Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mweyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza leo kupata nafasi hii ili niweze kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu tulipokuwa tunakwenda kwenye uchaguzi tuliomba atuletee Rais wa namna gani. Kwa hiyo nimshukuru, tusiposhukuru kwa kidogo huwezi kupata zaidi. Mwenyezi Mungu amesikia kilio chetu tumepata Rais ambaye tulikuwa tumemwomba kwa hiyo, ahsante sana Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, alivyoingia wakati anagombea kuna vitu aliahidi; aliahidi kusimamia rasiliamli za Taifa, ameanza kazi na mmeona. Aliahidi kununua ndege, aliahidi kujenga reli, aliahidi kuendeleza ujenzi wa barabara, aliahidi kuboresha huduma za afya, aliahidi kurudisha heshima na nidhamu kazini, aliahidi kubana safari za nje, aliahidi kuendelea kuboresha ukusanyaji wa kodi, aliahidi kuleta amani kwa watu kufanya kazi kupunguza kuandamana. Kwa sababu unakuta maandamano mengi yalikuwa ni kwa sababu watu hawana kazi za kufanya, lakini leo watu wanafanya kazi, muda wa kuandamana haupo, kwa hiyo nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia aliahidi kuendelea kupunguza kodi, hasa za wakulima, mmeona kwenye bajeti yetu kodi zimepunguzwa, niseme sasa wengi wameona, yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata bahati kubwa tusameheane, kwa sababu jana Mheshimiwa Dkt. Rwakatare na mimi niseme wazi Mheshimiwa Dkt. Rwakatare yupo hapa tunawapa kazi, Mchungaji ya kuombea Bunge hili ili watu tubadilike ukishirikiana na Mchungaji, Mheshimiwa Bilakwate yupo na Sheikh Ulega. Fanyeni kazi kubwa ya kuombea Bunge letu ili tubadilike tutetee maslahi ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni kweli kwa muda mrefu tumeibiwa, sasa tumesema basi na bahati nzuri tumepata bahati ya kupata Rais wa Wanasheria ambaye yuko humu ndani, tunakuomba Mheshimiwa , kwa sababu tumesema yaliyopita si ndwele utusaidie sasa tupambane tupate haki zetu kutoka kwa hao wazungu, kweli wewe ni rafiki yangu, tafadhali tuungane kwenye hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ustadh Ulega na Mheshimiwa Ustadh Lissu yupo pia. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa nizungumzie habari ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango; niseme ningekuwa niko kule Kigoma ningesema Mheshimiwa ushimwe chane yaani ubarikiwe. Umetendea haki Taifa, umetendea haki Bunge, umewatendea haki Watanzania wote na Wanakigoma. Niseme kazi ni kwetu wenyewe sasa kusimamia, suala la kusimamia rasilimali za nchi sio la Serikali peke yake, ni suala letu sote kuhakikisha tunasimamia rasilimali zetu kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Jimbo langu sasa la Kilolo kidogo. Kwenye Jimbo la Kilolo Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba atahakikisha tunapata maji safi na sasa hivi kazi imeanza, tumeanza kupata maji pale Ilula na sehemu nyingine mambo yanakwenda vizuri. Lakini pia kuna suala la kilimo cha umwagiliaji, kilimo hiki Iringa Wilaya ya Kilolo na Mkoa wa Iringa tuko milimani, kwa hiyo tunategemea sana kilimo cha mabondeni, wanasema vinyungu. Sasa ni suala la Serikali kutoa fedha kuboresha mifereji ili kile kilimo badala ya kuendelea kuzuia waache watu walime, waweke mpango mzuri, mifereji ya umwagiliaji ijengwe ili watu waendelee kulima badala ya kuendelea kuwazuia watu kulima kwa sababu tukifanya hivyo kuna hatari ya kupata njaa kwa Mikoa ya Iringa, Mbeya na mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kigoma kilimo cha mabondeni wanaita masebura, ni kilekile kwamba mnalima mabondeni, nikisema hivi Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amenielewa, kwamba masebura ni kilimo cha mabondeni sio cha kwenye vyanzo vya maji, vyanzo vya maji ni mbali lakini cha mabondeni wananchi waachwe waendelee kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokutafsiri vizuri sheria kutatufanya tulete njaa kwenye nchi hii. Kwa hiyo, nikuombe kabisa Mheshimiwa uniombee kwa Mheshimiwa Waziri wa Mazingira na Waziri wa Maji waweze kutafsiri vizuri zile sheria, kwamba kwenye vyanzo vya maji wazuie mita 60 lakini kwenye mabonde hawawezi kulima mita 60, hawaharibu vyanzo vya maji kule, wataalam wetu wasiwe wavivu wa kufikiria, ili washauri vizuri Serikali waende eneo husika wakaone kinachoendelea ndipo washauri Serikali, kwa sababu sasa hivi baada ya kutoa tangazo hilo Wakuu wa Wilaya kwa sababu wako kazini wanatetea vibarua vyao, Wakuu wa Mikoa, Watendaji wa Vijiji wameanza kuwanyanyasa wananchi. Sasa hata ile maana yote ya kupunguza kodi itakuwa haina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu REA nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliyepita kwa kuanzisha REA na Mheshimiwa huyu kuendelea kwa sababu leo nchi nzima inaenda kuwa nchi yenye nuru, taa zitawaka. Nishukuru kwamba katika Wilaya ya Kilolo vijiji vingi Mheshimiwa amenihakikishia tutapata na tutapata kwa sababu vyanzo vingi vya maji, vyanzo karibu vitano vya maji vinatoka Wilaya Kilolo, ndivyo vinavyojaza Bwawa la Kihansi, kwa hiyo lazima na mimi nipate ile ndiyo royalty au niseme ni privilege kwangu kwamba lazima tupate ili tuendelee kutunza vyanzo vya maji. Sasa ili tusiwakorofishe hilo, naomba Mheshimiwa tushirikiane waendelee kulima vile vinyungu vyao kwa kufuata taratibu ambazo zipo kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kulizungumza vizuri kabisa ni suala la barabara; Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Rais amehamia Dodoma, Wizara zimehamia Dodoma lakini asilimia 70 ya mbao zinazojenga hapa Dodoma zinatoka Wilaya ya Kilolo, lakini barabara ya Wilaya ya Kilolo iko dhooful-hali, Waarabu wanasema dhooful-hali yaani iko katika hali mbaya. Kwa hiyo, ningeomba utusaidie tuweze kupata lami, ni kilometa kidogo ziko kilometa takribani 17 na Serikali sasa hivi ilikuwa na mpango wa kila mwaka inajenga kilometa moja, lakiniā€¦

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwamoto, nimekuongezea dakika moja.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwahiyo naomba Mheshimiwa utufikirie ili tuweze kupata barabara ya lami lakini pia yale maboma ambayo yamebakia hayajamalizika, wananchi wamejitolea waweze kumalizia, Mheshimiwa tenga hizo fedha, uwezo huo unao. Naunga mkono hoja.