Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nitazungumzia suala zima la gesi na baadaye nitajielekeza kwenye suala la umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu katika taifa letu wananchi wa Tanzania wemekuwa na matumaini makubwa sana kuhusiana na suala la gesi ya Mtwara. Matumaini haya yametokana na sababu nyingi mbalimbali ikiwa ni pamoja na sababu ya miradi miwili mikubwa. Mradi namba moja ni mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ambalo limechukua takriban shilingi trilioni 2.5 katika utekelezaji wake na mradi wa pili ni mradi wa LNG (Liquefied Natural Gase) ambayo kama ingekuwa imetekelezeka kwa sasa ingekuwa imetumia Dola za Kimarekani bilioni 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sana Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikitumia akili ndogo sana kupanga mipango na kutekeleza miradi mikubwa na mambo makubwa. Bomba la gesi la Mtwara kwenda Dar es Salaam limetumia pesa nyingi sana, lakini kwenye ripoti ya CAG anaonesha bomba hili la gesi lina uwezo wa kufanya kazi kwa asilimia sita tu. Tafsiri yake ni kwamba hata hilo deni ambalo tumelikopa China la trilioni 2.5 hatuwezi kulilipa kwa sababu bomba hili halifanyi kazi vizuri; matokeo yake tutaanza kuchukua fedha kutoka kwenye madawa; tutaanza kuwabana wafanyabiashara kwa ajili ya kulipa deni hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo lingine ambalo ni kubwa sana. Naomba Mheshimiwa Waziri husika atakapokuja kuhitimisha atoe majibu ni ni kwa nini wanakuwa wana poor project plan ambayo inapelekea miradi mikubwa kama hii inashindwa kutekelezeka kwa ufanisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa LNG (Liquefied Natural Gas) haijawahi kutokea katika Taifa hili kuwa na mradi mkubwa kama huu. Huu ni mradi wa kihistoria, lakini cha kushangaza mradi huu umeshindwa kutekelezaka kwa sababu Serikali mmeshindwa ku-deal na investors.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kwenye meza yangu nina taarifa kutoka kwenye jarida kubwa kabisa la kimataifa la Reuters la Uingereza ambalo nimem-quote meneja wa Statoil anaeleza kwamba mradi huu umeshindwa kutekelezeka kwa sababu ya kusuasua kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kama utahitaji taarifa hii naomba umtume mhudumu aje aichukue copy yako nimekutolea. (Makofi,)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aseme tatizo ni nini? Nimesikia kwenye hotuba asubuhi anasema kwamba majadiliano bado yanaendelea. Wawekezaji wanalalamika, tatizo ni nini? Ni hivi, hawa investors ambao anawapiga danadana wamehamisha mradi huu wa LNG wameupeleka Msumbiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kupelekwa Msumbiji tafsiri yake ni kwamba kufikia mwaka 2021 ambapo mradi huu unakwenda kutekelezeka maana yake ni kwamba Msumbiji watateka soko la gesi katika Afrika Mashariki pamoja na Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri labda sijui ni kutofahamu, mimi nashindwa kuelewa! Unapozungumzia uwekezaji wa takriban dola za Kimarekani bilioni 60, bilioni 30 unakuwa unazungumzia uchumi wa Uganda. Uchumi wa Uganda ni takrban dola la Kimarekani bilioni 60. Unapozungumzia investment ya dola za Kimarekani bilioni 30 unazungumzia robo tatu ya uchumi wa Tanzania ambao ni dola za Kimarekani bilioni 45. Unapokuwa unazunguzia uwekezaji wa takriban dola bilioni 30 unakuwa unazungumzia mara kumi ya uchumi wa Rwanda. Uwekezaji huu ni mkubwa sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atupe sababu kwa nini mradi huu unashindwa kutekelezeka kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la umeme. Taifa hili lina vyanzo vingi vya umeme. Tuna maporomoko ya mito, tuna upepo, kwa mfano mimi mkoa wangu wa Singida kuna upepo wa kumwaga. Pia tuna makaa ya mawe ukienda kule Liganga na Mchuchuma takrban tani milioni 480 zimejaa kule, lakini bado umeme ni wa kusuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia mpango wa miaka mitano uliotolewa na Waziri wa mwaka 2016 - 2021 ukurasa wa 12 unaonyesha kwamba mwaka 2011 Serikali ilidhamiria kuongeza megawatt kutoka 900 mpaka 2,700 kufikia mwaka 2011, lakini cha kusikitisha mpaka inafika mwaka 2016 megawatt zilizoongezeka 1,246 na kwa bahati mbaya sana nimemsikia na Mheshimiwa Waziri asubuhi kwenye hotuba yake na nimeipitia kumbe zimeshuka tena mwaka huu zimekuwa Megawatt 1,051.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kama kuna Waziri yeyote hapa asimame aniambie kama kuna nchi yoyote imewahi kufanya mapinduzi ya viwanda kwa megawatt 2,000. Mnampa Mheshimiwa Rais mizuka ya uchumi wa viwanda na wakati mmeshindwa na mnajua haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnapowaita wawekezaji waje kuweze katika taifa letu na wakati umeme uliopo ni wa kukatika…

TAARIFA ....

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, yaani katika taifa letu ikitokea mvua hata ya saa moja tu, umeme unakatika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnapowaita wawekezaji waje kuwekeza na wakati umeme wenu ni wa kukatika na kuwaka, mnataka kuwaharibia mitambo yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Serikali inayojipambanua kwamba ni Serikali ya viwanda kuna mambo ambayo yalipaswa kupewa kipaumbele. Mimi binafsi nimeunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais za kununua ndege pamoja na kujenga reli ya standard gauge, lakini katika Serikali inayojipambanua kwamba yenyewe ni ya viwanda hii haikuwa kipaumbele. Kipaumbele namba moja kilipaswa kuwa ni umeme, kilimo na mambo mengine lakini kukimbilia kufanya mengine ndiyo maana mambo yanakuwa hayaendi. Niwashauri Waheshimiwa Mawaziri wamsaidie Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye skendo (scandal) kubwa sana ambayo nimewahi kuizungumza humu ndani na leo nairudia na nitairudia kwa ufupi tu. Nataka nijue kauli ya mwisho ya Serikali kuhusiana na capital gain tax ambayo haijalipwa kwenye transfer of shares kutoka kampuni ya BG kwenda kanuni ya Shell. Hii nchi si shamba la bibi, hii nchi ina wananchi na hii nchi ni ya wananchi. Nataka kauli ya mwisho kutoka Serikalini, hizi fedha ambazo mpaka dakika hii hazijalipwa. Tatizo ni nini? Akina nani walihusika? Ni nani alivunja sheria hii na amechukuliwa hatua gani? Mheshimiwa Waziri na Naibu wake naomba majibu hapa kesho atakapohitimisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.