Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nampongeza sana yeye, Naibu wake, Katibu Mkuu, timu ya wataalam na wote walioshiriki katika kupanga jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nataka kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwamba Serikali imejipanga vizuri sana katika kuondoa kero hasa za uwekezaji kwa sababu tunajua uwekezaji wote unaanza kwenye msingi wa ardhi. Baadhi ya uwekezaji mkubwa ambao tunautarajia kama wa LNG Wabunge wamezungumza, nataka kuwahakikishia kwamba wizara yangu imeshatoa hati ya eneo lote kwa TPDC, hakuna tatizo la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika eneo la uwekezaji wa bomba la mafuta kutoka Uganda, nataka kuwahakikishia kwamba Wizara yangu kwa kushirikiana na wabia tumeshapiga picha ya anga ya upana wa mita 200 katika eneo lote la mpaka. Kwa hiyo, najua kuna speculators ambao wameshaanza kupanda miti na vibanda humo, picha tunazo; hamtapata fidia watu ambao mnaweka weka katika maeneo hayo kwa sababu tumeshapiga picha za anga na kazi inaendelea katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumejianda kabisa kuondoa kero katika eneo la ardhi ili kuhakikisha wawekezaji wa ndani na nje wanawekeza wa ndani na nje wanawekeza na Watanzania wanapata unafuu katika kumiliki ardhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka huu wa fedha tutapanga master plan katika miji 30, tumeshaanza. Master plan ambazo zitaelekeza maeneo mbalimbali ya uwekezaji pamoja na hao wamachinga ambao wanasajiliwa, master plan hizi lazima zielekeze maeneo ya kufanya biashara. Wizara yangu haitasaini master plan yoyote ambayo haitaelekeza maeneo ya kufanya biashara hasa za watu wadogo wadogo katika miji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, katika umilikaji wa ardhi, EPZ tumewapa maeneo makubwa, lakini sheria tumetunga mwaka huu EPZ na TIC tumewapa jukumu lingine la kutoa hati. Zamani ilikuwa wawekezaji wanapewa hati na Wizara ya Ardhi. Kwa hiyo, EPZ na TIC sasa wanatoa wenyewe derivative right ili kupunguza urasimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika umilikaji wa Watanzania na wageni, uwekezaji na ujenzi wa Mipango Miji, jambo moja lililokuwa linawakwaza Watanzania ni gharama ya umilikaji wa ardhi. Mwaka huu pekee tumeamua kama Serikali kuondoa asilimia 67 ya tozo kubwa ambayo ilikuwa inawakwaza sana watanzania na wawekezaji katika katika umilikaji wa ardhi inaitwa premium. Kwa hiyo, fikiria kama wewe ulikuwa unatakiwa kulipa shilingi milioni 100 sasa kuanzia tarehe moja mwezi wa saba utalipa milioni 33. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali imeamua hivi ili kuwapa nafuu watu wengi zaidi waweze kumiliki ardhi na Serikali kila mwaka iendelee kupata kodi. Kwa hiyo, tumefanya makubwa sana katika kuhakikisha kwamba tunarahisisha suala zima la uwekezaji ili kuhakikisha kwamba kila mwananchi anamiliki ardhi bila kikwazo kikubwa.

Mheshimiwa Spika, hapa Dodoma ilikuwa ni eneo pekee ambalo wawekezaji wa nje hawawezi kufika kwa sababu ya mkanganyiko wa umilikaji wa ardhi. Mheshimiwa Rais aliagiza na utekelezaji umenza, imefutwa CDA na sasa watu wote wanaomiliki ardhi Dodoma wataanza kupata title deed kama wananchi wengine katika maeneo mengine ya Tanzania, na watapata title deed zenye miaka 99.

Mheshimiwa Spika, wale wote waliokuwa wanapata lease tumeanza utaratibu wa kubadilisha ili waweze kupata title deed za miaka 99. Walikuwa wanapata lease za miaka 33 lakini sasa tutawaongeza kila mwenye hati ataongezewa miaka 66 na kwa agizo la Mheshimiwa Rais kwamba hawa watu wote wabadilishiwe hati bila kuongezwa gharama yoyote, bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kila mmoja sasa mwenye lease aliyekuwa na hati Dodoma ni fursa aende Manispaa ili aweze kupata title deed ya miaka 99. Maana yake ni nini? Ukipata title deed sasa TIC wanaweza kumpa derivative right yule mwekezaji ambaye utampata kutoka nje ambaye anaweza akaingia ubia na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaendelea na jitihada za kufanya audit, tunajua katika kupanga mipango hii ya uwekezaji, wako matapeli wanaingia wana-take advantage kuchukua ardhi ya Tanzania kwa ajili ya kujipatia mitaji au kuhamisha mitaji, wanatumia ardhi yetu kufanya mortgage na kuhamisha pesa. Kwa hiyo, tunafanya audit kuwatambua wale wote ambao wamemiliki ardhi. Kwanza hawana sifa, wengine si raia, lakini wale ambao wamemiliki ardhi kubwa na bila kuziendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita Mheshimiwa Rais amefuta mashamba yenye ekari zaidi ya elfu ishirini Mkoa wa Morogoro, na katika kipindi cha mwaka huu mmoja na nusu Mheshimiwa Rais ameshafuta mashamba yenye ekari zaidi ya 100,000 katika nchi hii, na mashamba haya yanapangwa ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wa wawekezaji walio mahiri wanamilikishwa kwa kufuata sheria. Tunajua wapo watu wamemiliki hata maeneo ya madini kwa sura za Tanzania na hati za Kitanzania.

Vilevile wapo wenzetu wengine wana hati mbili mbili za kusafiria, kwa maana wana uraia wa nchi mbili. Tunafanya uhakiki na wale wote ambao watagundulika wana hati mbili mbili lakini wamemiliki ardhi ya Tanzania tutanyang’anya kama ambavyo tumeshawanyang’anya watu wengine. Ule wakati wa longo longo umekwisha sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kila mmoja anayetaka kumiliki ardhi atapewa na nataka kukuhakikishia Mheshimiwa Spika kwamba Serikali tumejipanga, tumerahisisha sana utaratibu na tumeondoa kero nyingi sana katika ardhi, umilikaji umekuwa smooth. Zamani ilikuwa ili uweze kupata hati unasubiri mwaka mmoja, leo maximum ni mwezi mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha mwaka mmoja tumejipanga twende katika lengo la wiki moja, na kutokana na mfumo tuliouanza kuufunga Dar es Salaam, tumeshaanza kufanya scanning ya document mbalimbali katika Wilaya ya Kinondoni na Ubungo; kwa Dar es Salaam
tutaanza kufikia lengo hilo la wiki moja mwakani. Tukifunga mitambo hii Nchi nzima, tunaweza kufika mpaka siku mbili. Vile vile Ulipaji wa kodi mwakani tutaanza kutumia mtandao; tutalipa kodi kwa kutumia mtandao wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie kwamba jitihada zinazofanywa na Mheshimiwa Rais lazima na sisi Wizara mbalimbali kama Wizara yangu ya Ardhi, tumuuunge mkono kwa kufanya yale yanayotuhusu ndani ya wizara yetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.