Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyoko mbele yetu imeingia katika migogoro mingi tu, hii bajeti ya mwaka huu. Kwanza nianze na suala la madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1633 Kanisa Katoliki lilimdhalilisha na akafungwa mwanasayansi mmoja anaitwa Galileo kwa sababu ya kwamba alisema dunia inazunguka jua. Baada ya miaka 350 Vatican tarehe 30 mwezi wa kumi siku ya Ijumaa mwaka 1992 waliomba dunia radhi na walimuomba mwanasayansi huyu radhi, kwa sababu ni mfumo, uwajibikaji wa pamoja. Zaidi ya miaka 350 Galileo aliombwa radhi na Vatican. Sioni kwa nini tunaona aibu Serikali kuomba radhi Watanzania kuhusu suala la madini, kwa sababu ukiangalia tangu mwaka 1994 mpaka leo hii sheria na mikataba ni uwajibikaji wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukasema kwa sababu Serikali ilikuwani ya mwaka 1995 ni tofauti na Bunge hili, hata Bunge la 2015 watu walifukuzwa Bungeni huku kwenye masuala ya Sheria za Gesi pamoja na Mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kushabikia tu hapa ndani; mwaka 2002 nilikwenda Harare, tulikuwa Zimbabwe, kwenye mgogoro huu huu wa mapambano ya kiuchumi. Vita vya kiuchumi ni vibaya sana, kweli kweli! lakini lazima tuwe wakweli. Wakati wa malumbano wakaanza kusema kwamba kuna watu wengine wanaitwa wametumwa na wazungu, wengine wamefanywa nini, leo hii Zimbabwe haina hata sarafu yake, Zimbabwe imeangamia kabisa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vita hii; na nipende kuweka wazi Kambi ya Upinzani hakuna Mbunge hata mmoja kutoka Kambi ya Upinzani anayepinga wizi wa dhahabu ya Taifa la Tanzania, hayupo. Tunaangalia maslahi mapana ya mama Tanzania na msimamo wa Kambi ya Upinzani, wezi, wizi wa rasilimali za Taifa tuzishughulikie sote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya yakifikiwa lazima tukubali historia tulitoka wapi, tunajifunza kwa historia na kwa kuwa sasa Serikali iliyoko madarakani imelitambua hilo, tuko tayari kabisa kabisa kushirikiana kwa hili. Tuko tayari kabisa kabisa kupambana vita hivi endapo tutaacha kuwa na propaganda za kisiasa ambazo hazilisaidii Taifa la Tanzania. Tanzania ni yetu sote, Tanzania si mali ya kikundi cha watu wachache, tubishane kwa hoja, lakini yale mambo ya msingi Mheshimiwa Waziri yenye maslahi mapana kwa Tanzania tuyazingatie sote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo leo hii tutarudi kwenye makosa yale yale ya mwaka 1997, 1998 na mwaka 1997 nilikuwa kwenye Bunge hili, mwaka 1998 nilikuwa kwenye Bunge hili, sheria zilivyoletwa wengine wakabaguliwa tutarudi back to square one. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme na nirudie tena na Watanzania watusikie vizuri kabisa, mapambano haya tuliyaanzisha na kwa kuwa wenzetu mlio wengi mmekubaliana na sisi, tuko tayari kuungana na nyie kwa sauti moja endapo tutaacha propaganda na tuwe tayari kushugulika kweli kweli tushirikishane kweli kweli kwa maslahi mapana ya Tanzania. Si mtu yeyote ajitokeze aseme kwamba hili ni langu, hili ni langu, kuna msaliti, kuna huyu, hapana! Tunatahadharisha tu and it’s better to be pro-active rather than being reactive. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tukiangamia, tunaangamia sisi sote, Watanzania wanaoumia wanaumia wote, watoto wanaokosa huduma wanakosa wote. Waliouwawa migodini haikuchagua huyu ni wa CCM huyu ni wa Upinzani, huyu ni wa nani, tuliumia sisi sote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo vita hivi vituunganishe kama Taifa la Tanzania lakini tuwe wakweli wa dhati kabisa tushirikiane, tuungane kwa pamoja, tutavusha Taifa la Tanzania. Wengine wakionekana wasaliti, wengine hapana ni wa kudandia, wengine ndiyo wenye akili zaidi kuliko wengine tunaliangamiza Taifa la Tanzania, tutarudi kama mambo ya Zimbabwe, tusiruhusu masuala ya Zimbabwe yaje Tanzania na Bara la Afrika unaona tunavyochezewa. Tuanze kufikiria zaidi miaka 10, 20, 30 ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yale tuliyozungumza mwaka wa 1997, 1998 yangezingatiwa leo hii tungekuwa tumepiga hatua mbele.

