Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Rashid Ali Abdallah

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wako mwingi wa Bunge hili umetumika zaidi kwa kujadili makinikia, na zaidi ya hilo umekwenda mbali zaidi kwa kuwataja Mawaziri ambao walifuatia, kuwataja wanasheria ambao walipita. Kufanya kitendo hiki cha kuwataja Mawaziri au wanasheria waliopita kisheria hasa sio sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameteua Kamati yake, na ameelekeza nini cha kufanya muache Rais afanye shughuli zake, sisi tujadili hotuba ya Bunge ambayo ni bajeti. Cha msingi ni kuhakikisha kwamba sheria zote za madini, maliasili na sehemu nyingine zote zinafumuliwa upya na kufanywa vizuri na kupitiwa mikataba mbalimbali ili tujue tunaanza wapi katika kuleta uchumi huu wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo niseme kwamba bajeti ni mpango maalum wa kupanga mfumo ule wa mapato na hatimaye kuweka matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha msingi baada ya kukusanya ni matumizi, Mheshimiwa Waziri nitamnukuu katika ukurasa wake wa 14 anasema ifuatavyo; “Nidhamu ya hali ya juu katika matumizi lazima isimamiwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha tathmini ya fedha inapatikana” lakini pia aliendelea; “kutokufanya matumizi pasipokuwa na kasma iliyoidhinishwa kwenye bajeti husika katika fungu husika.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hapa amesisitiza nidhamu ya matumizi, mwaka jana tulikusanya 70.1% lakini Wizara zote zinalalamika hazina fedha za maendeleo, sasa fedha hii imetumika wapi, je, Waziri amekuja kutuambia kuna tatizo wapi, kwa nini Wizara zisipate hela za kutosha, kwa mfano, Wizara ya Kilimo 3.8%; Chuo Kikuu Dar es Salaam 0%; Wizara ya Maji 8%. Katika mwendo huu ni dhahiri kwamba kulikuwa hakuna nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali. Na nasema kwamba nidhamu lazima ianze juu ije chini, nidhamu ikianza chini isiende juu haina maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kwamba matumizi yaliyofanywa kwa mji kuhamia Dodoma ilikuwa budgeted, sifikirii kama hii ilipita katika bajeti. Na hii ndio iliyotikisa bajeti hii kufikia Wizara zote hazina fedha, kwa hiyo, nidhamu ni lazima ijengwe kutoka juu kwanza, halafu chini ifuate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la utekelezaji wa bajeti. Kuna kasoro kubwa, bajeti mara hii ya maendeleo ilitekelezwa kwa 35% mpaka 40% na nchi haihesabiwi kama ina maendeleo mpaka itekeleze miradi ya maendeleo. Lakini OC 80% na maendeleo 35% mpaka 40%, Wizara haijatuambia ni kwa nini bajeti hii hata masuala ya maendeleo hayakupita vizuri, hawajatueleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika vipaumbele. Mheshimiwa Rais ailipohutubia hapa alisema atahakikisha anafuata maelekezo yote ambayo viongozi wengine walipita, ni vizuri ninukuu anasema katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja mwaka 2015 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza Watanzania kwamba; “vipaumbele vya Serikali kuhusu uchumi ni kuendeleza na kuimairsha misingi imara ya uchumi wa nchi iliyojengwa katika awamu ya uongozi uliotangulia.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bado nina wasiwasi Serikali hii ya Awamu ya Tano imetoa kipaumbele zaidi na msukumu mkubwa zaidi kwenye viwanda lakini msukumo mdogo kuja kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kinaongeza pato hasa mifugo 4.4% na nasema kwa mfano FAO ilifanya utafiti na ikesama kwamba kama Mtanzania atakula nyama kilo 11 kwa mwaka ambapo kwa mwezi ni kilo moja au atakunywa maziwa lita 45 kwa mwaka ambapo kwa mwezi ni lita nne, au atakula mayai 72 kwa mwaka ambapo kwa mwezi ni mayai sita basi tutakusanya shilingi trilioni 20. Hii ni sehemu ndogo tu, lakini pia Misri na Zambia ilitaka kununua nyama Tanzania tani 50,000. Lakini Tanzania ilikuwa inazalisha tani 23,000, nchi ziko tayari kununua tani 50,000 sisi tuna tani 23,000, ng’ombe wanakufa, mifugo wanapigana na watu huko, nini soko la wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inapoteza fedha hizi. Sasa ninasema wakulima elimu yao ni kilimo, maskini matibabu yao ni kilimo, maskini afya zao ni kilimo, leo Wizara haijapewa kipaumbele na Wizara hii ya kilimo. Tumepewa kipaumbele viwanda, viwanda hatujajua changamoto zipi, kilimo tumezoea changamoto zake, mwaka 2015/2016 awamu iliyopita Rais Kikwete alitoa pembejeo zenye thamani ya shilingi bilioni 78, lakini Mheshimiwa Magufuli kipindi cha mwaka 2016/2017 alitoa pembejeo shilingi bilioni 10, kutoka shilingi bilioni 78 mpaka shilingi bilioni 10 hii maana yake nini? Maana yake nyingine kwamba hana habari na kilimo, 65% ni kilimo, hii sekta kubwa ambayo inaajiri Watanzania, ni sekta ambayo sasa tunaipa mgongo tunakwenda kwenye viwanda hatujui changamoto zake zikoje. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri ni lazima ukitaka tusitake kilimo ndio asili yetu, wewe hukuwa na profesa umekwenda kwenye kilimo, watu wote waliosoma hapa wamesomeshwa na kilimo, leo kilimo unatoa shilingi bilioni 10. Kwa hiyo hii kilimo sio mvua tu, kilimo mvua na pembejeo, pamoja na dawa za kilimo ili kuimaisha kilimo kiwe viruzi zaidi na kilimo cha biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii haiwezekani kabisa kuvumilika ni lazima tubadilishe mwelekeo turudi kwenye kilimo kwanza.