Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo walizichangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kipekee nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuweza kujibu hoja hizo kama nilivyoeleza awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kipekee kuchukua nafasi hii kumshukuru sana kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake ya mara kwa mara na ushauri ambao amekuwa akinipatia katika utekelezaji wa majukumu ya kusimamia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, eneo ambalo sote tutakubali kwamba ni eneo mtambuka katika utawala wa nchi yetu na katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelekezo na ushauri ambao wananipatia katika kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini. Napenda pia kumshukuru sana Spika na Naibu Spika pamoja na Uongozi wote wa Bunge kwa ushirikiano mkubwa ambao mnaipatia ofisi hii ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za pekee ziende kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote ambao walitoa maoni ya ushauri ambao tunaamini kabisa utaweza kusaidia sana kuboresha utekelezaji wa majukumu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ipo kwa awamu mbalimbali za Serikali zilizotutangulia, Serikali hii ya Awamu ya Tano inaendelea kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inaendelea kutekeleza sera na Mipango ya Kitaifa ya muda mrefu ambayo wote tunafahamu ilibuniwa kwa ajili ya kuwaondolea wananchi wa Taifa letu umaskini lakini vilevile kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia sera na mikakati hiyo, lakini vilevile kupitia dira yetu ya Taifa ya Maendeleo pamoja na MKUKUTA na MKUZA, pamoja na Mpango wetu wa Maendeleo wa muda mrefu, tunaamini kabisa mipango hii itakapotekelezeka, basi lengo letu ni kujenga uchumi wa viwanda pamoja na maendeleo ya watu. Wote mtakubaliana nami kwamba ili kutekeleza sera hizi, tunahitaji Utumishi wa Umma ulio imara na makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwetu sisi katika Utumishi wa Umma, sekta ambayo naiongoza, nia yetu ni kuendelea kuboresha Sekta ya Utumishi wa Umma, kuhimiza misingi ya weledi, kuweka mifumo ya Menejimenti inayowezesha watumishi wa umma kuwajibika na kuwa na maadili ili waweze kutoa huduma kwa wananchi na wadau wengine na hivyo kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini endapo Watumishi wa Umma watazingatia sifa nilizozitaja awali, tutakuwa na utendaji mzuri katika utendaji wetu, utendaji ambao utakuwa na matokeo, lakini vilevile utendaji ambao utatuwezesha kuwa na tija zaidi, kuwa na mapato zaidi na hatimaye kuboresha zaidi maslahi ya Watumishi wa Umma; na wote mnafahamu hilo ndilo lengo letu la mageuzi kupitia Sekta ya Umma ambayo tunaendelea kuyafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Utumishi wa Umma ni sehemu muhimu sana katika utendaji wa Serikali, ni utumishi ambao unahitaji kutekeleza sera na mikakati mbalimbali ya Serikali iliyopo madarakani. Wote tunaamini ili Utumishi wa Umma uweze kutekeleza sera na mikakati ya Serikali iliyo madarakani ni lazima kuzingatia misingi ifuatayo:-
· Ni lazima kuwa na dira na dhima inayoashiria matakwa ya jamii ya kuleta maendeleo na siyo kwa maslahi binafsi;
· Kuwa na msingi ambao itaonekana Serikali inaungwa mkono na wananchi kwa kuwa jitihada zake zinaleta faida kwa wananchi wake; na
· Kuwa na mfumo wa kiutawala, Menejimenti na Kisheria inayoelekewa na kuheshimiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Utumishi wa Umma uongozwe na kusimamiwa ili kuhakikisha kwamba hauendi kinyume na misingi hiyo mitatu ambayo nimeieleza. Ili kuweza kulinda misingi hiyo niliyoieleza awali, Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko katika usimamizi wa Utumishi wa Umma; imekuwa ikifanya mabadiliko haya katika usimamizi wa Utumishi wa Umma mara kwa mara ili kuenenda na misingi niliyoitaja awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii imejidhihirisha wazi kupitia mageuzi ambayo tumeyafanya tangu uhuru, lakini vilevile kupitia program ya kuleta mabadiliko ya utendaji katika Utumishi wa Umma au Public Service Reform Program ambayo ilitekelezwa kuanzia mwaka 2000 mpaka 2014. Kama ilivyo katika Awamu mbalimbali za Serikali zilizotangulia, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuboresha Utumishi wa Umma ili uendelee kuwa na manufaa kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hatua mahsusi za kusimamia Sera na mifumo ya Menejimenti; matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano; nidhamu; mapambano dhidi ya rushwa; uadilifu na uwajibikaji; zimeendelea kuchukuliwa. Tunaamini kwamba kwa kuzingatia mambo haya, Watumishi wa Umma watafanya kazi kwa weledi na bidii, lakini vilevile bila kusahau maslahi yao kulingana na hali ya uchumi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tutaendelea kuimarisha vita dhidi ya rushwa kama hatua ya kuimarisha uadilifu, tutaendelea kuhakikisha kwamba viongozi na Watumishi wa Umma wanatoa Viapo vya Uadilifu. Vile vile pamoja na viapo hivi vya uadilifu, tutahakikisha kwamba Watumishi wa Umma wanakwenda kwa kuzingatia viapo vyao, wanawajibika kutokana na matokeo ya maamuzi ya kazi wanazozifanya ili kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka kwa kutumia ofisi na nyezo kwa manufaa binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hizi, Serikali vilevile itaendelea kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia unazingatiwa katika Utumishi wa Umma, lakini vilevile mifumo ya Kimenejimenti inayojumuisha matumizi zaidi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, nayo pia inaimarishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi yangu inachukua hatua thabiti za kukomesha watumishi hewa kwa kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taarifa za kiutumishi na mishahara wa Lawson na kuufanya uweze kuzungumza na mifumo mingine kwa kuongeza uwajibikaji kwa Wakuu wa Taasisi katika ulipaji wa mishahara na maslahi; kufanya ukaguzi wa kushtukiza wa mara kwa mara kwenye orodha ya malipo na mishahara; lakini vilevile kufanya ukaguzi dhidi ya mfumo wenyewe; na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kijinai watumishi wote watakaobainika kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa takwimu za haraka haraka, ukianzia tarehe 1 Machi, 2016 hadi tarehe 24 Aprili, 2016 watumishi 8,236 waliweza kuondolewa katika mfumo huu wa mishahara na utumishi. Mgawanyo wa watumishi hao kupitia Serikali Kuu ni watumishi 1,614 na katika Serikali za Mitaa ni watumishi 6,622. Ukiangalia hili ni ongezeko la watumishi 2,731 ukilinganisha na uchambuzi ambao uliwasilishwa tarehe 11 Aprili na Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika fedha ambazo zingepotea endapo watumishi hawa 8,236 wasingeondolewa katika mfumo kwa miezi hiyo, ingeligharimu Taifa letu takribani Shilingi bilioni 15.4. Kwa kuwa zoezi hili ni endelevu, nitaendelea kutoa taarifa kwa kadiri itakavyokuwa ikiwezekana, lakini vile vile viongozi mbalimbali wa Taifa letu nao pia wataendelea kutoa taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kumekuwa na tabia ya Watumishi wa Umma ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mfumo na wamekuwa wakiuhujumu mfumo huu na kwa muda mfupi tu tayari tumeshawafungia Maafisa Utumishi 56, lakini vilevile hivi sasa tunafanya uchambuzi wa kujua masuala yote ambayo wameyafanya kinyume na taratibu, lakini vilevile kuhakikisha wanarejesha fedha zote ambazo wamelisababishia hasara Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatutaishia kwenye kurudisha fedha peke yake, ni lazima mkondo wa sheria uchukue hatua yake na hatutasita! Tumefundisha Maafisa Utumishi 1,500 ambao wanaweza wakasimamia mfumo huu. Hatutasita hata ikibidi kuwafukuza wote! Kwa hiyo, napenda tu kutoa tahadhari kwa Maafisa Utumishi ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mfumo huu kuhakikisha wanausimamia kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yangu imechangiwa na takriban Waheshimiwa Wabunge 85, wakiongozwa na Mheshimiwa Jasson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, lakini vile vile Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na nitambue pia na kumshukuru Mheshimiwa Ruth Mollel, Waziri Kivuli wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa maoni na michango yao mizuri ambayo naamini kabisa itatusaidia katika kuboresha Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile muda uliopo hautoshi kujibu hoja zote kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge walivyowasilisha humu Bungeni, nitajitahidi kujibu hoja kwa kadri muda utakavyoruhusu. Napenda kuwahakishia Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zote zitajibiwa kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge wataweza kupata majibu hayo kabla ya kumalizika kwa Mkutano huu wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa