Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa nami nichangie mada iliyoko mbele yetu. Kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa na kuwasilisha Bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja moja kwa moja. Katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa 47 mpaka 48 Mheshimiwa Waziri amebainisha jinsi Serikali inavyojitahidi kudhibiti mapato kwa kuweka mashine za EFD na pia kuwa na mfumo wa kieletroniki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi zote za Serikali bado kuna baadhi ya wafanya biashara ambao sio waaminifu hawatoi risiti na kuna baadhi ya wananchi wengi bado hawaombi risiti. Hivyo basi, mapato mengi hayaingii katika mfumo ambao tumejiwekea.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana baadhi ya wafanya biashara na wananchi hawafahamu umuhimu wa kodi kwa maendeleo ya Taifa. Nilikuwa napenda kuishauri Serikali yangu sikivu pamoja na Wizara ni budi kwamba hii elimu ya mlipa kodi bado inahitajika sana katika jamii yetu na ikiwezekana iwe ni ajenda ya kuduma na hata ikiwezekana ianzie katika shule za msingi ili wanafunzi wetu waweze kuipata elimu hii ili mwisho wa siku watakapokuwa watu wazima na wao wasiweze kukwepa kodi kwani watafahamu faida ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa pia ninaomba niongelee kuhusu sekta ya utalii, nidhahiri kwamba sekta ya utalii imekuwa ikiingizia Taifa letu fedha za kigeni na ni sekta ya pili kwa kuingizia Taifa letu fedha za kigeni. Lakini kwa masikitiko makubwa sana katika bajeti hii, katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri halikutiliwa mkazo hili jambo kuhusiana na hii sekta ya utalii. Sambamba na hilo katika hotuba ya Kamati ukurasa wa 40 imebainisha kwamba bado sekta ya utalii inakabiliwa na changamoto za Kisheria pamoja na za kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba utalii ambao uko hapa nchini kwetu ni ule ambao ni high profile tourism ambapo watalii wengi wanaokua hapa nchini wanatumia matumizi yao makubwa zaidi ni pamoja na mahoteli na usafiri. Katika malazi mahoteli mengi sana yanamilikiwa na wageni, hivyo basi pesa nyingi za kigeni haziingii hapa nchini badala yake zinawanufaisha wale wageni katika nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa tu naomba niishauri Serikali yangu kwamba hebu ingeweka mkakati wa uhakiki wa kuona ni jinsi gani wazawa wanawezeshwa ili kusudi waweze kumiliki haya mahoteli ili mwisho wa siku, pesa hizi ziweze kubakia hapa hapa nchini na sisi tuweze kufaidika na pesa hizo. Kwa sababu kwa taarifa iliyopo pesa inayobaki kwenye utalii ni pesa kidogo sana ambayo ni hotel levy, pamoja na ile pesa ambayo inatokana na kwenye mishahara ya pay as you earn. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo jambo jingine ambalo katika utalii ni suala zima la usafiri. Usafiri unachukua asilimia 50 ya mapato katika suala zima la utalii, hivyo basi nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuamua kuleta ndege na kulifufua Shirika la Ndege, pamoja na dhamira ya dhati ya kuona kwamba ndege zaidi zinaweza kupatikana, kwa sababu upatikanaji wa ndege hizo utasaidia sana utalii katika nchi hii kwa hiyo kwa vyovyote vile pato la Taifa litaweza kuongezeka kutokana na utalii. Kwa sababu kwa takwimu zilizopo ni kwamba, zaidi ya dola 1.5 bilioni ambazo zimelipa kwenye sekta ya utalii, zimekwenda kwenye usafiri na kwenye usafiri huo waliofaidika zaidi ni mashirika ya ndege ya nje kwa mfano kama Qatar Airways, Emirates na mengine ambayo pia sikuyabainisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba hebu Serikali naendelea kumuombea Mheshimiwa Rais aendelee kufanya kazi kwa bidii sana pamoja na longolongo zote hizi zilizopo, pamoja na maneno ambayo baadhi ya wananchi wanamkatisha tamaa, wenzetu wa upinzani lakini ukweli ni kwamba mwisho wa siku watajua nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais kwa sababu ana nia nzuri sana kwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba niungane mkono pamoja na wenzangu wote ambao wamenzungumzia kuhusu hii tozo ya shilingi 40 katika mafuta na mimi pia niungane na wenzangu kwamba hebu Serikali ione ni jinsi gani tozo hii sehemu yake ipelekwe katika sekta ya maji ili kusudi tuweze kumtua mwanamke maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la sekta isiyo rasimi napongeza Serikali kwa yote, lakini mimi ushauri wangu ulikuwa ni kwamba ili kusudi tuweze kujua idadi ya watu walioko katika sekta isiyo rasimi, ni vizuri ukafanyika utaratibu wa sensa katika kila Wilaya, katika kila Halmashauri, katika kila Mji au Jiji ili kubaini hao watu wako wangapi, lakini mwisho wa siku ufanyike utaratibu wa watu walioko katika sekta isiyo rasmi waweze kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja na ninashukuru sana kwa kunipa fursa, ahsante sana.