Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri. Kwanza kabisa naomba nimpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa, kazi ya uzalendo, kazi ya kujitoa na kuhakikisha anatetea maslahi ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu kuwakumbusha Wabunge tukumbuke nyuma tulikotoka, Tanzania haikuwa kama hivi ilivyo leo. Wako watu walioumia, wako watu waliopoteza nafasi na wako watu waliopoteza muda wao kulitumikia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabisa naomba niwapongeze viongozi wote waliotangulia kwa kazi kubwa sana waliyoifanya. Ndiyo maana mpaka leo Chama cha Mapinduzi kiko madarakani kwa sababu naamini kila baada ya miaka kumi tunabadilisha uongozi na bahati nzuri Chama cha Mapinduzi kinashika nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake yote kwa ujumla inafanya kazi kubwa na ninaamini kabisa tunakwenda mpaka mwaka 2025 amalize muda wake yaani miaka kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuwa msikivu. Mwaka jana ni miongoni mwa watu niliochangia bajeti hii ya Wizara ya Fedha. Lakini kwa bahati mbaya wako baadhi ya Mawaziri waliniomba mwongozo kuhusiana na jambo la VAT on transit goods. Lakini leo nimeona wakishangilia. Hili nilitaka niliweke sawa tu kwamba ni vizuri na sisi ambao hatuna Ph.D tunapokuwa tunachangia, mnatusikiliza. Sisi wengine tunafanya biashara, sisi wengine tumezaliwa humo humo kwenye biashara, kwa hiyo, tuna baadhi ya mambo tunayajua muwe mnatusikiliza na tuna Ph.D za mitaani. Sasa Mheshimiwa Waziri nataka niombe sana pale ambapo sisi tunataka kuchangia basi yale mambo ya msingi muweze kuyachukua na kuweza kuyafanyia kazi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la VAT on transit goods tulilipigia kelele sana lakini mmelichukua mwaka huu mmeliondoa. Ninavyoona kwa bahati mbaya sana, mmeliondoa mmewekea kipengele cha wiki moja. Baada ya wiki moja mnawachaji tena VAT kwa mzigo unaokwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka turekebishe, turekebishe jumla! Nataka kushauri tu, Mheshimiwa Waziri, basi at least wekeni hata siku 30 kwa sababu kwa wiki moja kwa Bandari yetu ya Dar es Salaam na TRA yetu ya Dar es Salaam kila siku system iko down. Wiki moja itapita na matokeo yake tutawa-charge tena upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukuomba sana Mheshimiwa Waziri hili uliangalie, kesho unapokuja hapa basi uje utueleze nikuombe sana kama unataka kurekebisha jambo tulirekebishe moja kwa moja kwa sababu leo hii tumepoteza wateja wengi sana. Wateja wengi wamekimbilia Msumbiji kule Beira, wengine wamekimbilia nchi nyingine. Sasa tunapoanza utaratibu wa kutaka kuwarudisha wateja hawa basi tuhakikishe tunawawekea masuala yote ya msingi vizuri. Mfano, VAT tuiondoe, iwekeni mwezi mmoja, nafikiri kabisa hawa watu watarudi na biashara itaweza kuongoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutoa road license, kusamehe hii tozo ya road license, lakini tumechukua shilingi 40 tumeipeleka kwenye mafuta, naunga mkono hoja ya kuweka shilingi 40 katika kila lita, lengo letu ni maendeleo. Lakini toka uhuru tunalia suala la maji, ni wimbo wa Taifa kila siku maji, maji, maji. Kwa nini sasa shilingi 40 hizi tusizichukue tukaziwekea mfuko maalum wa maji vijijini. Tuitengee kabisa, tuiwekee kabisa ring fence pale kwamba hili hizi pesa tunazozipata ziende kwenye maji vijijini.