baada ya kusema hayo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao nitakuwa sijataja majibu ya hoja zao waridhike, tutawapatia kwa maandishi pamoja na Wabunge wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikielezea utenguaji wa uteuzi wa Makatibu Wakuu ambao walitenguliwa uteuzi wao tarehe 8 Aprili na alitoa ushauri kwamba ni vema Serikali iwalipe kifuta jasho (golden handshake) kwa kutumia uzoefu wa miaka ambayo wameitumikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, Makatibu Wakuu hao ambao wametenguliwa, wameshaandikiwa barua za kujulishwa hatima zao; vile vile wako ambao tayari tumewashuhudia wameteuliwa katika nyadhifa nyingine; mfano, wako ambao wameteuliwa kuwa Makatibu Tawala wa Mikoa. Pia kwa wale ambao utumishi wao tayari umeshakoma, Serikali itawalipa mafao yao kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya kwamba Serikali ihakikishe inazingatia sheria na kanuni wakati inapokuwa inachukua hatua dhidi ya Watendaji mbalimbali na kwamba kwa watakaokutwa na hatia za ufisadi na rushwa, wachukuliwe hatua za kinidhamu na kufilisiwa mali zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, uchukuaji wa hatua katika masuala mbalimbali, yaani kinidhamu kwa Watumishi wa Umma, umekuwa ukifanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ambazo ziko katika Utumishi wa Umma. Napenda tu kutaja vifungu vichache; ukiangalia kwa mujibu wa kifungu cha 34, 38 na 40 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 kuhusiana na suala zima la kufilisi mali zilizopatikana kwa njia ambayo siyo halali; mali ambazo zimepatikana kwa njia hizo ambazo hazifai, zinatakiwa zitaifishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema tu kwamba utaifishwaji huu unafanyika tu pale ambapo ushahidi unakuwa umethibitika na unakuwa umekusanywa na baada ya watuhumiwa kupatikana na hatia Mahakamani. Nilihakikishie tu Bunge lako kwamba Serikali hii itaendelea kuzingatia misingi ya utawala bora katika usimamizi mzima wa Utumishi wa Umma. Vilevile tutahakikisha kwamba nidhamu katika Utumishi wa Umma inakuwa ya hali ya juu na inaimarishwa, pia fedha zote na mali za umma zitalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Felister Bura, Mheshimiwa Mama Genzabuke na Mheshimiwa Mama Sara kuhusiana na madeni ya Watumishi wa Umma especially wa kada za chini; Walimu, Wauguzi, Polisi na alitoa ushauri kwamba ni vema yakahakikiwa ili kuhakikisha kwamba madeni haya ya watumishi yanaondolewa na hayatakuwepo tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kulithibitishia Bunge lako kwamba, tayari madai mbalimbali ya Watumishi wa Umma yamekuwa yakilipwa kwa nyakati mbalimbali. Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ameweza kuelezea namna ambavyo madai mbalimbali yasiyo ya mishahara jinsi ambavyo yamelipwa. Nalihakikishia tena Bunge lako Tukufu kwamba, tutaendelea kulipa kwa kadiri hali ya kiuchumi inavyoruhusu; na tunatambua kwamba madai hayo ni muhimu lakini lazima tuzingatie suala zima la uhakiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa malimbikizo ya mishahara, kwa madeni ambayo tayari yameshahakikiwa na yanayosubiri kulipwa watumishi 1,622 yenye thamani ya takriban Shilingi bilioni 2.1, tayari yamekuwa yakiendelea kuhakikiwa na pindi yatakapokamilika basi yataweza kulipwa kwa utaratibu unaofaa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka huu wa fedha peke yake tayari Serikali imelipa takriban Shilingi bilioni 26.9 kwa watumishi 28,787 kama madeni mbalimbali yanayohusiana na malimbikizo ya mishahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo tumekuwa tukiipata katika madeni haya ni hasa katika suala la mfumo wetu kukokotoa automatic arrears. Kwa wale watumishi ambao taarifa zao au madai yao yanaingizwa katika mfumo baada ya tarehe 15, mfumo wetu kwa namna ambavyo umekuwa set, payroll inakuwa imefungwa. Kwa hiyo, inakuwa ni vigumu kuweza kuingiza taarifa hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba tumeona hili ni tatizo na limekuwa likileta usumbufu mkubwa na hivi sasa tunalifanyia kazi ili kuona ni kwa namna gani suala hili linaweza kurekebishwa ili hata kama Mtumishi atakuwa ameingizwa katika mfumo, baada ya payroll kufungwa, basi ukokotoaji uweze kufanyika bila ya kumsababishia mtumishi usumbufu wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo tumekuwa tukiipata, unakuta mfumo unakokotoa automatic arrears, lakini vile vile unakuta katika Watendaji wetu au Waajiri na wenyewe wanaleta madai mengine manually kupitia karatasi. Sasa kwa kufanya hivyo, kunasabisha marudio katika gharama na kufanya hivyo ni lazima sasa ili tuwe na uhakika, tufanye uhakiki, tusije tukajikuta tunalipa gharama mara mbili na kuisababishia Serikali hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja nyingine kuhusiana na uhamisho kwa Watumishi wa Umma na kwamba uende sambamba na ulipaji wa fedha za uhamisho. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, tayari Serikali ilishatoa Waraka wa Utumishi Na.1 wa mwaka 2009 kuhusiana na udhibiti wa ongezeko la madeni ya Serikali kwa Watumshi wa Umma. Napenda kusisitiza kwa mara nyingine tena, waajiri wetu wahakikishe hawafanyi uhamisho kama hawajatenga fedha, kwa sababu wakifanya hivyo watajikuta wamekiuka suala zima la usimamizi wa Watumishi wa Umma na watakuwa wamewanyima haki watumishi ambao wamehamishwa bila kupata fedha hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine ya Mheshimiwa Makilagi, Mheshimiwa Mwakajoka pamoja na Waheshimiwa wengine kuhusiana na suala zima la uboreshaji wa misharahara ya watumishi, lakini vile vile kuweka uwiano mzuri wa mishahara ya Watumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali inatambua sana umuhimu wa kuboresha mishahara pamoja na maslahi kwa watumishi wake, lakini vile vile kuweza kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ili kuweza kuwavutia watumishi wengi zaidi waweze kuingia katika Utumishi wa Umma na kuhakikisha kwamba wanapenda kubaki katika Utumishi huu wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, kupitia Tume ya Mheshimiwa Ntukamazina wakati huo, iliandaa mapendekezo kwa Mheshimiwa Rais ya kuanzisha Bodi ya Mishahara na Maslahi. Ni Bodi ambayo tayari ipo na imeshaanzishwa na majukumu yake makubwa ni kumshauri Mheshimiwa Rais kuhusiana na suala zima la uboreshaji wa mishahara na maslahi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vile vile kueleza kwamba, tayari Bodi hii imekuwa ikifanya kazi nzuri na tayari imeshaanza suala zima la tathmini ya kazi pamoja na uhuishaji wa madaraja. Ni imani yetu kwamba itakapofika mwezi Februari, mwaka 2017 tathmini hii itakapokamilika, basi tutaweza kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujua ni kwa namna gani sasa tunaoanisha pamoja na kuwianisha mishahara pamoja na kuangalia ngazi mbalimbali za mishahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tulishafanya utafiti kupitia Bodi hii kuangalia watumishi ambao wanafanya kazi katika maeneo yenye mazingira magumu, ni kwa namna gani sasa wanaweza wakapata motisha. Rasimu ya mwongozo huo iko tayari na hivi sasa inakamilishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi Serikalini na itakapokuwa tayari ni imani yetu kwamba tutaiwasilisha pia kwenu ili muweze kuifahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi pia imeandaa rasimu ya mwongozo wa kupendekeza mishahara. Ukiangalia kuna sheria mbalimbali zinazoanzisha mamlaka na taasisi mbalimbali. Kila taasisi unakuta imejiwekea wajibu kupitia Bodi yake kupanga mishahara mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko taasisi ukiangalia kati ya Kiongozi Mkuu wa taasisi husika mpaka yule wa chini anayepata kima cha chini, uwiano unatofautiana sana. Wengine wana uwiano wa 1:63. Yeye anapata mshahara mmoja mwenzake ni mpaka akae miezi 63 ndipo aweze kumfikia. Pia utakuta taasisi nyingine ni uwiano 1:23, wengine ni uwiano wa 1:50. Kwa hiyo, ni lazima sana, wako ambao wamesema kama shirika husika linajitengenezea faida, linatengeneza fedha zake lenyewe, kwa nini lisiweze kujilipa gharama kubwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili kwa kweli tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuhakikisha kwamba mshahara hautazidi Shilingi milioni 15. Kwenye hili kwa kweli hatutarudi nyuma na tayari hatua zimeshaanza kufanyiwa maandalizi na wakati wowote utekelezaji utaweza kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine kuhusiana na suala zima la upandishwaji wa vyeo kwamba uendane na ulipwaji wa mishahara. Changamoto ambayo tumekuwa tukiipata; upandishwaji wa vyeo unapofanyika, ni lazima Mwajiri aweze kutuma taarifa mbalimbali za maamuzi ya Kamati ya Ajira ya Taasisi husika; lakini wanapotuma kwa ajili ya uidhinishaji Utumishi, wengine unakuta taarifa zao zinakuwa na makosa, wengine unakuta waliwapandisha bila kuzingatia miundo ya maendeleo ya Utumishi, wengine unakuta