Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua fursa hii kukushukuru sana kwa nafasi hii niliyoipata. Pia naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Mheshimiwa Mabula, Katibu Mkuu na Makamishna wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa, nimpongeze sana rafiki yangu Kamishna Mathew wa pale Dar es Salaam kwa kazi kubwa anayoifanya, halali usingizi, ni kwa sababu ya kuhakikisha migogoro inakwisha Dar es Salaam. Kamishna wangu wa Kanda ya Mashariki, kwa kweli amenisaidia sana katika mgogoro wa vijiji vinne vya Mlamleni, Luzando, Mwanambaya na Mipeko. Amefanya kazi kubwa na natumai kazi hii ataimalizia vizuri hapo mbele. Vile vile, kwa namna ya kipekee, nitambue kazi nzuri anayoifanya Kamishna wetu wa Kanda ya Kusini, kaka yangu Luanda, wote Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue fursa hii kurudia tena kusema kwamba kazi hii kubwa wanayoifanya, Mheshimiwa Waziri, tunalo sisi la kujifunza. Kwa sababu Waswahili wanasema, ukiona vyaelea ujue vimeundwa, Mheshimiwa Waziri Lukuvi, kwake yeye kwa kazi
kubwa anayoifanya na Wabunge wote humu tunamsifu, ni kwa sababu tunakwenda kila mahali, tunatatua migogoro na tunafanya vema sana. Hata kwangu Mkuranga migogoro niliyoitaja na mingine ambayo sikuitaja ameifanyia kazi kubwa sana. Namshukuru sana na Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo tatizo katika Kijiji cha Dundani na hili ni tatizo la maeneo mengi linalohusu fidia. Wananchi wanazuiwa kwa ajili ya uendelezaji wa ardhi zile kwa ajili ya uwekezaji, ni jambo jema. Tunapenda uwekezaji, lakini sasa inapofika mahali watu wanasubiri jambo kwa muda mrefu sana inafika miaka mitatu, minne, mitano, maeneo yao yanageuka kuwa mapori, hawawezi kuendeleza chochote katika maeneo yale. Hili linakuwa ni tatizo na linawakatisha tamaa sana wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri, yeye ni champion, atusaidie tutoke mahali pa namna hii. Wananchi wanaozuiwa kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu na yanageuka kuwa ni mapori, hawawezi kuvuna nazi zao, hawawezi kulima mihogo pale, hawawezi kufanya maendeleo ya namna yoyote, tuwasaidie. Kama tumeshindwa tutafute namna ya kukaa nao na tuwarejeshee maeneo yao waweze kuendelea na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nitoe ushauri ni eneo la upimaji na uendelezaji wa ardhi. Hili eneo lina potentiality kubwa sana, wazo langu ni kwamba, kwanza nawapongeza sana Wizara, wamekubali kuchukua taasisi na makampuni binafsi kuweza kushiriki katika kazi hizi na hili ni jambo jema, ni lazima tubiasharishe mawazo yetu. Hata hivyo, hapa bado liko tatizo, Wizara ya Ardhi mshirikiane vema hasa na wenzetu wa TAMISEMI, uendelevu wa ardhi kwa kutumia kampuni binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanachukua pesa zao lakini mlolongo unachukua muda mrefu sana, hasa mtu akiwa amekopa pesa yake benki kuweza kufanya marejesho haiwezi kuwa kazi nyepesi tena. Kutoka kununua ardhi mpaka kufika kuipima, mpaka kufika kuisaidia Serikali kuwauzia wananchi ili sasa papatikane ardhi iliyoendelezwa, inachukua kipindi kirefu sana. Matokeo yake inawakatisha tamaa, Mheshimiwa Waziri aMheshimiwa Mwenyekiti, amefanya kazi nzuri ya kuweka bei elekezi, maana sasa ardhi ilikuwa inafanya inflation, kila mtu anajipangia anavyoweza tu, sasa tume-control hilo jambo, ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, lazima tuwe na ushirikiano ili hii kazi ya kuipima ardhi yetu ya Tanzania kwa kutumia taasisi binafsi iweze kuwa yenye kuvutia, kazi hii ya kupima Mheshimiwa Waziri peke yake hataweza, tutarudia hapa mwaka hadi mwaka hata miaka mia moja, hatutaweza, ndiyo ile nasema lazima tubiasharishe mawazo yetu. Wizara ya Ardhi na Wizara ya TAMISEMI tushirikiane, milolongo, bureaucracy zimekuwa nyingi sana. Ushauri wangu ni huo kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.