Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Nashukuru Mheshimiwa Spika, kwanza naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika bajeti hii na nitajikita kwenye masuala makuu mawili ambayo ni kilimo na mambo ya mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nimeamua kugusia kilimo kwa sababu nchi yetu bado ipo kwenye category ya kimaskini na karibu asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo na katika hao asilimia 70, asilimia 80 ni wanawake. Sasa kwa nini nimeamua kuchagua kilimo kwa sababu naona kwenye kitabu cha mpango cha Mheshimiwa Waziri 2016/2017 malengo hayakugusa kilimo wala hayakugusa mazingira. Katika kilimo aligusia tu shamba la miwa na kiwanda cha sukari ambacho kitaanzishwa huko Mkulazi, kitabu hicho hicho baadaye 2017/2018 hajagusia tena kilimo, lakini amegusia tena shamba hili hili la Mkulazi, mazingira pia haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inashangaza kwamba hatuwezi kutoka kwenye huu umaskini katika nchi yetu, wenzetu mfano nchi ya Mexico ilikuwa maskini tena hata kuliko sisi nafikiri. Hata hivyo, mwaka 1940 waliamua kujikita kwenye kilimo na walichagua zao moja tu la ngano, sasa hivi Mexico ni nchi ya 13 duniani kwa utajiri na ni nchi ya 11 duniani yenye uwezo ya kununua bidhaa. Sasa sisi tunaimba tu tunagusa mambo mengi, mipango mingi ambayo haina focus na focus yenyewe ambayo tunayo tumesema sisi kilimo ndio uti wa mgongo lakini hatukipi priority.

Mheshimiwa Spika, sasa ni lini Mheshimiwa Waziri ataamua sasa tutoke hapa tulipo akaacha legacy katika nchi hii kwa kipindi hiki alichonacho, akajikita katika kilimo kukitengeneza kilimo? Kilimo sio tu kimekuwa hakitukomboi Watanzania, bali pia kimekuwa kikishuka. Kilimo kimeshuka kutoka asilimia 2.3 mwaka 2015 mpaka asilimia 0.3 mwaka 2016. Sekta ya Kilimo ambayo tegemeo kwetu na ambayo inaweza kututoa kwenye hali tuliyonayo, sekta ya kilimo ilitengewa bilioni 101 hadi sasa zilipelekwa bilioni 3.3 tu sawasawa na asilimia 3.31.