waliwapandisha bila kuweka bajeti katika mwaka huo wa fedha, lakini vile vile unakuta katika suala zima la ikama hawakuweza kulizingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda tu kuwataka Waajiri waweze kuzingatia maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi (Chief Secretary) pamoja na Katibu Mkuu Utumishi katika suala zima la upandishaji vyeo watumishi na waweze kujitahidi; wazingatie vigezo vilivyoelezwa na waweze kuchukua hatua kwa wakati ili wasisababishe madeni na malalamiko ya watumishi yasiyokuwa ya lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la upungufu wa watumishi katika sekta mbalimbali. Napenda tu kuliarifu Bunge lako na kusisitiza kama ambavyo nimeeleza katika hotuba yangu, katika mwaka huu wa fedha tutaajiri watumishi 71,496. Wako waliosema ni mchakato; ni mchakato, ni lazima ili kuweza kuandaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapofanya maandalizi ni lazima pia kuweza kuzingatia ukomo wa bajeti ya mishahara. Bajeti ya mishahara inategemea mapato ya ndani. Sasa inapofikia umezidi zaidi ya asilimia 51, tungependa sana kwa kiasi kikubwa bajeti yetu ya mishahara iwe kubwa, lakini inakuwa ni ngumu. Vipo vigezo vya Kimataifa tunafungwa navyo na ni lazima tuweze kuhakikisha tunavizingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Sekta ya Elimu katika mwaka huu wa fedha, tutatoa ajira mpya za watumishi 28,957, kwa upande wa afya, ajira 10,870; kwa upande wa kilimo ajira 1,791; mifugo ajira 1,130; uvuvi ajira 400; Polisi ajira 3,174; Magereza ajira 1,000; Zimamoto ajira 850 na ajira nyinginezo 23,324. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizo ajira nyinginezo 23,324 ziko pia nafasi 1,349 kwa ajili ya Watendaji wa Vijiji na nafasi 648 kwa ajili Watendaji wa Kata ambazo zitatumika kujaza nafasi za ajira kwa kada hizi katika Halmashauri mbalimbali nchini. Nipende tu kueleza ajira hizi zitaanza mwezi Mei, 2016. Kwa hiyo, nitaomba kwa kweli muweze kutupa ushirikiano wa dhati katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ikulu pamoja na Utawala Bora kulikuwa na hoja kuhusiana na Fungu 30 la Ofisi ya Rais, kwamba ilikuwaje mwaka wa 2015 walikuwa na Shilingi bilioni 310.3 zilizoidhinishwa lakini kwa mwaka huu wana Shilingi bilioni 354.6. Napenda tu kueleza kwamba, kiasi kilichoongezeka ni Shilingi bilioni 52.3 na kinatokana na nyongeza ya mishahara ya taasisi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu baada ya mishahara kupanda mwezi Julai mwaka 2015 na mishahara hiyo ndiyo inayolipwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Msigwa alitaka kufahamu, au alibeza kwamba nimepata wapi uhalali wa kuwasilisha bajeti hii Bungeni wakati utawala bora unakanyagwa? Napenda tu kusema kwa mara nyingine tena kwamba, utawala bora haukanyagwi. Kama ambavyo alieleza misingi mbalimbali 22 ya utawala bora, tutaendelea kusimamia utekelezaji wake, tutaendelea kuhakikisha kwamba hatukiuki Katiba. Vile vile nimhakikishie kwamba kupitia Ibara ya 55 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri ana mamlaka kamili ya kuwasilisha bajeti Bungeni. Vile vile wasilisho hili ambalo nimelifanya, limezingatia misingi ya utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia na hoja ya Mheshimiwa Mwakajoka kwamba Kiongozi wa Kitaifa, Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akishindwa kutambulisha Vingozi wa Vyama vya Upinzani wakati wa ufunguzi wa miradi mbalimbali mikubwa. Napenda kupingana na hoja hii, kwa sababu nikichukua takwimu za haraka haraka, tukiangalia katika ufunguzi wa flyover ya TAZARA; ufunguzi wa Daraja la Kigamboni; kwa Kigamboni mimi mwenyewe nilikuwepo. Meya wa Jiji alitambulishwa. Kwa nini hamwelezi hapa kwamba walitambulishwa? Pia walitambulishwa kupitia ufunguzi wa Mradi wa flyover.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa AG kwa ufafanuzi ambao ameutoa kuhusiana na TAKUKURU kupewa nafasi au mamlaka ya kupeleka kesi za rushwa Mahakamani. Kwa kweli ameeleza vizuri sana, lakini bado niendelee kusisitiza, ni maamuzi mazuri kuhusiana na suala zima la checks and balances.
Vile vile ukiangalia kwa DPP kupitia Ibara ya 59 ya Katiba yetu, imeeleza atakuwa na mamlaka ya kuendesha mashtaka. Kwa makosa yale ambayo Mheshimiwa AG ameyaeleza, yanayoangukia katika Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya 2007 ndiyo ambayo yamekuwa na mamlaka kwa TAKUKURU kuweza kushtaki bila kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, tunachukua ushauri na tutaendelea kuufanyia kazi kuona faida na hasara zake, endapo tutaamua kubadili mfumo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Grace Kiwelu alitoa kwamba kuna Shilingi milioni 90 ziliibiwa katika Basket Fund. Napenda nishukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametupatia taarifa mbalimbali kuhusiana na upotevu wa fedha. Nawahakikishia kwamba tutazifanyia kazi kwa kina na hatua stahiki zitachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Manispaa ya Moshi, tayari watuhumiwa wameweza kurejesha fedha ambazo walikuwa wamezifuja, lakini hii ni hatua ya awali tu. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakapokamilisha tathmini ya ushahidi na majalada haya yatakapopelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, yatakapopata kibali tutaweza kuyawasilisha Mahakamani na hatua stahiki zitachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa AG kuhusiana na majibu ya hoja ya hati fungani ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Kabwe Zitto; vile vile kulikuwa kuna hoja kuhusiana na IPTL na Tegeta Escrow ambapo shauri liko Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja ya hati fungani, kwamba ni kwa nini Serikali ya Tanzania au TAKUKURU haijaishtaki Benki ya Standard Bank. Napenda tu kueleza kwamba, suala hili linahusisha uchunguzi unaoendelea na vile vile suala hilo sote tunafahamu iko kesi nyingine Mahakamani. Tutakapokamilisha mashauriano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi na endapo ushahidi utathibitisha tuhuma ambazo zimeelezwa, bila kusita Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya mtu au taasisi yoyote ya ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja pia kwamba Maafisa wa TAKUKURU wasikae sehemu moja zaidi ya miaka mitatu. Tayari upo utaratibu, kwa mpango ambao TAKUKURU wamejipangia, wao ni miaka mitano mitano. Tutahakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha tunaouanza tutaanza kuhamisha watumishi 90 ambao wameshakaa kwa zaidi ya miaka mitano. Inakuwa ni miaka mitano kwa sababu, wakati TAKUKURU imeundwa upya mwaka 2007 waliajiriwa watumishi wengi zaidi.
Kwa hiyo, tukienda kwa miaka mitatu mitatu tutajikuta pia tunawavunja nguvu na matokeo yake wanaweza wakajikuta wana upungufu wa watumishi. Vile vile tunazingatia pia suala zima la gharama katika uhamisho huo ambao umekuwa ukifanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia kuna hoja ya Mheshimiwa Kakunda kwamba, wako watumishi ambao wanajikuta wameshtakiwa, wana mashtaka ya rushwa halafu wamekuwa wakitumia fedha za Serikali kwenda katika kesi zao Mahakamani; wamekuwa wakijilipa per-diems. Napenda kukemea, wako Wakurugenzi mbalimbali wa Halmashauri wamekuwa wakifanya hivyo. Tunaendelea kuwachunguza na itakapothibitika, watatakiwa kurudisha fedha zote ambazo walikuwa wakizitumia kwa ajili ya kwenda Mahakamani, lakini vile vile gharama zote ambazo walizitumia kwa ajili ya kuendesha magari na mafuta na kuwalipa madereva kuwapeleka Mahakamani kusikiliza kesi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni lazima likome na liwe fundisho kwa watendaji wengine wote mbalimbali watakaokuwa na mashauri mbalimbali ya kiutendaji na ya kuhusiana na rushwa Mahakamani kutumia gharama za Serikali kwa ajili ya kesi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna hoja kwamba wako watumishi wana kesi mbalimbali za jinai, lakini bado wanaendelea na Utumishi wa Umma. Niseme tu kwamba kupitia kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 imetoa discretion kwa Mwajiri aidha, mtumishi aendelee na kazi au asimamishwe mpaka hapo shauri lake litakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika Kanuni ya 30 (2) ya Standing Order, lakini vile vile kanuni ya 50(a) zimetoa discretion hii. Mara zote ambapo wamekuwa wakithibitika, hatua stahiki za disciplinary procedures za kusimamishwa pamoja na kuhitimishwa katika kazi zimekuwa zikichukuliwa. Niseme suala hili tunalitambua na kwa kweli kidogo na sisi limekuwa likitupa concern. Tumeshaanza sasa hivi kufanya mapitio ya Standing Orders mbalimbali, lakini tutayapeleka kwa wadau, watakachopendekeza tutaweza kuona ni nini kiweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mtuka ambaye alieleza kwamba suala la bajeti ya TAKUKURU kwa kweli imekuwa ni ndogo. Niseme tu kwamba tunamshukuru kwa ushauri wake na Serikali tutaendelea kuchukua hatua kuiwezesha TAKUKURU kwa kadiri uwezo wetu wa kifedha utakavyokuwa ukiruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kisangi aliendelea kupongeza suala zima la uanzishwaji wa clubs za wapinga rushwa na nimhakikishie kwamba tutaendelea kufanya hivyo kila mwaka itakapobidi na tunaomba ushirikiano wao wa dhati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwenye suala zima la upungufu na ukosefu wa majengo kwa ajili ya Sekretarieti ya Maadili. Napenda tu kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, tayari kwa jengo la Kusini Mtwara limeshakamilika na tayari wameshahamia, tunasubiri tu kukamilisha hatua chache zilizobaki kwa ajili ya kuhitimisha jengo hili liweze kukamilika kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika bajeti ya mwaka huu kama ambavyo mtaona, tumetenga bajeti katika fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Kanda ya Kati Dodoma. Tumeanza maandalizi, tutafanya usanifu wa jengo la Ofisi ya Sekretarieti, Makao Makuu au Maadili House na tunaendelea pia kufanya mashauriano na Wakala wa Majengo (TBA) ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kupata mbia wa ajili ya kuliendeleza jengo hili la Makao Makuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna hoja kutoka kwenye Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikiitaka Serikali ihakikishe kwamba inafungua Ofisi katika kila Mkoa kwa ajili ya Sekretarieti za Maadili. Ushauri huu tunaupokea na lengo letu kama Sekretarieti ni kuhakikisha kwamba, tunasogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kwa hivi sasa tumeshafungua ofisi saba na tutaendelea kufanya hivyo kwa kadiri hali itakavyokuwa ikiruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba mali na madeni ya viongozi zitangazwe kwa uwazi wakati viongozi wanapoingia madarakani na wakati wanapohitimisha uongozi wao. Ukiangalia katika Kifungu cha 20 kikisomwa pamoja na Kifungu cha saba (7) cha Kanuni za Maadili za Viongozi wa Umma, mwananchi anayo fursa ya kuweza kukagua daftari la tamko la mali na madeni atakapokuwa amelipia sh. 1,000, lakini haipaswi kutangaza mali zile hadharani. Unatakiwa uzitumie tu kwa sababu zilizokupelekea kufanya ukaguzi huo. Kwa hiyo, napenda tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 20 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, lakini vile vile matakwa ya kanuni ya saba (7) ya Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma za mwaka 1996.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia kuna hoja kutoka kwa Kamati ya Mheshimiwa Lubeleje pamoja na Waheshimwa wengine, kwamba TASAF iendelee kutoa elimu kuhusiana na TASAF Three. Nipende tu kuhakikisha kwamba tayari TASAF imekuwa ikitoa elimu kuhusiana na mpango huu na imekuwa pia ikieleza kuhusiana na taratibu mbalimbali na kero mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza zimekuwa zikijibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukitumia Redio mbalimbali za kijamii ambazo ziko katika Halmashauri zetu kuweza kujibu hoja mbalimbali ambazo zimejitokeza katika jamii kuhusiana na mpango huu wa TASAF awamu ya tatu. Niendelee tu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa wako karibu zaidi na wananchi na wenyewe pia waendelee kutusaidia kuuelezea mpango huu ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba, wako watu ambao wamekuwa hawafanyi uadilifu katika fedha hizi za TASAF! Napenda tu kuliarifu Bunge lako Tukufu, kuanzia mwezi Aprili tumeshaanza uhakiki kuangalia walengwa wote ambao wananufaika na mpango huu ambao hawastahili na tayari tumeshaondoa kaya 6,708, lakini vilevile tunaendelea kuchukuwa hatua stahiki za kinidhamu pamoja na za kijinai kwa wale ambao walisababisha majina haya kuingizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba asilimia 70 peke yake ya Vijiji ndiyo ambavyo vimefikiwa na mpango huu. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, katika mwaka huu wa fedha asilimia 30 ya Vijiji ambavyo vimebaki, Shehia na Mitaa mbalimbali itaweza kufanyiwa utambuzi pamoja na uandikishaji na baadaye malipo yatakuja kuanza katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kulikuwa kuna hoja nzuri sana kwamba, walengwa hawa wanaopatiwa ruzuku hii ya uhawilishaji, ikiwezekana waweze kuunganishwa na Mfuko wa Afya ya Jamii au CHF. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tayari Halmashauri 27 zikiwemo Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Singida pamoja na Mtwara, wamekuwa wakifanya vizuri na kaya takribani 52,980 zimeshajiunga na Mfuko huu wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa rai kwa wananchi wengine mbalimbali, tutakapokuwa tukiwahamasisha na kuendelea kuwaelimisha kuhusiana na umuhimu wa fedha hizi na Mfuko huu, basi wajitahidi kujiunga kwa sababu tunaamini itaweza kuwapunguzia gharama kubwa. Kama tunavyofahamu, ruzuku hii imepeleka pia masharti katika suala zima la elimu, lishe pamoja na afya. Kwa hiyo, tunaamini kwa gharama ile ya Sh. 10,000/= kwa mwaka mzima, itaweza kuwasaidia pia katika suala zima la afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja ilitolewa kwamba ufanyike ukaguzi maalum kuhusiana na ufanisi wa Mfuko, lakini vilevile kuangalia kama suala zima la kugawa fedha litaweza kuwa na tija. Napenda tu kusema kwamba tulishaagiza kwa CAG kufanya ukaguzi maalum kujiridhisha tu kama mambo yote yanaenda vizuri. Pia napenda tu kusema kwamba tija ipo. Ukiangalia katika Mfuko huu unaotolewa katika ruzuku hii ya uhawilishaji imekuwa ikienda sambamba na suala zima la kuelimisha wananchi pia katika suala zima la uchumi na umuhimu wa kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu imeunganisha na mpango wa kuweza kulipa ujira, wanakuwa wanapewa fedha kidogo, ruzuku ya uhawilishaji, lakini hapo hapo kwa siku 14 kwa wakati ambao wanapata ukata wa hali ya juu, wamekuwa wakiweza kufanya kazi mbalimbali za kijamii na kulipwa. Tumejionea pia kwa wale ambao wametumia fedha hizi vizuri, wameweza kwa kweli kujikomboa na wengi wao ndani ya miaka mitatu wameweza kuondokana na mfumo huu na kutoa nafasi kwa wananchi wengine kujiunga na mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kuhusu miradi ambayo haikukamilika katika TASAF awamu ya pili. Tayari tumeshafanya tathmini, iko miradi 137 ambayo haikuweza kukamilika katika TASAF awamu ya pili, lakini tayari tumekwishaingia makubaliano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tayari tumeshaelekeza kwamba Halmashauri ambazo hazijakamilisha, basi zijitahidi kuendelea kuhakikisha kwamba zinakamilisha mapema na pindi zitakapokamilisha miradi hiyo iliyobakia 137 TASAF itaweza kutoa Hati kuhusiana na ukamilishaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kuhusiana na MKURABITA. Wengi wameweza kuchangia sana kuhusiana na suala zima la mpango wa matumizi bora ya ardhi. Wote tunafahamu, katika nchi yetu ni asilimia 10 pekee ndiyo imeandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Vijiji vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kushirikiana na MKURABITA pamoja na Wizara ya Ardhi imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kwamba Vijiji vyote vinaandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kwa kutambua kwamba fedha inayotoka ni kidogo kidogo na hatuwezi kukamilisha asilimia yote 90 kwa mwaka mmoja, Serikali imeanzisha Mfuko endelevu wa Halmashauri mbalimbali kwa ajili ya urasimishaji wa ardhi katika ngazi za Wilaya na tayari katika mwaka huu wa fedha kuanzia tarehe 1 Mei, urasimishaji wa majaribio utaanza katika Mkoa wa Iringa; Iringa Mjini pamoja na Morogoro Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa waunge mkono na ni imani yangu Mheshimiwa Mchungaji Msigwa hutachukulia na kulipeleka kisiasa suala hili na utaweza kuliunga mkono. Tutahakikisha kwamba fedha zile zitakazotolewa; MKURABITA watatoa milioni 100 kwa kila Wilaya, kwa kuanzia na Wilaya hizi za majaribio.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Halmashauri zitaweza kukopeshwa na Benki ya CRDB ili kuweza kuhakikisha kwamba suala zima la upimaji na suala zima la uuzaji wa viwanja linafanyika ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaingia katika mfumo rasmi wa umiliki wa ardhi. Wote tunatambua; unapokuwa na ardhi ambayo imerasimishwa itaweza kukusaidia pia kuweza kuitumia kama dhamana kwa ajili ya kujipatia mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja pia kwamba, baadhi ya Benki hazitambui hati mbalimbali za kimila. Napenda kutoa rai kwa Benki mbalimbali, hati hizi zinayo thamani sawa kabisa na waweze kuhakikisha kwamba wanaziunga mkono na kuweza kutoa mikopo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitimisha kwa kuomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu muweze kuiunga mkono hoja hii ili kutuwezesha kutekeleza vema majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Taasisi zake kwa ufanisi katika mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.