 2002 mpaka leo ardhi haijaendelezwa. Mheshimiwa Waziri tunaomba ofisi yako sasa itusaidie kutupatia ardhi hii ili wananchi wa Mvomero na Watanzania wengine waweze kufaidika na ardhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu Mheshimiwa Waziri ni upungufu wa wataalam. Mvomero tuna upungufu mkubwa wa wataalam. Nimpongeze Mheshimiwa Rais amevunja CDA, wataalam wa CDA nawakaribisha Mvomero. Tusaidiane wataalam waje Mvomero, tunahitaji baadhi ya wataalam katika maeneo yafuatayo. Tunahitaji Maafisa wa Mipango Miji wawili waaminifu, huo ndiyo upungufu wetu wa kwanza, wa pili tunahitaji Mthamini, na Mrasimu wa Ramani. Tunaomba Mheshimiwa Waziri kwa kuwa haya mambo mengine nitakuwa nayo kwa maandishi nitakuletea, tunaomba tupate watumishi hawa ili Mvomero sasa isonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni kutopata gawio la asilimia 30. Mvomero tunadai zaidi ya shilingi milioni 178, gawio hili hatujalipata bado. Mheshimiwa Waziri, kuna ahadi za Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa William Lukuvi alizozitoa Mvomero. Naomba kuzitaja ahadi zake, ahadi ya kwanza aliahidi kutuletea vifaa vya upimaji (RTK) vifaa hadi leo Mvomero hatujavipata. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaomba utusaidie ahadi yako, tekeleza, tuletee vifaa vya upimaji. Ahadi ya pili tunaomba kukamilisha uandaaji wa mipango na matumizi ya ardhi kwa vijiji 52 kati ya vijiji 130. Ahadi ya tatu Mheshimiwa Waziri tunaomba ukamilishaji wa upimaji wa mipaka ya kiutawala vijiji 32 kati ya vijiji 130. Mheshimiwa Waziri tunaomba sana utusaidie vifaa vya upimaji ili Mvomero tusonge mbele zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mvomero hatuna ofisi ya ardhi, tunatumia ofisi ya Idara ya maji. Sasa umetoa ofisi tatu na unaendelea na mipango mizuri kwa maeneo mengine Mvomero umeisahau, tunaomba kwenye mipango yako mizuri uweze kutusaidia ili na sisi tuwe na ofisi ya ardhi. Mwisho ni kuhusu Ofisi ya Kanda ya Mashariki ambayo baada ya kutoa tamko rasmi sasa kwamba Kanda ya Morogoro inaondoka na badala yake tunahamia huku Dodoma. Mheshimiwa Waziri kwanza nikupongeze ulianzisha Kanda mwaka 2015, ukajenga ofisi nzuri Morogoro, ofisi imefanya kazi nzuri wananchi wa Mikoa ya Pwani na Morogoro wamepata Hati zaidi ya 5,000; sasa kuondoa Kanda leo na kuturudisha tena Dodoma kwa kweli naona unaturudisha nyuma.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri masuala yangu mengine nikuletee kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.