Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika mjadala huu ambao ni muhimu sana kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono maoni yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani na niiombe sana Serikali kwamba mara nyingi ukitaka kwenda vizuri ni vizuri ukajiangalia kwenye kioo. Sasa haya maoni yaliyotolewa hapa kama Serikali ikiamua kujiangalia kwamba upande wa pili wanaonaje, inaweza ikasaidia sana na ikawa na mchango mkubwa na tukakwepa kwepa haya mambo ambayo jinsi tunavyokwenda mbele tunaendelea kuumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kwa kweli napata shida sana Wabunge wenzangu ambao wanawakilisha Watanzania ambao tunajua hali zao wanavyosema kwamba hii bajeti ni bajeti ya aina yake, ni bajeti nzuri. Kwa sababu nikianza kwenye kuangalia vipaumbele, nashangaa kabisa kwamba tunavyoweka ndege katika nchi hii kama kipaumbele sijui tunatumia vigezo gani, kwa sababu ukienda kwenye huu Mpango wa Maendeleo wa Taifa ukurasa wa Nane kuna uchambuzi umefanyika pale unaoonesha key sector katika pato la Taifa, hakuna ndege na katika michango yote hakuna ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango anafahamu kwamba unapotaka kuwekeza kwenye kitu chochote ni lazima uende kwenye kuangalia ni wapi utapata matokeo makubwa (comparative advantage). Sasa inavyoamuliwa kwamba tukawekeze ndege wakati huu shilingi karibu trilioni moja, kwa sababu tumeshanunua ndege mbili, tumetenga billioni 500, tunachukua madeni yote ya ATCL na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye hili jedwali ambalo nimelirejea, mchango wa kilimo ni asilimia 29 kwenye pato la Taifa. Hata hivyo, ukienda kuangalia leo kwenye bajeti ya kilimo cha umwagiliaji tumetenga billioni 24, tena hizo bilioni 24 bilioni 15 zinatoka nje, za kwetu tulizotenga ni bilioni tano. Leo hii tunanunua chakula kutoka nje ya nchi, ukienda kuangalia imports za nchi hii asilimia tisa ni chakula, tunawezaje kupiga hatua? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa kama tunakwenda kuweka pesa nyingi namna hiyo na tunasema na tunakaa hapa kweli tunajivuna kwa sababu najaribu ku-recall Mzee wangu rafiki yangu sana Mheshimiwa Keissy siku moja hapa Mheshimiwa Heche alisema anataka kiwanja Tarime, Keissy akasimama akasema kule kwao wanataka barabara tena za changarawe, leo hii tunakuja hapa tunapiga makofi kwamba eti ndege ni kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukienda kuangalia competency yetu kwa maana ya soko la ndani silioni, ukienda kuangalia competency yetu Kimataifa kwa maana ya kushindana na kupata faida, sioni, hatuna economies of scale, hatuna ukubwa wa kuweza kushindana na ikawa ni faida. Kwa hiyo, suala la biashara ya ndege is a high risk business, ndio maana watu wanakwendaga kukopa sio kulipa cash.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri kwamba huu ni mkenge ambao tumeamua kuuvaa na nafikiri kama tunawakilisha kweli Watanzania ambao siamini kama wanafika hata 10,000 ambao wanaweza wakawa na manufaa na hiyo ndege. Nafikiri tungesimama kama Bunge tukasema kwa kweli huu uwekezaji wa aina hii tumepotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye hoja yangu ya pili, nikienda kwenye hoja yangu ya pili…

TAARIFA .....

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, siipokei kwa sababu haina ukweli wowote kutokana na rejea mbalimbali ambazo ziko mbele yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya pili ni kwamba, bajeti hii ukiiangalia kwa makini ina asilimia kubwa sana ya kubahatisha, asilimia kubwa sana ya kupiga kamari. Kwa sababu tuna pesa ambazo tumesema trilioni 7.7 tunakwenda kukopa tena ndani kwa kiasi kikubwa, tuna trilioni 3.9 ambazo tunatarajia tupate kutoka nje ya nchi kwa maana ya misaada kwa maana ya mikopo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ukweli na uhakika wa kupata fedha hizi ni mdogo sana, bado tuna tatizo la Zanzibar ambalo linatuletea matatizo. Kwa hiyo, nafikiri tukitaka kuwa realistic bado tuna kazi kubwa ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni kuhusu mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga. Ukiangalia kwa kauli ya Waziri mwenyewe anasema huu ndio msingi mkuu wa kuchochea mageuzi ya viwanda katika nchi hii lakini ukienda kuangalia wanasema kila kitu kimekamilika, ukienda kujaribu kusoma katika Wizara zote unaona kwamba tatizo lililopo sasa hivi ni Serikali yenyewe haijatoa GN, are we serious?

Mheshimiwa Spika, kweli tuko serious kwamba tunataka kwenda kwenye mageuzi ya viwanda katika speed ya namna hiyo, wanasema mwekezaji amekwisha patikana na ameshatenga pesa, lakini Baraza la Mawaziri lilikaa mwaka jana likaamua kwamba wakapitie upya na kuona vivutio vile vilivyopo vina maslahi gani kwa Taifa. Ni jambo zuri lakini huoni kwamba hiyo ni ndoto katika hali ambayo

unasema unaye mbia lakini hujampa package ya incentives, maana yake utakapokuja kutoa hizo incentives anaweza aka- withdraw.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, ni hili linaloendelea la mchanga, naomba niungane na wote wanaosema kama Rais yuko serious na kwa kweli vita hii haikuanza leo, mnakumbuka kulikuwepo na Kamati ya Dkt. Chipokola ya mwaka 2004 na ukienda kuisoma haina tofauti na mambo ya Osoro ya jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwepo na Kamati ya Lawrence Masha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja na naomba ile kinga ya Marais waliotangulia iondolewe.