Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii ambayo ni muhimu sana ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kitendo chake cha kuzuia yale makontena pale bandarini na nampongeza sana kwa kuunda ile Tume ya kuanza kuangalia kiini hasa cha utoroshaji wa madini hapa nchini. Ripoti ya Tume inabidi Waheshimiwa Wabunge tuipongeze sana kwa sababu pale ndiyo mwanzo wa kuanzia, madini ya nchi hii yamekuwa yakitoroshwa kwa muda mrefu sana na kwa kiwango kikubwa.Tumeshuhudia baadhi ya migodi hapa nchini inatengeneza mpaka viwanja vya ndege ndani ya mgodi. Tumeshuhudia baadhi ya migodi hapa nchini inaweka kampuni za ulinzi kutoka nje kwenye migodi ya hapa nchini, maana yake ni nini hiyo? Maana yake ni utoroshaji kwamba wanatayarisha viwanja vya ndege, wanatayarisha ulinzi kutoka nje ili sisi tusiweze kuona na baadaye madini hayo yanaondoka kwa kiwango kikubwa. Sasa hii ripoti inadhihirisha kwamba tumeibiwa muda mrefu sana.

TAARIFA .....

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mimi mwenyewe nimeviona hivyo viwanja na nimeona hizo kampuni kwenye migodi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hapa Waheshimiwa Wabunge lazima tushikamane, hii ni hoja ya Serikali, sasa hizi hoja za kupinga ambazo zinatolewa aidha, madini hayo ni mengi au siyo mengi lakini kuna dalili za utoroshaji jamani, lazima tushikamane. Sasa tunapotoa hoja hapa ooh tutashtakiwa, ngoja twende tukashtakiwe, kwani tunaogopa kwenda International court, tunaogopa kwenda kwenye arbitration, twendeni tukashtakiwe na tutatoa arguments, tuna ushahidi ambao umeonekana na Kamati imedhihirisha. Waheshimiwa Wabunge hiki ni kipindi ambacho tunatakiwa tushikamane kwa sababu tutakapofanikiwa kudhibiti madini yetu maendeleo yatakuwa kwa kasi sana, kwa hiyo, nawaomba tushikamane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii sijaona Mheshimiwa Waziri akizungumzia suala la ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Madini. Namuomba aipangue bajeti yake na ahakikishe kwamba anaweka huo msimamo wa kuweka hela za Kiwanda cha Kusafisha Madini. Wakati masuala haya yanaendelea kushughulikiwa ngoja tuanze mchakato wa kujenga kiwanda chetu hapa kama tukishindwa basi tuingie ubia na watu binafsi kwa maslahi yetu lakini lazima tuhakikishe kwamba kiwanda hicho tuna ki-manage sisi tusije kufanya makosa tena na kuibiwa. Namshangaa ndugu yangu Mheshimiwa Lissu juzi wakati anaongea alipokuwa ana-criticize ya kuongelea case ya Bulyanhulu, naifahamu case hiyo nimeishughulikia na wakati huo Mheshimiwa Lissu alikuwa anatetea sana wachimbaji wadogo na namna makampuni makubwa ambavyo yanataka kuwadhulumu wachimbaji wadogo mali zao. Jana akawageuka tena anaponda mimi nimeshangaa sana. Kwa hiyo, nasema tushikamane ili tuondoe hili tatizo ili tuweze kupata hela nyingi za kuweza kuleta maendeleo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie REA III, REA wamefanya kazi nzuri sana ila katika kipindi hiki hawakufanya kazi nzuri ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Sasa sijui ni kwa sababu gani lakini mipango ambayo wameiweka kwenye REA III tunategemea waanze kutekeleza vizuri. Pale Muheza kwenye Jimbo langu Mheshimiwa Waziri unajua umenipa REA III vijiji 44, list ya mkandarasi ambayo umenikabidhi ina vijiji 37, nakuomba urudishe vile vijiji vyangu saba ili wananchi wa kule ambao wameanza kufunga nyaya waweze kupata umeme. Vijiji hivyo ni vya Kwakope, Kibaoni, Magoda, Mbambala, Kitopeni, Masimbani, Msowelo vyote hivyo wananchi wameshajitayarisha na wako tayari kwa ajili ya kufungiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda kupongeza sana juhudi ambazo zinafanyika kwa ajili ya bomba la mafuta la kutoka kule Hoima Uganda mpaka Tanga. Tunaamini hii ni chachu na wananchi wa Tanga wanategemea sana kwamba bomba hilo litawaletea maendeleo makubwa ya viwanda na vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.