Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kupata fursa hii adhimu kabisa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mbunge wa Jimbo, vilevile Kiongozi wa Kitaifa nitagawa mchango wangu katika maeneo makubwa mawili. Eneo la kwanza nitazungumzia kama mwakilishi wa Jimbo langu, lakini naamini nikipata fursa nitazungumza mambo yote haya nitachangia kitaifa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiniuliza kuhusu bajeti naionaje? Nitakubaliana kabisa na wenzangu wengi kwamba bajeti ina sehemu imefanya vizuri na ina sehemu kwangu mimi imenikwaza. Sasa kwa sababu sehemu iliyofanya vizuri watu wameshazungumza na kuisifia, nitajikita zaidi katika sehemu ambazo zimenikwaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kifupi katika ile kuondoa kodi ya leseni ya barabara nimezungumza na wapiga kura wangu, watu wa bodaboda, taxi drivers kimsingi wanashukuru sana. Wanasema hii kodi imewasaidia sana na niliwahi kuwauliza mnasemaje kama Serikali ikiamua kuirudisha tena kule mnasemaje? Wengi hasa wa pikipiki wamesema bora hivi ilivyo sasa hivi, huu mtazamo wanauunga mkono sana. Kwa hiyo, hili nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mimi kwa jimbo langu la mjini nina tatizo sana la umaskini na umaskini kwangu mimi ninaupima katika mzunguko wa pesa. Mheshimiwa Waziri mzunguko wa pesa katika Mji wa Dar es Salaam umeshuka sana. Nashukuru kwamba umefanya juhudi za kufuta kodi mbalimbali pale bandarini, ambayo naamini kwa namna moja ama nyingine itaweza kuchochea uchumi, lakini naomba uyaangalie haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa watu wa Dar es Salaam utatusaidia sana kama utaleta ajira mpya. Ninapozungumzia ajira mpya nakusudia kuna walimu wengi wamesoma, wamemaliza course zao mbalimbali wanasubiri ajira. Kuna eneo la afya wanasubiri ajira, kuna wataalam wa kilimo, bila kusahau majeshi yetu yote vijana wanasubiri ajira na bahati mbaya sana hawa watu wanaotarajia kuajiriwa hawataki kukaa vijijini, wanakuja kukaa mjini. Kwa hiyo tuna kundi kubwa la watu liko pale Dar es Salaam linatumia lakini halizalishi.

Mheshimiwa Waziri utanisaidia sana kama ukioanisha na hili la kupandisha madaraja watumishi wetu, kutoa increment kwa watumishi wetu, bajeti haisemi. Nimewahi kuzungumza na walimu, wafanyakazi wa afya wanalalamika kwamba sasa hivi increment hakuna, sasa hivi watu hawapandishwi madaraja, kwa hiyo Mheshimiwa waziri hili utakuwa umenisaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Waziri utanisaidia sana kama benki zetu zikiwa na fedha. Mikopo kwenye benki zetu za baishara, watu wa Dar es Salaam wengi wao wanaishi kwa kufanya biashara na wanakopa katika benki hizi za kibiashara, benki hizi ndogondogo mitaji yao ni midogo. Natambua kwamba Serikali imekopesha mpaka bilioni 500 lakini tunapenda ingekuwa ni vizuri tukafika angalau trilioni moja.