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini amejibu hapa, amesema hata mrahabatunaopata tofauti na kwenye dhahabu ni asilimia tatu na almasi asilimia tano na ni kwa mujibu wa Sheria na kwa mujibu wa mikataba. Sasa tuunganike sote, tuone Taifa linavyoibiwa kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, ningependa kulitahadharisha Bunge na leo ni siku ya Ijumaa. Mtume Muhammad aliwahi kuwausia waumini wake, maarifa ni kitu chake kilichompotea muumini, popote akipatapo na akichukue. Hili suala la madini lazima Wabunge wapewe semina kwanza, kwamba uchumi wa madini ukoje, biashara ya madini ikoje. Tupewe semina kwanza tujue duniani biashara hii ikoje, tukifanya mabadiliko ya sheria kwa mhemko tulionao tutatandikwa kweli kweli kwa sababu tutafanya ni ushabiki kabla hatujajua mambo haya na tukubali huyu ana taaluma hii, huyu ana taaluma hii, tuwe na taaluma shirikishi, tushirikiane pamoja kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ili tuweze kutoka hapa, tuwe na mifumo endelevu ambayo inahimili. Leo hii yuko Rais Magufuli, kesho atakuja Rais mwingine, lakini kuna mifumo ambayo ni ya Kikatiba. Tukawa na Katiba mpya ambayo Rais yeyote yule anayekuja lazima ataheshimu katiba, sheria na taratibu, tutasonga mbele tukitoka hapa tulipo kwa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema haya kwa nia njema kabisa kabisa. Bila kupata elimu ya kutosha ya uchumi wa madini tutapata matatizo makubwa sana na lazima tukubali kushiriki kwa pamoja tutafute suluhisho ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine, Bunge letu hili huwa tunashabikia vitu ambavyo hatuvijui, Mithali 18:13 inasema kujibu au kushangilia kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu. Sasa tusije tukaanza kujishangilia, kujidhalilisha sisi wenyewe tunamdanganya nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ushabiki huu ambao unaendelea kwenye Bunge letu. Tunaona mambo ya ajabu ajabu ambayo yanaendelea kwenye Bunge letu, niombe tena chonde chonde; kwa mfano tuko kwenye viwanda viukuze uchumu wetu lakini viwanda tulikuwa navyo. Viwanda vilishabinafsishwa na kwenye zoezi la kubinafsishwa hata sisi wengine tuliumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi nimeshtakiwa Mahakama Kuu nadaiwa dola milioni moja kwa ajili ya mambo ya ubinafsishaji, Dkt. Mwakyembe anajua ile kesi ya NBC nashtakiwa mimi na wanaotushtaki ni hao hao wa upande mwingine ambao ndiyo wanashirikiana na hao kutudhalilisha kwa sababu ya kulitetea Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri nakuomba angalia sana Sekta ya Madini, angalia Uvuvi. Ukiangalia tozo zilizoko kwenye sekta ya madini, tozo zilizoko kwenye masuala ya uvuvi wa bahari kuu tukiwekeza vizuri kwenye sekta ya madini tukaondoa kodi zisizo na tija kwenye sekta ya madini, tukaondoa tozo zilizoko kwenye sekta ya madini ambazo ziko karibu kodi na tozo zaidi ya 57, tutavutia watalii kutoka milioni moja kwenda kwenye milioni mbili. Tutoke kuwa niexpensive destination hapa Tanzania utalii peke yake utaendesha uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunashika nafasi ya 110 kati ya Mataifa 133 katika ushindani wa utalii na mapato ya utalii; lakini ni wa pili katika vivutio vya utalii duniani. Let us think big, let us think globally and act locally. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubali kwamba Taifa hili tukiwekeza vizuri kwenye madini, kwa mfano hata kwenye uvuvi, bahari kuu ina kilometa za mraba 230,000; mapato gani tunayopata kwenye uvuvi? Nendeni mkasome ile na Mheshimiwa Waziri wa Fedha tulikuwa wote pamoja kwenye ile ripoti ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato.

Sasa tuwe tunaanza mapema kutengeneza na tuwe na muendelezo wa bajeti hizi ya mwaka 2015, 2016 ninazo zote hapa 2017. Angalia hata deni la Taifa, limetoka trilioni 35, likaenda 39 leo hii ni trilioni 50.8. Tanzania tunazidi kwenda kusiko, lazima tuwe na bajeti ambazo ni endelevu kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, na vyanzo hivi vipya vya mapato tushirikiane sote. Kwa sababu tukisema tu deni la Taifa himilivu, watoto wetu na vizazi vijavyo vitakuja kututandika makaburi yetu viboko kwa sababu tulikuwa hatuwezi tukafikiri vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mwenyezi Mungu akubariki.