Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kutoa maoni yangu kuhusiana na hotuba ya Mheshimiwa ambayo imeletwa kwa ajili ya mapendekezo ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nitoe pole kwa ndugu zetu walemavu waliopata rapture pale Dar es Salaam, ni sawa inawezekana ni katika kutekeleza sheria, lakini ni vema sasa hata utekelezaji wa hizi sheria tukaangalia ni namna gani, nimuombe Mheshimiwa, ndugu yangu, dada yangu Mheshimiwa Jenista, dada ambaye unasikiliza na unasimamia masuala haya hasa mambo ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu nina kuamini utalishughulikia suala hili kwa kushirikiana na mamlaka husika ili tuweze kuona ni namna gani wale walemavu wameweza kutendewa ndivyo sivyo, kwa kweli si jambo jema kwa kupiga walemavu hata kama tunatekeleza sheria. (Makofi)

Kwa hiyo nikuombe ndugu yangu kwa umahiri wako dada yangu Jenista ulionao ninaamini suala hili utalishughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vilevile masuala yaliyotokea Tabora kwenye michezo tunasema michezo inadumisha amani, upendo, utulivu. Wamecheza kule pamoja na Jeshi la Wananchi sasa sielewi matokeo yalikuwaje, matokeo yake MP’s wakaingia uwanjani na kuanza kupiga wachezaji na wananchi, hilo nalo naomba Waziri anayehusika alishughulikie hili tujue sasa nini maana ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naomba nipongeze sasa bajeti hii iliyoko hapa mbele yetu inayopendekezwa. Bajeti hii kwa kweli imeweza kulenga maeneo mbalimbali na lengo lake kubwa tunaona ilikuwa ni kupunguza kodi ili kuweza kuwasaidia wananchi kufikia uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imeweza kutoa misamaha mingi ya kodi ambazo nyingi zilikuwa ni kama kero kwa wananchi, kwa mfano naweza kusema katika jimbo langu la Kavuu kata ya Majimoto na kata ya Usevya wamekuwa wakilalamikia sana kodi ya majengo, kodi ya guest house, kwa kweli kuwaondolea kule kutawawezesha na wao angalau kusonga mbele, kwa sababu kule sisi tunategemea siku za mnada tu, kwa hiyo hata tulivyokuwa tukitoa zile kodi kwa kweli ilikuwa inawaumiza wananchi na wako huko najua wananisikia, mitandao iko mingi tu wananisikia wanajua nawakilisha mawazo yao hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lakini naomba niende katika suala zima ambalo limekuwa likiongelewa la shilingi 40. Katika hii shilingi 40 tunaelewa lengo ni jema na ni zuri kwa Serikali, lakini ukiangalia kwa ndani hii pesa imeongezwa kwenye mafuta, bidhaa za mafuta ikiwemo na mafuta ya taa. Bidhaa hizi za mafuta ya taa na wananchi wetu vijijini hasa katika jimbo langu ambalo halina umeme, wanatumia mafuta ya taa kwa maana kwamba watachangia hii shilingi 40, sasa kwa msingi huo huo wa wao kuchangia hii shilingi 40 nimuombe Mheshimiwa Waziri usiwe na kigugumizi kwa kuitoa hii shilingi 40 katika ku-cover deni la Serikali la shilingi milioni 28 hii shilingi 40 ipeleke kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lazima iende kwenye maji, usiwe na kigugumizi Mheshimiwa Waziri katika hili kwa kweli ukifanya hivyo ndipo utakapokuwa bajeti yako sasa umeinogesha ipasavyo, pale tutakapoweza kuiweka hii pesa kwenye maji kwa sababu lengo lako ni kukusanya hii shilingi milioni 28 ili iende ika-cover lile deni lenu Hazina, sawa hatukatai ni pesa ya maendeleo, sasa tutakaposema kwamba ile shilingi 40 isiende kwenye maji vyanzo wewe vya kupata hii milioni 28; unayo shilingi bilioni 28 unavyo vyanzo? Itafute kwenye vyanzo vingine na hii shilingi 40 uliyoongeza kwenye bidhaa za mafuta ambazo wote itatugusa mpaka wananchi wa kijijini iende kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine namba niongee kuhusu ahadi ya shilingi milioni 50, katika hotuba ya Kambi ya Upinzani ukurasa sita wameongelea ahadi ya milioni 50. Ahadi hii ni ahadi ya Chama cha Mapinduzi, tumuache Mheshimiwa aliyepita kila kijiji kuomba kura na kuitoa ahadi hii haitekeleze, tukianza kudandia gari kwa mbele, tutapata kugongwa. Muachieni Mheshimiwa aitekeleze ahadi yake, maana yake imeshakuwa ni nini tumeshapewa maelekezo hapa na Serikali namna gani pesa hii itatoka lakini nashangaa kwenye ukurasa wa sita ndio ajenda kuu ya bajeti ya ndugu zangu pale, tuachieni tuka-organize wananchi wajiunge waweze kupata pesa hizi kwa utaratibu maalum na msiseme ni ajenda yenu, maana kazi yenu kudandia mbele magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kodi ya majengo tumesema itaanza kwa shilingi 10,000 nyumba za kawaida na shilingi 50,000 kwa ghorofa, nikuombe Mheshimiwa Waziri katika hili utunyumbulishie ni nyumba gani italipa shilingi 10,000 ni ghorofa gani italipa shilingi 50,000. Maana ukiniambia nyumba kwangu jamani nina tembe, sasa yule mwenye tembe kadi ya bima tu ile ya CHF hana, leo ukamwambie atoe shilingi 10,000 inawezekana? Sasa utuambie ni nyumba ya aina gani itakayoanzia shilingi 10,000 na ni nyumba gani itakayoanzia shilingi 50,000 . (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake huwezi kuniambia ghorofa kama lile LAPF pale ama Kilimanjaro Hotel itafanana na nyumba ya kuishi ya mtu mwenye ghorofa moja ama huwezi kuniambia nyumba ya vyumba viwili vya kulala hapo ukifika Mwitikila hapo itafanana na nyumba ya vyumba vitano self ya kulala.

Kwa hiyo, naomba mtuambie vigezo. Maana utakapoweka hivi wale ndugu zangu watoza ushuru na watoza kodi wao wataenda kutoza kama lilivyo hawataweza kusema huyu anafaa, huyu hafai, wao wataenda kutoza kama mlivyolielekeza na wengine wanaweza kusema kwamba sasa nyumba yangu ghorofa saba silipi, tumeambiwa ya ghorofa ni shilingi shilingi 50,000. Sasa lazima mueleze hapo kwamba ni nini mnakusudia katika kupata haya majengo na haya majengo yako kivipi? Huwezi ukaenda mtu mwenye nyumba sita ukamwambia akalipa shilingi 10,000 sawa na yule mwenye nyumba ya chumba kimoja ambacho labda ni chumba, sebule na choo haiwezekani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja na ninaungana na Waheshimiwa wote na wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.