Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Omary Ahmad Badwel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kunipa nafasi na niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali kwa mwaka unaokuja wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya toka amechaguliwa mwaka 2015 na sisi Wabunge tunamuunga mkono na tunaahidi kwamba tutaendelea kumuunga mkono ndani ya majimbo yetu lakini pia kama viongozi wa kitaifa ndani ya nchi yetu yote ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali pia kwa ujumla kwa masuala ya umeme ambayo sasa inaonekana REA III inakwenda vizuri na mimi Mbunge wa Bahi nilikuwa nikilalamika hapa kila wakati juu ya kukosa umeme, lakini naona mambo yangu safari hii shwari, kwa hiyo nashukuru sana Serikali kwa kuitambua na kuona Wilaya ya Bahi nayo inaweza kupata umeme tena kwa maana ya vijiji vyote Wilaya nzima, ahsante sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake wa kupunguza kodi mbalimbali na hususan zile ambazo zinawalenga wananchi wa chini ambao wamekuwa wakifanyia biashara mbalimbali hususani mazao, tunaipongeza sana Serikali na
hivi karibuni niliuliza swali pamoja na mazao mengine lakini pia nilizungumzia sana habari ya ubuyu na ukwaju, nilikuwa naomba pia Serikali itoe ufafanuzi sasa kwa sababu haya yanaonekana kama mazao ya misitu hivi huwenda yasiwe yanajumuishwa katika hili zoezi la upunguzaji wa ushuru mpaka tani moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi Bahi kule ukwaju na ubuyu ni sehemu ya mazao muhimu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kina mama na vijana ambao wamekuwa wakitafuta maisha. Kwa hiyo, ni vizuri ubuyu na ukwaju ukatangazwa hapa rasmi kwamba nao utaanzia tani moja kutozwa ushuru ili wale wananchi wenzetu wanaofanya kazi hii Bahi na ukizingatia Bahi ni Wilaya ya ukame ina vitu vichache sana hivyo ambavyo wananchi wanaweza kuvitumia kwa ajili ya maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa kuondoa hii tozo ya kodi ya magari kwa maana ya kodi za barabarani na kuamua kuipeleka kodi hiyo kwenye mafuta, uzuri wa jambo hili tu kwamba ingawa tutatozwa lakini we don’t feel kwamba kuna kitu tunachangia tofauti na wakati ule ukiambiwa kwamba lipia shilingi 300,000/400,000 unaguswa kuzikusanya hizo fedha lakini sasa kwa mtindo huu tumekuwa tulikipa pole pole bila kufikiri kwamba unalipa na hiyo tunaendeleza kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bahi ni eneo la ukamae na Wabunge wenzangu ni mashahidi safari hii ukitokea Morogoro tu ukifika pale Gairo ukianza tu, Mkoa wa Dodoma unaanza kukutana na ukame mkali, tofauti kabisa na wenzetu katika Wilaya zingine na mikoa mingine. Kwa hiyo, nilidhani kwamba kuna haja kubwa ya kuangalia Mkoa wa Dodoma huu katika suala la miundombinu ya umwagiliaji hususani Wilaya yangu ya Bahi. Wilaya ya Bahi ni ndiyo Wilaya kame zaidi kuliko zote katika Mkoa huu wa Dodoma, lakini Mungu ameijalia Wilaya Bahi ina ardhi kubwa ina mabonde mazuri, lakini tunakosa fursa ya miundombinu sahihi ya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bahi tuna skimu za umwagiliaji kumi, kati ya skimu hizi kumi kama zimekuwa zimeendelezwa vizuri na zinafanya kazi vizuri zingechangia kwanza wananchi wenyewe kupata chakula cha kutosha katika eneo la Wilaya ya Bahi. Lakini pia kwakuwa hapa Dodoma sasa ni Makao Makuu na watu wengi wanahamia tungeweza pia kupata vyakula mbalimbali hapa jirani kuliko kutoa vyakula mbali kutokana na hali halisi ya ukame wa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwahiyo naiomba sana Serikali embu ipitie upya ile miradi kumi ya umwagiliaji iliyopo Bahi, maana mingine ama imechakaa na ni ya muda mrefu, lakini mingine ilijengwa ikaishia nusu haikukamilika, haifanyi kazi, mingine ilianza hata robo haijafika na fedha nyingi zimepotea na zile fedha hazifanyi kazi yoyote, nilikuwa naomba sana Wizara husika waje Bahi wapitie miradi yetu yote hii kumi waone namna ambavyo watawasaidia wananchi wa Bahi kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili hali ile ya sisi kuomba chakula kila mwaka ipungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo na tathimini ifanyike ili wananchi wa Bahi waweze kupatiwa chakula hata kama ni cha bei nafuu kwa sababu hali kwa kweli ni mbaya sana sio sisi tu kama wananchi, lakini hata mifugo kwa sababu mvua haikunyesha vizuri pia hata hali yetu ya mifugo itakuwa ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la viwanda Mheshimiwa Waziri sisi Bahi ndiyo Wilaya tunaongoza kwakuwa na ng’ombe nyingi katika mkoa huu wa Dodoma, lakini hatuna hata viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa nyama ambavyo vingesaidia sana wananchi wale mifugo yao ambayo wanaifuga ingeweza kuleta tija zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri huwa nakusihi hapa namna unavyo waahidi Wabunge viwanda na mimi Bahi nahitaji kiwanda cha usindikaji nyama, ninakuomba sana tushirikiane tuweze kupata kiwanda hicho ili wananchi waweze kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji, Bahi kama nilivyosema ni Wilaya kame na mji wa Bahi ule ulikuwa ni kijiji tume u-promote mpaka umekuwa mji kwa sababu ile ni Wilaya mpya lakini tumekuwa na shida ya muda mrefu sana ya maji katika mji wa Bahi. Nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri miradi ambayo tumeomba ya Bahi kwa miaka saba sasa wa maji pale Bahi mjini hatujapatiwa fedha, kwahiyo siku moja na sisi bajeti ioneshe kwamba Bahi mji ule unakwenda kupewa maji ya kutosha ili wananchi waweze kujenga kitu ambacho kimewashinda sasa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia miradi hii ya maji imekuwa na gharama kubwa mno, nataka niishauri Serikali inawezekana ninao ushahidi kwamba miradi hii ya maji imekuwa ikiongezewa fedha nyingi sana na wataalam wetu sio waaminifu, wamekuwa wakiongeza fedha hizi za miradi ya maji na inakuwa fedha nyingi kiasi kwamba tunashindwa kutekeleza miradi mingi katika vijiji vyetu na nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu iangaliwe kama tunauwezo leo wa kusema barabara ya kilometa moja inatengenezwa kwa bilioni 1.2, tunauweza kusema leo umeme ukisambazwa katika kijiji kilometa kumi utalipwa kiasi fulani, lakini pia tunaweza kufika mahali tukasema kwamba maji yakisambazwa katika kijiji kwa kilometa tatu au nne yatakuwa na gharama kiasi fulani hata kama mazingira yatakuwa tofauti kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa hali hii ambayo tunakwenda nayo siyo rahisi sana kutekeleza hii miradi ya maji, unaambiwa kila mradi ukigusa unaambiwa ule ili ukamilike unataka milioni 700; ili ukamilike unataka milioni 600, lakini wanakuwa watu binafsi wanachimba visima wanasambaza maji wanauza ukimuuliza umetumia milioni ngapi wanasema nimetumia milioni 30, lakini Serikali hakuna milioni 30 ni milioni 200; milioni 300; milioni 400 kitu ambacho kimekuwa ni kikwazo kikubwa. Nadhani kuna haja ya kuipia wataalam wetu hawa waelekezwe vizuri na kupitia kuona gharama za miradi ya maji zinakuwa kwenye standard kama miradi ya barabara. miradi ya umeme na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeiacha miradi ya maji wanabuni wenyewe tu kutokana na hali halisi kwahiyo katika ubunifu huo wako wataalamu ambao wamekuwa sio waaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Dodoma tunao punda, tulinde hawa punda kule vijijini wananchi wengi hawana uwezo wa kusafirisha mazao kwenye magari, pikipiki na na kadhalika wanatumia punda leo tukimaanisha kiwanda hapa kila siku punda wanakwenda na punda ndio wanyama nadhani hapa Dodoma wanaozaliana kwa uchache sana, lakini wanyama wenye msaada mkubwa sana, nadhani Serikali iangalie namna ya kuwalinda hawa punda kwa sababu la sivyo hawa punda watapotea latika Mkoa wa Dodoma, Mkoa wa Singida na maeneo ya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli unafika pale mpaka punda wale unawaonea huruma, kwa sababu punda ni rafiki zetu wazuri, wamekuwa wakitusaidia miaka mingi kwenye mashamba yetu mizigo yetu mbalimbali, lakini leo tunaagalia na wengi tunapita hapo tunaona na nimesikia kile kiwanda kimefungwa sina hakika. Nilikuwa naomba jambo hili liwekewe mkazo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba punda wanalindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie tu kwa kuunga mkono hoja hii, namtakia kila la heri Mheshimiwa Waziri hotuba yake hii ipite salama na baadaye kazi ya maendeleo iweze kuendelea kwenye nchi, ahsante sana.