Mheshimiwa Waziri, kero ya maji bado ni kubwa na magonjwa yanayosababishwa na maji bado ni makubwa. Niombe sana suala hili tuliweke kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine siungi mkono kwa baadhi ya Wabunge wanaosema tuongeze shilingi 50 kwenye mafuta. Unajua ni rahisi kusema tuongeze na ninavyoona sasa itakuwa kila kitu unaongeza kwenye mafuta, tutafute vyanzo vingine ili tuweze kupata fedha za kuweza kutimiza bajeti yetu. Naunga mkono shilingi 40 lakini siungi mkono shilingi 50 kuongezwa kwenye mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yalikuwa mengi sana ambayo nilitaka kuongelea ni jambo hilo. Lakini la tatu nataka kuongelea uwanja wa ndege wa Sumbawanga. Kwenye bajeti ya mwaka jana tulipitisha bajeti ya uwanja wa ndege ujengwe wa kiwango cha lami, tumekuwa tukipigania sana. Lakini kubwa ambalo ninaliona sasa hivi ambalo nalipigania ni kwamba wale watu ambao wanatakiwa walipe fidia ambao wanazunguka uwanja wa ndege gharama za ujenzi zimezidi, ninaomba wafikiriwe upya ili waweze kufanyiwa uhakiki kwa gharama ya sasa. Na niipongeze kabisa bajeti yako, lakini nimpongeze kabisa kwa kujenga uwanja wa ndege sio uwanja wa ndege peke yake Sumbawanga lakini viwanja vingine vyote ambavyo vinajengwa kwa sababu ninaamini kila kwenye uwanja wa ndege maendeleo yatakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuliongelea, nataka niulize tu hivi shisha Mheshimiwa Waziri wa Fedha uko hapa na Waziri wa Mambo ya Ndani yuko hapa. Shisha hii ni haramu? Shisha hii ni madawa ya kulevya? Na kama ni madawa ya kulevya kwanini TRA mnakusanya kodi? Kwa nini ile tumbaku inapofika bandarini mnai-charge kodi? Na kama ni madawa ya kulevya, Waziri Ummy yuko hapa naye atujibu na kama ni madawa ya kulevya au shisha inatumika vibaya, hata sigara inatumika vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sigara watu wanaweka bangi mule, sigara unaweza ukaweka kitu chochote kile. Ni kazi ya polisi kuhakikisha ile shisha haitumiki vibaya lakini sasa leo tunaipiga marufuku, anatoka mtu tu huko sijui kagombana na mke wake au na mpenzi wake anakuja kusema shisha marufuku na hiyo marufuku ya shisha iko Dar es Salaam peke yake! Ukienda Arusha wanavuta shisha ukienda Dodoma hapa wanavuta shisha, ukienda sehemu nyingine wanavuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niombe Mheshimiwa Waziri kama shisha hii ni madawa ya kulevya tuipige marufuku leo na kwenye kodi tuiondoke maana kwenye kodi imo, ukiwauliza wale jamaa wa TFDA wanasema haina madhara. Ukimuuliza yule Mkemia Mkuu anakwambia haina madhara, lakini ukija huku wanakuambia hii inatumika na madawa ya kulevya. Ni wajibu wa polisi, ni wajibu wa kila raia akiona kama kuna mtu anatumia madawa yale au anatumia shisha vibaya akamatwe. Lakini ukienda nchi za kiarabu wanavuta, ukienda Uingereza wanavuta, ukienda dunia nzima kasoro Dar es Salaam. Nataka niseme, liangalieni tusiwaumize wananchi, wako watu wanalipia kodi Dar es Salaam lakini ikitoka inapigwa marufuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuongelea jambo la mwisho, ni suala la Bodi ya SELF. Bodi hii mwaka jana iliahidi kutoa mikopo ya shilingi bilioni 12 lakini hatimaye mwaka jana walitoa shilingi bilioni tisa. Mwaka huu walipanga shilingi bilioni saba kuweza kuwakopesha wafanyabiashara/taasisi kubwa. Lakini kwenye bajeti hii tumepanga shilingi bilioni 20 mwakani lakini bodi hii imevunjwa, haipo. Sasa hizi fedha zote tunazozipanga jamani tunangoja nini? Bodi hii imevunjwa leo ina mwaka mzima. Hebu jaribu kuangalia kama kuna jambo ambalo lingetakiwa kufanyika kwa haraka, lifanyike kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja.