Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi nami nichangie hoja hii iliyoko mbele yetu.

Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama mahali hapa kuchangia hii hoja, aidha niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango, Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa kutuletea bajeti ya kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni nzuri, ni ya matumaini makubwa kwa wananchi na wananchi wameipokea pamoja na kebehi zote zinazotolewa na Wapinzani Wabunge wenzetu, lakini bado wananchi wameisifia na wanakwenda kuitekeleza kwa sababu ni bajeti shirikishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mawasilisho ya Kambi Rasmi ya Upinzani, wenzetu wameibeza bajeti hii katika misingi ya takwimu. Kutofautiana kwa vitabu Volume One, Two, Three, Four ni suala la takwimu tu ndugu zangu, haiwezi kuwa suala la kihistoria kwamba bajeti hii haifai. Kuna wachangiaji wachache wametuhumu sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kujenga kiwanja cha ndege kule Chato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais wa Tanzania lakini ni Rais anayetambulika kimataifa, ni Rais anayetambulika na dunia nzima, ajenge kiwanja cha ndege mashuhuri, tena kikubwa sana kule Chato, watu wengi watapenda kwenda kuona amezaliwa wapi Rais Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu ni wa kimataifa na watu wengi wanampenda, kujenga kiwanja cha ndege ni kitu kidogo sana na binadamu hana jema…

TAARIFA.....

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, binadamu hafananishwi na mwenzake, kila mtu na mazaliwa yake, mapendo yake, juhudi zake na mambo yake tofauti, kwa hiyo siipokei hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la ukusanyaji wa fedha TRA. Mwaka jana wakati tunapitisha Sheria ya Fedha (Finance Bill) tulikubaliana TRA inaenda kukusanya kodi ya mapato kwa ajili ya mapango na kadhalika. Sheria hiyo ya Fedha, tuliipitisha hapa Bungeni wakiwemo Wapinzani ambao leo wanaikebehi. Sababu za TRA kukusanya kodi iko katika ukurasa wa 28 waende kusoma, kipengele cha 38. TRA imefanya ufanisi mkubwa sana katika ukusanyaji wa kodi na TRA ina mtandao mpana sana hapa nchini kulingana na Halmashauri zetu.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba nijielekeze kwenye kuchangia bajeti. Bajeti hii siyo tu imeanisha namna ya kukusanya mapato kwa ufanisi, bali pia imefafanua namna ya kupata, kutumia na kwa uwazi zaidi, ndio maana tunampongeza sana Dkt. Mpango pamoja na Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji. Kubwa zaidi ambalo limewapendeza wananchi ni kwamba bajeti hii imejielekeza kuwanufaisha wakulima wadogo na walalahoi wa vijijini kwa sababu inaenda kuboresha kilimo kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta pekee inayogusa wananchi walio wengi ili waweze kuendelea na kuondoa umaskini ni sekta ya kilimo. Kwa hiyo, bajeti hii inakwenda kuboresha kilimo na kuondoa umaskini katika nchi yetu na ndio maana wananchi wameipokea kwamba ni bajeti ya kihistoria na inaenda kuwanufaisha wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya 2016/2017. Bajeti hii imeainisha ufanisi, pia imeainisha changamoto, bado kuna changamoto chache. Katika miradi ya maendeleo tumeona kwamba fedha zetu za miradi zilichelewa, tuna imani kwamba Waziri wetu anaenda kuangalia kwa umakini sana changamoto ya kuchelewesha fedha za miradi, vilevile kuhakikisha kwamba zinafika kwa wakati na zinakwenda jinsi bajeti hiyo ilivyokuwa imeidhinishwa na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna mikakati ya mipango tuliyojiwekea kwamba haijakaa vizuri na hiyo nayo ni eneo la kuliangalia kwa sababu haina maana mipango yetu tuiweke mizuri lakini haiendi kutekelezwa jinsi ambavyo tumeainisha kwenye kitabu cha mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwamba ili bajeti hii iwe shirikishi tuweze kuteua kamati itakayosaidiana na Baraza la Madiwani kuhakikisha kwamba Wenyeviti wa vijiji, Maafisa Watendaji, wazee wawili, viongozi wa dini, timu kamili iweze kuundwa kuhahakikisha kama watchdogs, kuhakikisha kwamba fedha zinazokwenda kwenye miradi na fedha zinazotoka kwenye tozo mbalimbali zinazokwenda kwenye maji ziweze kuangaliwa, ziweze kunufaisha wananchi jinsi ambavyo Bunge limepitisha na kuhakikisha kwamba zimewanufaisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye kukuza uchumi. Tanzania tumebarikiwa, tunazo rasilimali nyingi, tuna rasilimali watu, Rais wetu alisema kwamba kwenye maeneo mbalimbali imesheheni maprofesa, madaktari, mainjinia lakini bado tuna tatizo la rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwajibikaji na utekelezaji wa masuala mbalimbali bado uko nyuma kwa ajili ya utendaji usio wa uaminifu, wezi na mambo kama hayo. Naamini kwamba Waziri wetu Mheshimiwa Angellah Kairuki katika eneo hilo anahusika. Yeye ni Waziri makini, aende kuangalia ni namna gani atajengea uwezo watumishi wa umma ili waweze kuwa waaminifu kuhakikisha kwamba miradi yote ya maendeleo, mipango yote inayoelekezwa katika kuleta maendeleo, suala la rasilimali watu linapewa kipaumbele kuacha hata rasilimali fedha. Kwa sababu Baba wa Taifa aliwahi kusema kwamba fedha siyo msingi bali watu ndio maendeleo zaidi na juhudi inaletwa na rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye suala zima la vipaumbele katika nchi yetu. Katika utekelezaji wa bajeti ninashauri Serikali iangalie maeneo ya pembezoni. Naomba kutoa mfano mdogo, leo hii ukamchukua mwanamke wa Kihadzabe, ukamweka pale ukampa milo mitatu, ukampa mavazi, ukampa na mafuta ya kujipaka. Upande huu ukampa mwanamke wa Kiswahili, ukampa chakula milo mitatu, ukampa mavazi, ukampa na mafuta, yupi atakayeonesha impact haraka? Ni yule ambaye hana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wetu wa Manyara tuko pembezoni sana, tuna makabila ambayo bado wako nyuma sana, tunaomba utekelezaji wa bajeti hii ilenge maeneo ya pembezoni, iweze kuwanufaisha wananchi wale wa chini sana ili na wao waweze kuona maana ya kuwa Tanzania, maana ya kuishi katika hali nzuri kuondokana na umaskini na kuondokana hali duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara tuligawanyika kutoka Mkoa wa Arusha mwaka 2002, lakini hadi leo resources nyingi bado ziko Arusha. Mkoa wetu unazalisha mazao mengi sana, mazao haya yanafaa kwa ajili ya kuanzishwa viwanda vidogovidogo. Tazama ng’ombe wengi wanatoka Mkoa wa Manyara, wanatoka Simanjiro, Kiteto, Hanang na Mbulu lakini kiwanda cha nyama kiko Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iangalie kwa umakini sana ni wapi inaenda kuanzia kwa kuweka kitu gani? Ni wapi inaenda kuanzia viwanda kwa ajili ya rasilimali zipi? Tunaomba Kiwanda cha Nyama kijengwe Babati ili tuweze kutengeneza ajira ya wananchi wetu na kuweza kunufaisha wananchi wa Manyara na wanufaike na rasilimali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie potential ya kila mahali, Mkoa wa Manyara una potential katika michezo ya riadha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.