Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Jamal Kassim Ali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango na Bajeti ya Serikali. Kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya hususani katika suala la kusimamia rasilimali la taifa hili kuhakikisha rasilimali hizi zinanufaisha taifa hili na wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi toka alivyoanza kazi, toka alivyoapishwa mambo aliyoyafanya ni makubwa ni mambo ambayo yanajieleza yenyewe kwamba ni miongoni mwa Marais ambao wameji-commit katika kutusaidia kuleta maendeleo katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na timu yao kwa bajeti nzuri, kusema la ukweli bajeti hii imeenda kujibu ile dhana ya kwamba tunaenda kwenye Tanzania ya viwanda, tumeona namna gani sera za fiscal yaani kodi zilivyowekwa ili kusaidia uanzishwaji wa viwanda vya kati na vikubwa. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na maeneo machache ya kuchangia kama sehemu ya ushauri, eneo la kwanza ambalo ningependa kuchangia ni suala la kodi ya mapato. Kodi ya mapato kwa mujibu wa Katiba yetu ni kodi ya Muungano na chombo ambacho kinasimamia kodi hii ni Mamlaka ya Mapato ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua nchi yetu ina sehemu mbili kuna sehemu ya Zanzibar ambayo Zanzibar ina Serikali yake ambayo kwa upande mmoja inategemea kodi ambazo zinatokana na mapato ambayo kwa upande wa Zanzibar TRA ndio inakusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria yetu ya kodi ya mapato taasisi zote ambazo zitafunguliwa kama sehemu ya tawi la makao makuu, basi ofisi hizo hazitatoza kodi ya mapato, yaani kodi ya mapato itatozwa at a corporate level.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni nini, kwa upande wa Zanzibar tumekuwa na makampuni mengi ambayo Makao Makuu yake yako Dar es Salaam yanaendesha shughuli zao za kibiashara Zanzibar. Kwa harakahara tuna taasisi za fedha kumi yaani mabenki kumi ambayo zinafanya biashara Zanzibar. Tuna kampuni za simu tano, tuna kampuni za bima na kampuni mbalimbali ambayo yanatoa huduma na yananafanya biashara Zanzibar lakini kwa mujibu wa sheria yetu ya kodi ya mapato hazilipi kodi Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi ambayo inayokuswanya na TRA Zanzibar ndiyo kodi ambayo inaenda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya shughuli zake za uendeshaji na kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua Zanzibar, kiuchumi, uchumi wake ni mdogo, pia vyanzo vyake vya mapato ni hafifu. Naamini sasa busara itumike kwa makampuni haya ambayo yanafanya shughuli zake Zanzibar kama sehemu ya matawi basi na yenyewe yaanze kulipa kodi Zanzibar ili iweze kusaidia kuongeza mapato kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hivyo basi iweze kufanya shughuli zake za maendeleo na kijamii kama ambavyo tumeahidi kwenye ilani yetu ya chama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ningependa kuchangia kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani. Mwaka jana tulivyokuwa tunapitisha Finance Act kwenye Sheria ya VAT, tulipitisha kwamba bidhaa zote ambazo zitatengenezwa Tanzania Bara na kununuliwa Zanzibar na mnunuzi ambaye atakuwa amesajiliwa na VAT basi biashara hizi hazitatozwa kodi au bidhaa hizi hazitatozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kumekuwa na uzito katika utekelezaji wa suala hilo, kuna kesi nyingi sana, wafanyabiashara wetu ambao wananunua bidhaa hizi ambazo zinatengenezwa Tanzania Bara ikiwemo mabati, bidhaa za urembo wakitozwa kodi hiyo na wakienda Zanzibar wanatozwa tena. Kwa hiyo, kumekuwa na tozo mara mbili ambayo wafanyabiashara wetu wamekuwa wakitozwa na sheria iko wazi imeainishwa na tuliipitisha. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-windup labda utupe msimamo wa Serikali juu ya hili pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwaka jana tulipitisha Sheria ya Finance Act tulifanya mabadiliko katika Sheria ya The Electronic and Postal Communication Act kwa kuyataka makampuni yetu ya simu kwanza yawe listed katika Dar es Salaam Stock Exchange, lakini pia yatoe asilimia 25 ya hisa zake kwa wananchi au wakazi wa Tanzania. Lengo kuu ambalo Mheshimiwa Waziri alilolisema ilikuwa kwanza kuwapa fursa Watanzania nao kushiriki katika uchumi huu mkubwa ambao unakuwa wa sekta ya mawasiliano lakini pili kujenga uwazi wa kujua kwamba nini hasa biashara hii ya makampuni haya ya simu yanapata kutokana na muda mrefu kutokuchangia vile ipasavyo kwenye kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Watanzania kupitia Rais wetu tumeamka kwamba kwenye sekta ya madini tunaibiwa. Kila mtu aliyenyanyuka katika Bunge hili kuchangia, watu wote wamezungumza kwamba kwenye sekta ya madini tunaibiwa. Aidha, tunaibiwa kutokana na kutokuwa na uwazi wa kutosheleza kwenye biashara hii au sababu zinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwa vile Rais amesema sheria hizi atazileta Bungeni tuzifanyie maboresho na mikataba hii.

Kwa hiyo, niishauri Serikali itakapoleta sheria hizi wakati umefika sasa wa sheria hizi pia, makampuni haya makubwa ya madini yawe listed kwenye Dar es Salaam Stock Exchange iwe sharti namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sharti la pili lazima kuwe na local content participation. Lazima nao wafaidike na rasilimali yao, japo hatuna pesa nyingi lakini kwa kidogo kidogo tulichokuwa nacho naamini kabisa tunaweza tukachangachanga hicho na tukapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sheria nimezungumzia suala la sheria, lazima iwe mandatory si suala la mtu kupenda, tuna makampuni mengi zaidi ya Acacia, yanachimba madini. Kwa hiyo, lazima tuweke sheria ambayo makampuni yote ya madini yawe listed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya yote kuna umuhimu yakawa listed kwenye Dar es Salaam Stock Exchange.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwa kuunga mkono hoja, kuipongeza bajeti hii, naamini ni bajeti ambayo inatupa mwanga wa dira yetu ambayo tumeiweka ya kwenda Kwenye Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia.