Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba kabla sijaendelea niwaambie wenzangu Waheshimiwa Wabunge waende katika Kitabu cha Maendeleo Fungu Namba 21 Hazina wataona pale kuna shilingi bilioni 60 kwa ajili ya Village Empowerment hapa ndio kwenye zile shilingi milioni 50 kwa kila kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijaribu tu kumsahauri Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hili ni agizo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi na humu ndani tuko vyama vingi ni vema hizi shilingi bilioni 60 ungeanza katika Majimbo yale ya Chama cha Mapinduzi ambao kimsingi ndio wameahidi kwenye Ilani yao, hizi Ilani nyingine ambazo hatujawahi kuziona ungeweka pembeni kwanza, kwa hiyo shilingi bilioni 60 ambayo iko kwenye Fungu Namba 21 Kitabu cha Maendeleo hiki hapa wote msome Village Empowerment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii adhimu kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya, kazi hii ya kuzuia makinikia, ni kazi ambayo ni ya ujasiri mno haijawahi kufanywa na kiongozi yeyote wa Taifa hili tangu Awamu ya Pili, ya Tatu na ya Nne. Kama tunasema zimeundwa tume lakini zimeishia kuwa ni Tume ambazo labda zimeweka makabrasha pembeni lakini huyu amechukua hatua ya kwenda hata kuzuia.

Kwa hiyo, ni jitihada za kijasiri sana ambazo zinapaswa kuungwa mkono na kila mzalendo wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimshauri na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria yuko hapa kwamba kuna watu wanatutisha kwamba tutashitakiwa. Lakini kwa bahati nzuri Mwenyekiti wa Barrick ameshakuja kuonesha kwamba anahitaji maridhiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili kwa sababu siyo jinai ni madai, madai yanaanza kwanza kuzungumza ninyi wenyewe, inaposhindikana ningeshauri kwamba tusiogope tuende kwenye Mahakama ya Kimataifa (International Court of Justice - ICJ), kule tunapelekana baada ya kushindwa kuelewana. Kwa hiyo hii ni mahakama huru kabisa tunakwenda kule tunashitaki na tunaweza tukapata haki zetu stahiki, kwa sababu kuna dispute imefanyika ndani ya mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka niseme hata kwenye Mahakama zetu, kuna ile alternative dispute resolution ambayo kabla hamjaamua kushtakiana mnaweza kwanza mkakaa ili kutafuta amicable way ya ku-solve matatizo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri najua wewe huna makeke ni mtulivu na ni mwanasheria ambaye umebobea, kwa hiyo hili naamini litakwenda vizuri.

T A A R I F A

HE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii kwa kuwa amesema ndugu yangu Khatib kwamba naye anaelewa kwamba mwelekeo ni kulipa basi naipokea, safi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwenye tozo ya shilingi 40 kwenye mafuta, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapozungumza hii tozo, kwanza inaanza kutozwa kwenye ushuru, yale makampuni yanayoingiza mafuta ndio kwanza wanawekewa hii tozo. Mafuta yakishalipiwa ushuru yakishatoka, yakishaingia kwenye usambazaji hakuna tena kodi pale, mafuta hayana VAT ndio maana EWURA wako pale kwa ajili ya kuweka bei kikomo. Sasa hivi kwa sababu tunaingiza mafuta kwa njia ya bulk procurement maana yake ni kwamba hata EWURA wataangalia competitive price na kwenye price stabilization ya mafuta REA ipo, reli ipo, kwa nini tushangae mafuta leo? Hata hiyo shilingi 50 ya maji ipo, mbona gharama hazikuongezeka? Kwa hiyo hili ni suala la kitaalam. Mambo haya ya mafuta niwaambie hata hayo mafuta ya taa sasa hivi tunaagiza kiasi kidogo sana, yako makampuni 23 yanayoingiza mafuta hapa nchini, lakini hayazidi matano yanayoingiza mafuta ya taa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuta ya taa yanatumika kwa kiasi kidogo sana sasa hivi, tusidanganye, ni lazima Watanzania tutanue wigo wa walipa kodi. Walipa kodi walikuwa ni wachache sana ndio maana hao hao kila siku wanakamuliwa, lakini tunavyotanua wigo wa walipa kodi maana yake ni kwamba hata huyu mtu mdogo ambaye anatumia lita mbili atuchangie shilingi 80. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii niseme kwa dada yangu Mheshimiwa Majala, wewe ni Muislam na katika uislam kuna Zakatul - Mal (zaka ya mali) kila shilingi 100 unatakiwa uilipie japo shilingi mbili na nusu, hii haikwepeki. Hata katika Wakristo fungu la kumi lipo, kodi haijawahi kumpendeza yeyote. Tunasema hapa lazima watu walipe ushuru, lazima walipe kodi, kama ambavyo kanisani watu wanatoa sadaka na kama ambavyo kanisani watu wanatoa fungu la kumi na kule misikitini watoza Zakatul- Mal na hata huu mwezi wa Ramadhan wewe unatakiwa utoe Zakatul- Fitr kabla ya kuswali sala ya Idd. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mamlaka hii ya Magufuli ni mamlaka inayotoka kwa Mungu na haya ndio maagizo kwa mujibu wa vitabu. Kwa hiyo, lazima tutanue wigo wa ulipaji kodi, kodi inapolipwa na watu wengi kwanza inakuwa ni rahisi kulipika, inapungua, pia tunaongeza katika mfuko wetu tunapata kodi nyingi zaidi. Nani aliyewaambia kodi ya road licence ilikuwa inaenda kununua maandazi ya wafanyakazi wa TRA? Ilikuwa inaenda kwenye huduma. Kwa hiyo, hata hii ya tozo ya mafuta inakwenda kwenye huduma, hivyo tusubiri mwakani kama utekelezaji haupo, tuwaambie mmechukua shilingi 40 kwenye kila lita utekelezaji wake uko vipi, lakini suala la kodi halikwepeki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la viwanda. Kule Tanga viwanda vyetu vingi vimefungwa kwa sababu ya mambo ya kodi pia wengine ni kwa sababu ya ushindani wa kibiashara. Naomba nitoe rai Kiwanda cha Afritex cha nguo kimefungwa, nimeshazungumza sana Mheshimiwa Waziri, pia wenzetu wale wa Tanga Fresh wanapewa deni ambalo haliwahusu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri ulisimamie deni hili ili wawekezaji hawa waweze kuona comfort ya kufanya biashara katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kiwanda cha Chai cha Mponde, umeshazungumza kwamba wawekezaji kupitia Mfuko wa LAPF watakwenda kuwekeza pale, lakini sasa ni mwaka wa tatu bado tunaona mambo hayaendi. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba katika Halmashauri ya Bumbuli, Jimbo la Bumbuli, Kata 14 zinalima chai, kwa hiyo, kufungwa kwa kiwanda hiki ni msiba mkubwa wale wananchi kwa kweli tumewakosea sana, wanashindwa kuzalisha mali na wanashindwa kuongeza pato la Taifa kupitia uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni usambazaji wa umeme vijijini. Ninashukuru kwamba Wizara ya Nishati na Madini imetoa vijiji 146 katika Mkoa wa Tanga, ni vijiji vichache sana ukifananisha na Mikoa mingine. Nimuombe Waziri mwenye dhamana aliangalie hili kwa umakini sana, kwa sababu kama katika Halmashauri ya Lushoto na Halmashauri ya Handeni, Halmashauri pekee zina Majimbo mawili mawili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Waziri mwenye dhamana tuangalie hili kwa kina sana kuhakikisha kwamba tunapata viwanda vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nashukuru naunga mkono hoja.