Mheshimiwa Spika, mifugo na Uvuvi vilitengewa bilioni 15.8 hadi sasa zilitolewa bilioni 1.2 tu sawa na asilimia nane, sasa tunavukaje hapa? Fedha za maendeleo katika sekta hii ya kilimo ambayo ni kilimo, mifugo na uvuvi na shughuli zote zinazohusiana na uvunaji na kilimo, zilitolewa chini ya asilimia 97 katika Wizara hii. Sasa tutaongea sana, tutapanga sana lakini hatuwezi kutoka hapa tulipo kwa kutokuwekea kilimo kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 nchi yetu ilianzisha Benki ya Kilimo ambayo ilitarajiwa kupewa trilioni moja, lakini Benki hii mpaka sasa imepewa bilioni 60 tu. Benki hii ili-target kuwapa mikopo wakulima 200,000 kila mwaka, lakini mpaka sasa ni wakulima 3,700 tu wameweza kupata mkopo. Kwa hali hii hatuwezi kuvuka hapa tulipo, umaskini bado utaendelea kuwa pamoja nasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa nane wa kitabu cha Mpango kimesema kwamba baadhi ya shughuli za kiuchumi zilishindwa kufikia maoteo ya viwango vya ukuaji ikiwemo sekta ya kilimo ambayo ni dhahiri sasa tunajua kwa sababu gani ambayo iliweza kukua kwa asilimia 2.1 tu. Shirika la Chakula Duniani (FAO) 2014 ilisisitiza tena kwa nchi maskini za Afrika tujikite katika kilimo, kilimo ndio kinachoweza kutuletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, jopo hili la wataalam limesema kwamba tuendelee kushikilia Maputo Declaration ambayo tuli-commit Watanzania kutenga ten percent ya bajeti yetu kwenye shughuli za kilimo na kuhakikisha pia kwamba kilimo hiki angalau kinakuwa kwa six percent kwa mwaka, sisi tupo chini ya hapo, tunaongelea two point, one point, hatuwezi kuvuka. Naomba bajeti iangaliwe upya iweze kujikita katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mifano iko mingi ya nchi ambazo ziliweza kuendelea, hata Wakoloni wetu Waingereza miaka ya 1800 walikuwa na agricultural revolution ndio wakafika hapo sasa hivi, sasa kwa nini sisi hatuamki wakati tuna mifano na tukijua kwamba population yetu asilimia kubwa ni hawa wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali pia katika ukurasa wa saba wa kitabu cha Mpango namba 12 imekiri kuwa mfumko wa bei ulikuwa pia umechangiwa na ukame au kuchelewa kwa msimu wa mvua. Wabunge wengi ni Wabunge wa maeneo ya vijijini ambao wanashughulika na kilimo na Wabunge wengi tumeona njaa mwaka huu na bado wananchi wetu wanalia kwa njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasisitiza kwamba Serikali sasa inabidi iwekeze pia kwenye sekta ya maji, kwenye irrigation hatuwezi kuvuka kwenye kilimo cha sasa hivi cha kutumia jembe na kutegemea mvua tukasema kwamba tutaweza kupata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nilipatwa na kigugumizi, nimepatwa na bumbuwazi kuona kwamba issue ya road license malipo yake yamepelekwa kwenye lita ya mafuta. Wiki kadhaa zilizopita humu Wabunge karibu asilimia kubwa waliosimama kwenye sekta ya maji, walikuwa wanapendekeza Sh.50/= kwenye kila lita ya mafuta kwa ajili ya Mfuko wa Maji, sasa road license mnajaribu kumbeba nani katika hili, inamsaidia nani? Ile tozo ya shilingi 40 kwa kila lita inakwenda kujenga barabara, barabara inamsaidiaje Mtanzania ambaye anakufa na njaa?

Mheshimiwa Spika, kwa nini hiyo hela wasitafute means nyingine za kuwasaidia hao wenye kudaiwa hiyo road license au malimbikizo yao, badala ya kuwapongeza kwa kuweka kwenye lita ya mafuta. Mheshimiwa Shabiby yeye anakuja na concept yake kwamba inakuwa ina unafuu lakini haina unafuu, inakwenda kuwakandamiza wakulima, inaenda kutukandamizi sisi, maji ni uhai tutaendeleaje hivi?

Mheshimiwa Spika, hii naomba iangaliwe upya iwe reviewed ile Sh.50/= ambayo ilikuwa inakwenda kwenye Mfuko wa Maji iendelee kuwepo kwenye Mfuko wa Maji kwa sababu hii ndiyo itakayotukomboa sisi, bila maji maendeleo yanapatikana wapi? Bila maji kilimo hakipo, hatuwezi kuwa tunategemea kilimo cha mvua wakati kuna mabadiliko ya nchi ambayo hata sisi tumeshindwa ku–accommodate. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhima ya bajeti ya mwaka wa 2017/2018 imejikita katika kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii. Naomba tu niwaachie hili swali, kivipi? Hapo tu, naomba mkajitafakari kwa hapo, najua mna timu yenu ya wataalam, Mawaziri najua mpo vizuri, naomba mtujibu, kivipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 19 na 20 wa kitabu cha Mpango kimegusia suala very briefly mabadiliko ya maisha ya watu. Hotuba ilipogusia hili naona ilijizungusha bila kutuambia haijajielekeza umaskini utashuka au utashushwa kwa kiwango gani? katika nchi yetu na nafikiri walishindwa kujieleza utashuka kwa kiasi gani kwa sababu wameshindwa kushika zile sehemu muhimu ambazo zitatutoa wananchi kuondoa umaskini; kilimo na maji, elimu na vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti iliyopita ilitekelezwa kwa chini ya asilimia 30 na miradi ya maendeleo haijawahi kuzidi asilimia 40. Nafikiri hapo ndio maana Mheshimiwa Waziri alipata kigugumizi cha kuweza kutueleza kwa umakini, umaskini unaweza ukaondoshwaje...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, ahsante.