Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara muhimu sana, Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kwa dhati ya moyo wangu, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za dhati za kuzuia wizi kwenye rasilimali za nchi yetu na hasa rasilimali katika sekta ya madini. Jambo ambalo tunatakiwa wote tuwe clear ni kwamba hakuna anayepinga au anayekataa uwekezaji. Mheshimiwa Rais hapingi wala hakatai uwekezaji na siku zote Mheshimiwa Rais amekuwa akihimiza wawekezaji wa ndani na wa nje waje kwa wingi kadri iwezekanavyo. Mheshimiwa Rais anachochukia ni wizi wa rasilimali zetu na ambao tukiuacha uendelee utaturudisha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashe asubuhi wakati anatoa taarifa kwa Mheshimiwa Sixtus aligusia kidogo, sisi Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ni wahanga wa kudhulumiwa na haya makampuni ambayo wakati mwingine hayafuati taratibu na sheria zinazotakiwa. Resolute Tanzania Limited wamechimba dhahabu pale Nzega tangu mwaka 1999 na sasa hivi wamesimamisha uchimbaji lakini navyoongea sasa hivi Resolute wameondoka na service levy zaidi ya shilingi bilioni kumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Mara zote tukifuatilia wanatoa visingizio vya kisheria, by-laws lakini kimsingi wanapaswa watulipe fedha hizi. Nina imani kubwa Serikali hii ya Awamu ya Tano itaingilia kati kutusaidia ili Halmashauri ya Wilaya ya Nzega tusiweze kudhulumiwa shilingi bilioni kumi zetu za service levy ambazo kimsingi ni haki yetu tulipaswa tupate kama sehemu ya ushuru wa huduma kutoka kwa Kampuni hii ya Resolute. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kampuni hii imesimamisha uzaliashaji na haina mfanyakazi hata mmoja lakini tunajua ma-directors wapo na tunajua director mmoja ni Mtanzania na wengine wa nje. Tunajua bado wapo wana issue zao zingine za kikodi na mambo mengine wanaendelea ku-sort out lakini kampuni ipo. Kwa hiyo, bado kuna uhalali wa sisi kuendelea kudai na wao kutulipa stahili yetu kama ambavyo inastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kushauri ni kwamba Mheshimiwa Rais ameonesha mfano kwenye eneo la madini lakini naomba jitihada hizo za Mheshimiwa Rais ziende sasa mpaka kwenye rasilimali ya gesi. Bahati nzuri gesi ambayo tumeigundua kwa kiwango kikubwa hatujaanza kuichimba nako huku kuna dalili kwamba tusipokuwa makini pia kuna uwezekano mkubwa wa wawekezaji kwa maeneo haya wakaendelea kutunyonya au kutudanganya na hatimaye tukajikuta kwamba hatupati stahili zetu kama ambavyo tunatakiwa. Kwa hiyo, jitihada hizi ziende hata kwenye eneo la gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie eneo la wachimbaji wadogo. Napongeza jitihada za Wizara, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Kalemani tumekuwa tukiwasiliana lakini na watendaji wake wa madini, Ofisi ya Tabora na ya Kanda nipongeze kwa jitihada ambazo sasa hivi wanazifanya katika kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogowadogo maeneo ya Nzega na yanayozunguka wanapata leseni na shughuli zao zinarasimishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Nzega kuna maeneo mengi tu ambayo leseni zilizokuwa zinamilikiwa na hii Kampuni ya Resolute ambayo imeondoka na kimsingi walisha-surrender leseni zao. Wananchi wengi ambao sasa wameamua kuondokana na umaskini kwa kufanya shughuli hizi za uchimbaji mdogo mdogo wamekuwa wakiomba leseni ili waweze kuchimba kihalali lakini kutokana na mfumo wa kuomba leseni, mfumo bado unaonesha leseni hizi zinamilikiwa na hawa Resolute, kwa hiyo wananchi kila wakiomba mfumo unawakatalia lakini maeneo hayo yako wazi, Resolute walishaondoka hawafanyi chochote. Kwa hiyo, naomba Wizara ifanye utaratibu ili maeneo haya sasa ndani ya mfumo yafunguliwe ili wananchi na vikundi ambavyo vimejihamasisha, vimeji-organize, wameamua kuondokana na umaskini kwa kuanzisha ajira katika shughuli za uchimbaji mdogomdogo mfumo uweze kuwakubaliana kuomba leseni hizi na kuweza kupata hatimaye wafanye shughuli zao kihalali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya yamezunguka eneo lililokuwa la Mgodi wa Resolute lakini hata maeneo ya Mwangoye ambayo yako ndani ya Jimbo la Bukene pia yanakabiliwa na tatizo hili. Nina imani kubwa sana na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kalemani na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Tabora na Kanda, nina uhakika jambo hili liko ndani ya uwezo wao na watalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni bomba la kutoa mafuta Uganda mpaka Tanga. Jimbo langu la Bukene na Wilaya ya Nzega ni moja ya maeneo ambayo yatanufaika na kupitiwa na bomba hili. Juzi Jumatatu nilikuwa Jimboni na kuna Kampuni ya GSB ambayo ndiyo wamepewa kazi ya kufanya tathmini ya mazingira na athari za kijamii, walituita pale ili kutu-sensitize kuhusu bomba hili. Niseme kwamba wananchi wa Jimbo la Bukene na Wilaya ya Nzega wako tayari, wanalisubiri bomba kwa mikono miwili na habari njema tulizopata ni kwamba maeneo yote ambayo bomba litapita kutakuwa na fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ushauri wangu ni kwamba yule mkandarasi mkuu wa bomba ahakikishe kazi zile ndogo ndogo ana-subcontract kwa makampuni ya wazawa ili na wenyewe waweze kufaidi. Pia kazi za vibarua zisizohitaji utaalamu wa juu basi wapewe vibarua ambao wanatoka katika maeneo ya vijiji husika ambapo bomba litapita. Nimeambiwa kwangu pale katika Kata ya Igusule ndipo kutakuwa na kituo kikubwa ambacho kutakuwa na wafanyakazi zaidi ya 1,000. Kwa hiyo, sisi tunalichukulia hili kama ni fursa ya ajira, kupata uzoefu na kuinua hali ya maisha ya wananchi wetu wa Jimbo la Bukene. Kwa hiyo, wananchi wa Igusule, Mwamala, Kasela, Mwangoe na Lusu wako tayari wanalisubiri bomba hili kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu umeme wa REA Awamu ya Tatu. Nichukue fursa kwa dhati kabisa niipongeze Wizara na hasa Naibu Waziri Mheshimiwa Kalemani ambaye alikuja Jimboni kwangu na kuhamasisha umaliziaji wa umeme wa REA Awamu ya Pili. Sasa hivi maeneo yote ambayo umeme umeweza kufanikiwa kumetokea mabadiliko makubwa kabisa kwa hali za maisha na hali za kiuchumi za wananchi. Kwa hiyo, Jimbo langu la Bukene ni mfano wa namna ambavyo nishati ya umeme inaweza kubadilisha maisha ya mahali fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja na nawapongeza sana watendaji wote wa Wizara hii, ahsante.