Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mnyimi wa fadhila kama nisipomshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi hiki kifupi kwa wananchi wa Tanzania. Mwenyezi Mungu ampatie afya, ampatie nguvu na ampatie uwezo wa kuendelea kuifanya, ili adhma yake iweze kutimizika kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii kwa mwaka huu kwa kweli imefanya kitu ambacho kimewagusa wananchi wa Tanzania na hususan wananchi na akinamama wa Mkoa wa Rukwa. Bajeti ni nzuri na bajeti hii tukiisimamia nina imani kabisa kwamba itatekelezeka kwa asilimia kubwa zaidi na hatimaye kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la maji. Maji imekuwa ni kizungumkuti, maji imekuwa ni suala tete kwa akina mama, ni suala tete kwa wananchi wa Tanzania. Mimi napenda kutoa ushauri kwa Wizara yangu ya Afya na Wizara yetu ya Fedha kwamba tunaomba hii shilingi 40 naomba tuongeze tena shilingi 10 iwe shilingi 50. Kwa sababu hii fedha inahitajika kurudisha deni la Serikali, inahitajika kuleta umeme na inahitajika kuleta maji.

Mheshimiwa Mwenyekii, tunasema kwamba tunatua ndoo ya akina mama kichwani, lakini ukiangalia karibia asilimia 60 vijijini na vitongoji hakuna maji safi na maji salama. Mfano Mkoa wa Rukwa, ningeomba Serikali iangalie umuhimu wa kuangalia kutoa maji katika Lake Tanganyika. Lake Tanganyika maji yako ni mazuri, lakini tatizo ni kwamba, hayajawekewa mradi wa kuyaleta kwa wananchi. Mwambao wote huko wa Lake Tanganyika kuanzia Kala mpaka Karema, (Katavi) hakuna maji salama na maji safi, lakini Lake Tanganyika iko pale! Tungeiomba Serikali ikaangalia mradi wa kutoa maji Lake Tanganyika kwenda kwa wananchi wetu ili kinamama waweze kupumzika na suala la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema kwamba, tunatua ndoo ya mama, kama tunatua kweli ndoo ya mama, lakini mimi naona kuna wasiwasi wa kumpatia tena mzigo mwingine. Mzigo mwingine ni mkaa, nilizungumza katika mchango wangu wa msingi katika maliasili na utalii tukasema ya kwamba ni vema tukapewa semina Wabunge kuhusu mkaa endelevu ambao ni rafiki wa misitu, ili tukiuelewa ikawa ni faida kwa akinamama wasipate mzigo wa pili kabla ya kutuliwa ndoo ya maji kichwani. Kwa maana hiyo, tunaiomba Serikali tuongeze hiyo shilingi 10 iwe shilingi 50 ili iweze kutoa tatizo hili ambalo linakuja la pili kwa akinamama zetu kuwa mzigo wa pili ndani ya kichwa chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaloomba lingine ni kwamba, ni kuhusu suala zima la barabara. Mkoa wa Rukwa tumechelewa, Mkoa wa Rukwa tulisahaulika kuhusu barabara. Hadi hivi sasa bado hatujaungana na Katavi, bado hatujaungana na Kigoma, bado hatujaungana na Tabora. Ninaomba kwa sababu tunakubali kuunga Mikoa yetu na hizi fedha zinatoka katika Serikali yetu ya ndani, kwa hiyo, tunaomba fedha hizi zitoke katika ukamilifu wake ili tuweze kuunganika na Mikoa yetu ya jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mkoa wa Rukwa tunaungana na Kongo, tunaungana na Zambia, tunaomba Matai-Kasanga na Matai-Kasesya hizi barabara zikamilike. Kukamilika kwa barabara zitawasaidia akinamama kwenda kwenye masoko ya mazao yao hali kadhalika kwenda kupata huduma ya afya kwa sababu Mkoa wa Rukwa hatuna Wilaya hata moja yenye Hospitali ya Wilaya, zote tuna Hospitali Teule kwa maana ya Vituo vya Afya; kwa hiyo, akina mama wanatoka huko wanakuja Mkoani kuja kupata huduma ya afya, tunaomba hizi barabara, hizi fedha za ndani zitoke katika asilimia hata 75 angalau hizi barabara sasa ziweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninapenda kuzungumzia suala zima la elimu. Tunao watoto wetu walemavu, hawa watoto wetu walemavu wanahitaji kupata elimu, lakini vifaa vyao vya kufundishia ni vifaa vyenye gharama kubwa zaidi, Halmashauri hawawezi na hata wazazi kuchangia hawawezi. Lakini juzi nimesikia kwa Mheshimiwa Waziri akisema kwamba Waziri Mkuu amepokea vifaa vya elimu. Naomba hivyo vifaa vya elimu ya kufundishia viweze kupelekwa shule ya Malangali ya Watoto Viziwi, Vipofu pamoja na Albino hali kadhalika shule ya Mwenge ambako kuna watoto wenye mtindio wa ubongo waweze kupelekewa vifaa hivyo, waweze kupata elimu nao waweze kujiunga na sisi katika maendeleo ya jamii ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la shilingi milioni 50. Shilingi milioni 50 tumeizungumza na inawezekana kutekelezeka. Kutokana na kasi ya Rais wetu kuhakikisha kwamba, rasilimali ya nchi hii tunaitumia Watanzania, nina imani kabisa kwamba, hizi shilingi milioni 50 za kila kijiji zitapatikana kutokana na jitihada iliyopo katika Serikali yetu.

Kwa hiyo, ninaomba Serikali iweke tu utaratibu wa namna ya kuzisimamia na namna ya kuzifikisha kwa walengwa na wale wanaohusika ili ziweze kufanya kazi ya maendeleo. Nina imani kabisa kwamba jitihada ya Rais wetu Magufuli atasimamia ahadi zake kwa sababu hili alikuwa akilizungumzia sio kwa kuombea kura, alikuwa analizungumzia kwa kutaka kuhakikisha kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)