Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu katika kujadili bajeti hii ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kunijalia afya njema, uwezo na hekima katika kujadili majadiliano mbalimbali katika Bunge hili. Leo hii napenda sana nimuombe Mwenyezi Mungu anijalie hekima ili niendelee kuishauri Serikali yangu ambayo ni sikivu na naamini kabisa kwamba watanielewa na kufanyia kazi maoni yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza, naomba kidogo nikosoe jambo moja. Kuna Mbunge amemaliza kuchangia akasema kwamba Serikali ya CCM ni wezi, lakini katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 8 inaonesha ni jinsi gani Serikali inavyomilikiwa na wananchi kwa maana kwamba watendaji wanafanya kazi kwa niaba ya wananchi. Kwa hiyo, itakuwa si sahihi nikiendelea kuruhusu Mbunge mmoja kusema kwamba Serikali ya CCM ni wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hilo ambalo yule Mbunge ametoka kuchangia akasema Serikali ni wezi liweze kufutwa kwenye Hansard. Kwa sababu Wana-CCM siyo wezi na ndiyo maana mara kwa mara Serikali ya CCM imekuwa ikijikosoa pale ambapo inaona imekosea, bali ni mtendaji mmojammoja ndiye anayekosea, hivyo huwezi ukasema kwa kutumia ule msemo kwamba samaki mmoja akioza wameoza wote, anashughulikiwa mtendaji mmojammoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, naomba tena niende katika kipengele kingine cha kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Ninayo furaha kubwa sana kwa siku ya leo kumpongeza Rais wetu. Kwa sababu gani ninampongeza Rais wetu? Rais huyu ni fahari ya Watanzania, ni fahari ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi, ni fahari ya mataifa mbalimbali na ni fahari kwa dunia nzima. Mambo ambayo anayafanya Mheshimiwa Rais Dokta Magufuli anastahili kupewa pongezi yeye kama yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge siku moja alidiriki kusema kwamba Mheshimiwa Magufuli alisema ni Serikali ya Dkt. Magufuli, hapana, siyo kwamba alisema chagua Serikali ya Magufuli bali alitaka tumuamini yeye kama mtu lakini si kwamba Serikali ni ya kwake, Serikali inamilikiwa…

TAARIFA....

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Bwege kwa kweli siwezi kuikubali na ndiyo maana nilianza kwa utangulizi wa kuongelea Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lowassa alikuwa ni mtendaji na atawajibika kama mtendaji. Mimi sitaki kuyahesabu yaliyopita, nasonga mbele na haya tuliyonayo sasa hivi. Ndiyo maana nikasema siku ya leo naomba Mungu aendelee kunipa hekima na naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, kwanza naomba unilindie dakika zangu kwa sababu nilizitenga kwa makundi, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli sisi wana CCM tunayo kila sababu ya kujivunia. Hata mimi mwenyewe naposimama hapa siku ya leo nasimama najidai kwa sababu tumemchagua Rais, tukamnadi sisi wenyewe, tukatembea kijiji kwa kijiji, nyumba kwa nyumba, shuka kwa shuka tukitafuta kura za Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Leo hii siwezi kuona aibu kuivaa nguo ya kijani kutembea barabarani kumuongelea Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa sababu mambo anayoyafanya naamini kabisa hakuna Mtanzania ambaye angeweza kuthubutu, mambo aliyoyafanya ni ya msingi sana na ni mazito na yanawagusa wanyonge. Ndiyo maana katika michango yangu ndani ya Bunge hili nimekuwa nikimtaja Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwamba ni Rais ambaye yuko tayari kuwatumikia wanyonge na napoona kuna kitu ambacho kinawakandamiza wanyonge nimekuwa nikijaribu kuishauri Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kurudi katika michango ya bajeti. Naomba kuchangia suala la Deni la Taifa. Katika kitabu chake Waziri wa Fedha na Mipango ameongelea suala zima la ustahimilivu wa Deni la Taifa. Mimi sipingani na hilo lakini nachokisema ni kwamba Deni la Taifa kama ni stahimilivu waendelee kukopa lakini Deni la Taifa linapokuwa linaongezeka halafu Watanzania wanaendelea kuishi katika maisha ya umaskini, tunaona hakuna sababu ya kukopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali jambo moja, tunapokopa na tunapoendelea kuongeza Deni la Taifa kama anavyosema kwamba bado ni stahimilivu, liende likawekezwe kwenye miradi ambayo inaweza ikawasaidia Watanzania. Kwa mfano, kuna matatizo ya maji mpaka leo kila Mbunge akisimama humu ndani analalamikia suala la maji katika jimbo lake, Mkoa wake na Wilaya yake. Sasa najiuliza swali, hivi Deni hili la Taifa ambalo linaongezeka siku hadi siku halafu wananchi bado wanaendelea kulia na maji, mnasema kwamba tunamtua mwanamke ndoo kichwani lakini katika hili bado hatujafaulu. Naomba niendelee kuishauri Serikali iweze kuzingatia mambo haya ya kurekebisha masuala mazima ya miradi ya maji. Kuna miradi mingi sana ambayo inaanzishwa lakini haikamiliki. Kwa hiyo, utaona ni jinsi gani Deni hili la Taifa bado halijawa la kuwanufaisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kidogo Mkoa wa Mwanza. Kwa mfano, kuna mradi mkubwa wa maji kule Ilemela ambao ulikuwa unafadhiliwa na World Bank, mradi huu ulikuwa ni wa vijiji kumi lakini katika hivi ni kijiji kimoja tu cha Kayeze ambacho ndiyo kimepata maji, lakini vijiji vingine kama vile Nyafula, Kasabangu, Nyamadoke, Kabangaja, Sangabuye na kwingineko kote huko bado hawana maji. Ukiangalia pale Mwanza tumezungukwa na Ziwa Victoria, fikiria wale tu ambao wanaishi kandokando ya Ziwa Victoria wanaenda kuchota maji machafu ina maana Serikali imeshindwa kuwasogezea maji katika nyumba zao. Naomba sana Serikali iliangalie suala la usambazaji wa maji katika vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika mradi ambao unatokea Misungwi kuelekea Kahama na Shinyanga umeviacha vijiji vya Nyangomango, Ilambogo na Ibinza. Siku moja Mheshimiwa Mbunge wa Misungwi hapa aliongea kwa uchungu sana na watu hawakumuelewa lakini mimi nilimuelewa kwa sababu nimepita katika vijiji vile na nikaona tatizo lililoko pale. Hatutaweza kuvumilia hali hii ambapo miradi ya maji inapita halafu inaviacha vijiji vile vya kandokando pale vyote havina maji halafu mnaona maji yanapita kutoka Ziwa Victoria yakienda sehemu nyingine halafu vile vijiji vinakosa maji. Naomba sana Serikali iweze kujirekebisha katika suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia upande wa Sengerema kuna mradi mkubwa ambao unatakiwa kusambaza maji lakini bado kuna vijiji ambavyo havina maji, kwa mfano Kijiji cha Kwang’washi na chenyewe hakina maji, wananchi kila siku wanalia, akina mama wanaamka wanatembea kilometa zaidi ya 20 kwenda kutafuta maji. Kwa kweli kama tuko tayari kusaidia wananchi wetu ambao ni wanyonge, hebu tuwasaidie katika kutatua matatizo yao ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu sijaona suala la kilimo. Kama tunavyofahamu asilimia 75 ya Pato la Taifa inachangiwa na kilimo. Sioni ni kwa sababu gani tunashindwa ku-link bajeti kuu ya Serikali na suala zima la Kilimo. Naomba Waziri wa Fedha na Mipango atakaposimama atueleze sisi Waheshimiwa Wabunge suala la kilimo analiweka vipi, tunaelekea wapi, kwa sababu kama tunaenda kwenye uchumi wa kati au uchumi wa viwanda tutafikaje kwenye uchumi wa viwanda wakati kilimo hakitiliwi maanani. Naomba sana Serikali iweze kutilia maanani suala la kilimo kwa sababu kilimo kitaweza kusaidia wananchi wengi kuajiriwa kwenye mashamba lakini hatimaye pia kuondokana na suala zima la njaa, kwa sababu tunaona vijiji vingine wanakufa na njaa na hili hatuwezi kuacha kulisemea kwa sababu wananchi hawatatuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee hali ya uchumi. Kwa masikitiko makubwa sana nilipokuwa nikisoma kitabu cha fedha na mipango, Waziri anasema kwamba hali ya uchumi ni nzuri. Kusema ukweli hali ya uchumi si shwari, hali ya uchumi ni mbaya sana, wananchi wanaishi maisha ya kimaskini, hata hajui kama atapata hata mlo mmoja, si tu milo miwili au mitatu, hajui hata kama atapata mlo mmoja. Naomba Serikali inapokuwa inaandika vitu ijaribu kuangalia maisha ya Watanzania kwanza yako vipi. Inawezekana wataalamu ambao wanaandika hivi vitabu wao wana maisha mazuri, kwa hiyo, hawafikirii wale Watanzania ambao wana maisha mabaya, ambao maisha yao hayako katika hali nzuri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.