Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika, kwanza kabisa nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Hoja ya Bajeti ya Serikali iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kwa kusema tu kwamba naunga mkono hoja na baada ya kuunga mkono hoja niseme pia kwamba bajeti hii imeitendea haki sana sekta ya kilimo nchini. Ninaposema sekta ya kilimo ni kwa maana ya sekta ya kilimo, mazao, mifugo na uvuvi na pia sekta ya ushirika hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tozo, pamoja na kwamba wako walioonekana kama hawaridhiki na ufutaji wa tozo na kodi mbalimbali katika kilimo, lakini sisi tunaovaa kiatu ndio tunajua kilikuwa kinatubana kiasi gani, na kwa maana hiyo tunatarajia kwamba tozo na kodi mbalimbali ambazo zimeondolewa zitaongeza tija katika kilimo, lakini pia zitaweka mazingira mazuri ya wadau wote wa kilimo ku- participate (kushiriki) bila kukwazwa na mazingira hayo ya kodi na ushuru mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, wakulima wamekuwa wakilalamikia tozo hizo na wafanyabiashara na watu wengine katika minyororo ya thamani na wao pia wamekuwa wanalalamikia tozo hizo. Kwa hiyo, tumeziondoa na Serikali imekubali kuziondoa na kuzifuta baadhi yake, nyingine kuzipunguza ili kuhakikisha kwamba wote wananufaika, win-win situation; Serikali ibakie na mambo yake ikinufaika lakini na wananchi pia wapate nafuu na kunufaika na jitihada wanazofanya katika mashamba na maeneo mengine ya uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba baada ya hayo tutaona mabadiliko ya bei ya mazao yetu ya biashara, lakini pia tutaona uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka, tutaona ufugaji ukipata nafuu zaidi baada ya kuondoa kodi hizi na tumeweka mazingira yanayovutia uwekezaji sasa katika mifugo. Eneo hili limekuwa halipati uwekezaji mzuri kwa sababu ya tozo na ada mbalimbali zilizokuwepo.

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba tunaendelea kama Wizara na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba upatikanaji wa pembejeo unakuwa kwa wakati na kwa bei ambayo wakulima wanaweza kumudu. Hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo zilizokuwako katika uingizaji na usambazaji wa mbolea na viuatilifu. Vilevile tunaendelea na mchakato wa uagizaji wa baadhi ya mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba mwishowe bei tutakayoiweka itakuwa inahimilika, wananchi wanaweza kuimudu na kwa hivyo ituwezeshe kuongeza uzalishaji katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, Programu ya Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) imekamilika maandalizi yake na tumefanya mambo kadhaa. Pamoja na mambo tuliyoyafanya ni kutoa Mwongozo wa Kilimo, pia Mwongozo wa Ufugaji.

Mheshimiwa Spika, katika programu hii suala la umwagiliaji limepewa kipaumbele, na safari hii umwagiliaji tunaoufikiria kuuwekea msisitizo mkubwa ni umwagiliaji wa mazao makuu ya chakula. Kwa muda mrefu umwagiliaji umekuwa katika maeneo ya mpunga na mbogamboga, lakini sasa katika awamu hii ya Programu ya Kilimo ya Pili tunataka kwenda kwenye zao kubwa la chakula nchini ambalo ni mahindi. Umwagiliaji ufanyike pia katika uzalishaji wa mahindi ili kujihakikishia usalama wa chakula na uzalishaji wa muda wote ambao hautuletei mashaka.

Mheshimiwa Spika, niombe kutumia nafasi hii kuwatangazia wananchi kwamba sasa hivi maeneo mengi nchini wanavuna, lakini niwaombe sana baada ya kufanya mavuno hayo utumiaji wa chakula chao uwe wa makini kwa sababu hali ya hewa katika nchi zinazotuzunguka haikuwa nzuri na kwa hiyo, kutakuwa na mahitaji makubwa ya kununua chakula kutoka Tanzania kwenda nchi za nje.

Wananchi hawazuiliwi kuuza lakini wanashauriwa wauze na kujiwekea akiba ya kuwatosha.

Mheshimiwa Spika, narudia kusema naunga mkono hoja.