Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kwanza. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika mwezi huu wa Ramadhani tukiwa wazima na kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kabisa kwa kuunga mkono hotuba ambayo imetolewa na Wizara hii ya Nishati na Madini. Kwa kweli Serikali kwa upande wa Wizara hii imejitahidi. Vyovyote tutakavyofanya na kusema hatuna budi kuishukuru Serikali kwa jitihada inazochukua katika suala la sekta hii ya nishati na madini hasa tukizingatia usimamizi imara uliopo katika Awamu hii ya Tano ya Serikali yetu chini ya uongozi makini kabisa wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia sina budi kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa namna ambavyo amepokea wito wa uungwana kabisa na busara kulipokea deni ambalo ZECO inadaiwa na TANESCO na kuahidi kulilipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile dawa ya deni ni kulipa, Mheshimiwa Rais amechukua hekima na busara kuweza kukubali na mpaka hivi sasa deni la shilingi bilioni 11.8 limeshalipwa ambapo shilingi bilioni 10 zimelipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na shilingi bilioni 1.8 zimelipwa kupitia ZECO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hatuna budi kuipongeza Serikali kupitia TANESCO, tusipoipongeza tutakuwa hatuna shukrani. Pamoja na upungufu yote ambayo TANESCO inayo lakini kazi inayofanywa lazima tuishukuru na kuithamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwenye kitabu humu miradi mbalimbali imeshatekelezwa ikiwemo Kinyerezi I na II ambazo zinaendelea lakini pia tuna REA, usambazaji wa umeme vijijini, kazi inafanywa kubwa kwa mazingira magumu. Tukipita sisi wengine tunaona juu ya milima kuna nguzo huko, tunashangaa zimetandazwaje, chini ya mabonde huko tunakuta nguzo tunashangaa zimetandazwaje, lazima tuwe wenye kushukuru na lazima tuwapongeze. Naamini kwamba Serikali kupitia TANESCO itatatua changamoto hatua kwa hatua ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utaelekea huko huko kwenye nishati ya umeme na hapa nitazungumzia mfumo uliopo baina ya Shirika la TANESCO na ZECO. Niseme wazi kwamba kutokana na mfumo uliokuwepo siku za nyuma na pengine huu uliopo sasa hivi, ndiyo umepelekea ZECO kuwa na deni kubwa kwa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielezee yale ambayo yamepeleka mfumo huu kuonekana kama unaendelea kuipa deni ZECO. Kwanza ni tozo ya KVA. Hii nikizungumza wataalam wanaelewa, ni tozo ya watumiaji wakubwa wa umeme kwa mfano viwanda na kadhalika. ZECO tunachukua kilovoti 132 kwa bei ya shilingi 16,550 lakini watumiaji hawa wa kilovoti 33 ambao wanachukua kwa Tanzania Bara wanatozwa shilingi 13,200 kwa kilovott moja. Kwa hiyo, utaona difference iliyopo ya mfumo katika uendeshaji na kuipelekea ZECO kuweza kulimbikiza deni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wawekezaji ambao wana tamaa ya kuwekeza Zanzibar wanashindwa kuwekeza kwa ajili ya tozo hii, hivyo naomba sana Serikali ilizingatie. Kwa mfano, mwaka 2011 utaona pia mtiririko wa mabadiliko ya tozo unavyobadilika, naweza kutoa mfano mwaka 2011 ZECO iliongezewa tozo ya asilimia 81.1 wakati Tanzania Bara iliongezwa tozo ya asilimia 19.4 tu, ni difference kubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali izingatie sana kupitia Shirika hili la Umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoa mfano pia mwaka 2013 TANESCO na ZECO walikubaliana kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwamba sasa umefika wakati hizi kilowatts per hour Zanzibar ipunguziwe kwa asilimia 31. Matokeo yake, TANESCO iliendelea kuingiza hiyo asilimia 31 hatimaye deni hili likatajwa mwisho wake kuwa ni shilingi bilioni 121.9 ambayo round figure ni shilingi bilioni 122 wakati ZECO wanaendelea kuhesabu kwamba wameshatolewa punguzo la asilimia 31 na kulikubali deni hilo kuwa ni shilingi bilioni 65.5. Kwa hiyo, tunaweza kuona difference hizo na naomba sana Mheshimiwa Waziri husika na timu yake waweze kuangalia kwa upande huu wa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la ZECO kuwa end user, nikizungumza end user anakuwa kama mtumiaji wa kawaida wa Tanzania Bara. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu mtumiaji wa kawaida wa Tanzania Bara anapelekewa umeme kupitia miundombinu ya TANESCO lakini ZECO tunaletewa umeme kwa bei ambayo mtumiaji wa Tanzania Bara anapewa with operational costs za ZECO, miundombinu na gharama zote ni za ZECO. Kwa hiyo, tuangalie hali inavyokwenda tuone mfumo uko vipi, nia yangu ni kueleza mfumo huu tuweze kuusahihisha ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hili tunasema kwamba ZECO na TANESCO ni mashirika ya Serikali, moja kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano na lingine kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. ZECO yenyewe inakuwa na madeni ambayo inadai Taasisi za Serikali ikiwemo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Hussein Mwinyi, Wizara yake imeweza kupunguza shilingi milioni 400 deni ambalo tulikuwa tunawadai na sisi ndiyo tumeweza kurudisha TANESCO. Kwa hiyo, tuangalie haya mambo ili sisi tuweze kulipa deni na Serikali taasisi zake iweze kulipa. (Makofi)

Kwa hiyo, hilo ni moja ambalo nilipenda nizungumzie kwa upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna huduma nyingine za jamii ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja. Kwa mfano, ZAWA ambayo inashughulika na masuala ya kusambaza maji Zanzibar, tunaidai zaidi ya shilingi bilioni 20. Tunashindwa kuwafungia umeme kwa sababu Watanzania wanaoishi Zanzibar watakosa maji. Kwa hiyo, inabidi shirika hili tuone mfumo gani ambao utaweza kuwa bora na mzuri ili tusije tukaingia kwenye migogoro ambayo mimi sipendi kuiita kero, nasema bado ni challenge, tuzirekebishe hizi challenge ili Watanzania wote wanaoishi Tanzania Bara na wale walioko Zanzibar ambao wote ni wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania waweze kunufaika na huduma hii bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili Shirika la ZECO linafanya kazi kubwa kuikusanyia mapato TANESCO. Mbali na hayo madeni ambayo yametokana na hizo sababu nilizozitaja, tunatumia umeme kuanzia shilingi milioni 400 hadi shilingi milioni 500 kwa mwezi na bahati nzuri kuanzia mwaka 2015 Desemba tunalipa current bill kwa maana kwamba ankara kamili ya kila mwezi. Kwa hiyo, ili kuweka sawa mambo haya, tuonekane na sisi ZECO kule kwamba tunaifanyia biashara TANESCO ambayo ni taasisi ya Jamhuri yetu ya Muungano Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mwingine, tumeweza kuikusanyia shilingi bilioni 41.8 katika kipindi cha miezi tisa kuanzia 2016 hadi kufikia Machi, 2017. Kwa hiyo, sasa nachoshauri mbali na kuwekwa huyu Mtaalam Mwelekezi nitaomba ushauri wake ufuatwe ili twende sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni kwamba sisi ZECO basi angalau tupewe fursa ya kuwa agent wa TANESCO ili tuweze kulipwa na kuweza kugharamia operation cost ili tusiweze kuleta migogoro katika Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, pamoja na kuunga mkono hotuba hii naomba sana ushauri huu uweze kuzingatiwa ili tuweze kuimarisha Muungano wetu. Ahsanteni sana.