Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo kwa hakika naona hata hii siku moja mliyotupa haitoshi kabisa, ingefaa kila mtu hapa akapata muda wa kuchangia kwa sababu ni fupi na inaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye ukurasa ule wa 47 unaozungumzia huduma za kibenki, naanzia pale kwenye ukurasa wa 44 na nitakwenda moja kwa moja kwenye mikopo. Kuna riba inayotozwa kwa anayekopa lakini kuna riba anayopewa yule anayeweka. Wanakwenda kuwekeza kwenye savings au kwenye FDR na hizo hela zinakopeshwa sasa ile riba imetofautiana sana, anaekopeshwa analipa asilimia 17, huyu ambaye ameweka analipwa asilimia mbili mpaka tatu ndiyo inafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kuna haja gani mtu apeleke hela yake benki akaweke kama analipwa kidogo hivyo? Mbaya zaidi kuna yale makato ya service charges. Ukienda kwa mwaka kama mtu ameweka laki moja yake na hakuweza kuongezea unakuta yote imekatwa kwenye service na hakuna kitu anachopata, maana yake ni nini? Namuomba Waziri wetu aangalie jambo hili, akae na hizo benki husika ili waweze kuona tatizo hili kwamba limekuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile mikopo kuna ile mikopo ya wafanyabiashara na kuna mikopo ya wafanyakazi. Hii mikopo ya wafanyakazi haina matatizo kufuatilia, yeye anafanya kazi pale au hata kama ni Mbunge upo hapa mkopo wako utalipika tu na hata nikiondoka leo bado yale mapato yangu yatalipa ule mkopo. Kwa nini tunatozwa kiwango kinacholingana na wale wafanyabiashara? Mfanyakazi anatakiwa atozwe kidogo zaidi na isipishane zaidi na ile ya kuwekeza, ningeomba kufahamu jambo hili siyo haki kabisa. Mikopo hiyo ina bima, ufuatiliaji ni mdogo kwa kweli naona wakati sasa ufike, Waziri akae mezani na haya mabenki waone ni jinsi gani wanarekebisha jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo la mabenki, niende katika ukurasa wa 17 ule utaratibu au mikakati ya kupunguza umaskini. Napongeza hatua ya Wizara hii kutoa mafunzo kwa wataalam, lakini katika kutoa mafunzo kwa wataalam sikuona Wizara imejipanga kutoa mafunzo kwa wale ambao ndiyo wanaonufaika na elimu hii inakuaje? Mnatuelimishia wataalam, lakini hamkupanga fungu la kuelimisha wale ambao ni wanufaika, sioni kama hapo tutapiga hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri sasa aangalie wataalam hao wakishaelimika pia aweke fungu ambalo wataelimishwa wajasiriamali wadogo wadogo, wale wa VICOBA, watu wote ambao wanataka kuingia kwenye biashara ili waweze kunufaika na hii elimu ambayo wamepatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 34 naomba nizungumzie kidogo kuhusu ukaguzi wa hesabu za Serikali. CAG anakwenda kwenye ukaguzi lakini tumeona kabisa na tumeelezwa hela ya kumuwezesha CAG ni kidogo japo kwa kipindi kilichotajwa ameweza kupatiwa, lakini tunaomba CAG afikiriwe, tumemuombea bajeti iliyopita na sasa tena tunamuombea kwa sababu tulienda tukaona kuwa hakuweza kutembelea maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 35, kuhusu usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma. Naona hapa wameeleza vizuri usimamizi unavyokuwa lakini nauliza kwamba, Serikali ilikuwa na hisa kwenye mashirika mengi tu lakini hatukuorodheshewa hadi sasa imekidhi asilimia ngapi kwenye mashirika kadhaa na ufuatiliaji wake ukoje. Mashirika mengi yalikuwa mikononi mwa Serikali, mengine sasa yamekwenda private, mengine hayapo tena kabisa na Serikali. Je, Serikali imefuatilia hisa zake kwa yale mashirika yote? Hapa tunapata wasiwasi. Mimi nipo kwenye Kamati ya PAC na tuliona kwamba kuna maeneo ambayo Serikali imesahau hata hisa zake. Nilikuwa naomba sana Wizara ifuatilie ili iweze kujua imewekeza wapi na inalipwa kwa jinsi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika currency yetu, hela yetu hizi noti. Coins hazina tatizo japo zote zinaitwa noti nacoins, naomba Wizara izungumze na Benki Kuu itoe elimu ya kufanya utunzaji wa noti.Kamati yangu ilipata nafasi ya kwenda kutembelea Benki Kuu tukaona jinsi ambavyonoti hizo sasa inafikia mahali wana-thread, wanaondoa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni gharama sana ku-thread ni bora tungekuwa na notiambayo ingeweza kudumu, amezungumza mzungumzaji mmoja kabla yangu lakini mimi nataka niende mbali zaidi. Utunzaji wa notie unatakiwa uwe kwenye akili ya mtu it is a mindset.Mtu anaichukua noti yake vizuri, anaweka kwenye wallet, lakini Watanzania wengi anachukuanoti yake anafunga kwenye kitambaa, anasokomeza anakosokomeza. Hiyo noti hata ingekuwa ya gharama namna gani lazima itachakaa. Naomba Serikali ione umuhimu wa kuelimisha watoto toka wakiwa wadogo namna ya kutunza hela, namna ya kuthamini noti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nchi za nje unakuta dola siku zote imenyooshwa wanashangaa wakija Tanzania dola inakunjwa, wakija Tanzania pound inakunjwa, hela haikunjwi ndugu zangu, ukitunza hela inakutembelea. Weka notiyako kwenye wallet, hela ipendeze na hiyo hela itadumu na mfukoni itaenea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie umuhimu wa kuona kwamba imefikia wakati yeyote anayetaka kujaribu biashara kabla hajaingia kwenye biashara aingie katika elimu au ataelimishwa na wale wanaomhusu au atakwenda kupata mafunzo. Tuna vyuo vyetu vingi tu kimojawapo ninachokifahamu kwa undani sana ni Chuo cha Ushirika (Moshi Cooperative University).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna wakati wanafunga shule, wakifunga chuo nilikuwa naomba Waziri akiweza kutukutanisha akatupa semina kama Wabunge wake na tukianza kwenda kukutana na wale tunaowasimamia wapate elimu katika vyuo hivyo na sisi wenyewe pia tutachangia gharama za kuelimisha watu hawa. Tukielimika kutakuwa hamna tatizo, tutakuwa na Waziri wetu mzuri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri mzuri na wote tutazungumzia maendeleo, sioni kwamba saa zote tukikaa tulaumu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusanyo yanatosha kutuambia tupongeze, naomba nichukue nafasi hii kupongeza sana Wizara hii kwa makusanyo yaliyopatikana na pia nipongeze Wizara hii kwa jinsi ambavyo imejitahidi kulipa deni la Serikali, hatuwezi kudaiwa kila siku, dawa ya deni ni kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja asilimia mia moja.