Natambua Serikali tumeshusha riba kutoka asilimia 16 mpaka asilimia 10, lakini mimi natamani kwa nini tusishushe mpaka asilimia tano kwa sababu hii mikopo inayokopwa na mabenki, ni mikopo ambayo risk yake ni ndogo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kama atayafanya haya atakuwa amenisaidia kwa kiwango fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atanisaidia sana mimi mtu wa Dar es Salaam kama atalipa madeni au madai. Bajeti inaonyesha mwaka jana baada ya kufanya uhakiki tulikuwa na madai yanayofika trilioni 1.9 na tukalipa bilioni 700 maana yake kuna pesa zimebaki kama trilioni 1.2. Mheshimiwa Waziri ukilipa hizi tena tumelipa deni la nje, takribani trilioni saba, sasa kama tunalipa deni la nje trilioni saba ni vizuri tukamaliza haya madai ya ndani kwa sababu haya madai ya Wakandarasi, madai ya Wazabuni, madai ya Bohari Kuu ya Madawa, madai ya watumishi, madai ya huduma mbalimbali haya yataleta mzunguko pale Dar es Saalam na wananchi wetu wataanza kuona nafuu ile unayoikusudia kuipeleka. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri ninasikitika sana, Dar es Salaam pale ninakabiliwa na hali ngumu, chakula kikipanda. Mwaka huu ndani ya kipindi kuanzia mwezi wa tatu mpaka tunakuja hapa mwezi wa sita iliwahi kufika kilo ya unga shilingi 2,400, na unga ndio chakula nafuu kwa watu wa Dar es Salaam, kwa sababu ugali hauchagui mboga. Sasa unapopanda unga maana yake mwananchi wa kawaida atapata hali ngumu, wamejitahidi kupunguza matumizi wameacha mambo yote yasiyokuwa ya lazima, lakini mtu hawezi kuacha kula. (Makofi)

Sasa Mheshimiwa Waziri utatusaidia sana ukiongeza hifadhi ya chakula na hasa mahindi ili inapofika kipindi kama hiki cha ukame hifadhi yetu ya chakula iwe inauzwa kwa bei nafuu kwa wafanyabiashara wetu ili bei ya vyakula isipande. Kwa sababu bei ya vyakula ikipanda kunasababisha hali ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wanapokuwa na njaa, wakati mwingine hawaoni umuhimu wa standard gauge. Mheshimiwa Rais anaweza akafanya mambo makubwa ya kujenga reli hayo, makubwa ya umeme na kuleta ndege lakini hivi mwananchi mwenye njaa atathamini vipi haya? Na kwa kweli kama tunataka kuleta mtengamano, kama tunataka wananchi wa kawaida waone Rais anachapa kazi lazima tutatue suala la njaa na kutatua suala la njaa ni kushusha bei ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ni kwa maana hiyo bei ya chakula lazima ishuke, lazima hifadhi yetu ya chakula itumike kama kiwango ambacho kitaenda ku-regulate pale ambapo mazao yanapokuwa hayapatikani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ya Halmashauri, kwenye mapato ya Halmashauri mimi nasikitika sana, kwa kweli wachangiaji wengine wanachangia lakini wengine sio wahusika wa moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua sisi watu wa Dar es Salaam ni wahusika wa moja kwa moja. Katika property tax, Kinondoni mwaka uliopita tulikusanya shilingi bilioni 7.8, baada ya Serikali kutukusanyia mwaka huu wametupa shilingi bilioni moja. Kuna hela zinapotea hapa jamani, wengine tunaposema kwamba tunataka kusaidia nchi yetu, inakuwaje tunapoteza mapato kama haya kwa sababu tu ya kugombania nani akusanye? Kwa nini basi Waziri kama anaona inafaa lazima hizi peza wakusanye wao, kwa nini katika haya Majiji hasa Jiji la Dar es Salaam kwa nini Halmashauri zisiwe kama agent, kwamba wao ndio wakusanye halafu wakukabidhi wewe ufanye unavyotaka? Si lazima zile pesa zote shilingi bilioni 7.8 tutumie sisi Kinondoni lakini roho inauma kwamba mnatoka kwenye mapato ya kukusanya shilingi bilioni 7.8 mnarudi mnapewa bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongeza kodi ya mabango ambayo nimemuuliza Mhasibu wangu ambaye nimempigia simu leo hii akaniambia ni shilingi bilioni tatu tumelenga. Sasa kwa kulenga shilingi bilioni tatu ninyi wenzetu mtaichukua mnaenda kuifanyia majaribio wakati hii kodi ya majengo hatujafika mbali, tunaongeza na kodi ya mabango tunaenda kupoteza shilingi bilioni tatu?

Mheshimiwa Waziri, fikiria kama vipi, Manispaa za Kinondoni kwa sababu nayo ni Serikali zikusaidie ili tusipoteze hizi fedha, kwa sababu tunaweza kupoteza fedha zaidi shilingi bilioni 30 kwa Dar es Salaam tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabadiliko ya sheria, nimesoma hapa katika kitabu cha Financial Bill hapa kuna mabadiliko ya sheria yanakuja, Sheria Na. 290…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)