Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niungane na wenzangu kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika Wizara hii, kwa kweli hongereni sana. Pia nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi anayoifanya ambayo tunaiona, nampongeza sana na sisi sote tuko nyuma yake, tutaendelea kumuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kuzungumzia juu ya upimaji wa ardhi. Katika kupima ardhi, ardhi ndiyo mtaji pekee ambao kila mwananchi wa Tanzania, walio wengi, wanaweza kuwa nao. Ardhi ndicho kitu pekee kinachoweza kutukomboa iwe ni wakulima, wajasiriamali, wanawake au vijana, wote tuna kipande cha ardhi. Pamoja na kazi nzuri abayo Mheshimiwa Waziri amekuwa akiifanya, pamoja na kushusha kodi ya premium kutoka asilimia saba kwenda asilimia mbili; ni kazi nzuri, hongereni; lakini hebu tuangalie bajeti ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tulionao, bajeti ya maendeleo ambayo imekwenda ni asilimia 30 tu, fedha zilizopatikana ni asilimia 30 tu. Hebu tuangalie malengo waliyokuwa nayo. Katika mwaka huu walipanga kwamba wangetoa hatimiliki 400,000, lakini zilizotolewa mpaka tarehe 15, mwezi Mei mwaka huu ni 33,979, sawa na asilimia nane tu ya lengo la mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuwa na wasiwasi, malengo ni mazuri, nia ni nzuri, tunataka wawekezaji waje hapa kufanya biashara waje kuwekeza, wanawekezaje kwenye ardhi ambayo haijapimwa? Tunainuaje hiyo, tunawasaidiaje wananchi hawa ili waweze kufanya kazi yao vizuri? Hao wawekezaji wakija wanataka kujenga viwanda, ardhi haijapimwa. Nadhani lazima tuwaunge mkono fedha ziende ili wapime, malengo yao yafikie, kinyume cha hapo hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeangalia miji yetu ilivyo, miji imekuwa ikikua kiholela, nyumba zimekuwa zinajengwa bila mipangilio. Kule Jimboni kwangu Vwawa, Mji wa Vwawa, kuna maeneo yamepangiliwa, kuna maeneo hayajapangiliwa kabisa, maeneo mengi ni squatters, ukienda miji mingi maeneo mengi bado ni squatters.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupima hayo maeneo tutaendelea kutumia gharama kubwa katika kuendesha nchi hii kwa sababu hata kuwafikia kwenda kutoa huduma hakupo. Sehemu tunazotaka kwenda kujenga huduma za afya, huduma za miundombinu mbalimbali tunashindwa kwa sababu maeneo hayajapimwa. Sasa kasi ya maendeleo ya wananchi ni kubwa ukilinganisha na kasi ya Serikali ya kupima ardhi. Naomba, kama kuna sehemu ya kuwekeza zaidi hili ndilo eneo la kuwekeza, hapo tutakuwa tumepiga dili zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwekeza kwenye ardhi uka-plan, ukaipangilia vizuri, migogoro itapungua, yote itapungua. Nyumba zitakuwa nzuri, kodi zitaongezeka, makusanyo yatakuwa ni mazuri, hata nchi nyingi zinategemea makusanyo ya kodi za nyumba, kodi za viwanja. Sasa kama tusipoipa uzito, tutashindwa. Naomba hilo lipewe uzito unaostahili ili nchi yetu iweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda Mheshimiwa Waziri anipe majibu; pamoja na kazi nzuri aliyoifanya, mimi ni mdau kule Kigamboni, kule Kigamboni alitangaza Mheshimiwa Waziri, alipoingia tu madarakani; akasema ndani ya mwezi mmoja watapata hati, sasa naona amepewa hela kidogo hati hazijatolewa Kigamboni. Mpaka leo wananchi hawana hati, leo hii bado tunahangaika, tunajiuliza ule mji, ile satellite ipo au haipo na ile ramani Mheshimiwa Waziri ilikuwa nzuri hata mimi mwenyewe niliipenda lakini iko wapi? Hati wananchi hawana, mpaka sasa hivi tunashindwa hata tufanye nini. Naomba, hebu akalifanyie kazi tupate hati, twende kukopa ili tuweze kuwekeza katika maeneo mengine tuinue uchumi wa nchi hii. Mheshimiwa Waziri, nafikiri hilo ni la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu ambayo napenda kuchangia ni kuhusu Shirika la Nyumba. Shirika hili ni kweli linafanya kazi nzuri, limejitahidi sana kuwekeza, limejitahidi sana kujenga nyumba na kuna changamoto kadhaa wanazo. Hata hivyo, nawaomba Shirika la Nyumba, hebu angalieni kwenye Mkoa mpya wa Songwe, kule Jimbo la Vwawa ndiyo mkoa umeanza, tunahitaji ofisi, tunahitaji nyumba nyingi, hamjaanza na maeneo yapo. Hebu njooni muwekeze pale ili wananchi wapate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mazuri sana, kuna viwanja pale Mlowo, kuna Mji wa Ihanda, kuna maeneo mazuri sana yamepimwa mengine, hebu njooni muwekeze ili wananchi wapate nyumba nzuri zitakazofaa ili waishi. Bila kufanya hayo, kwa kweli tutashindwa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia pia kwenye kitabu hiki cha bajeti, Mheshimiwa Waziri ameandika, ametupa jedwali kubwa ambalo linaonesha Kamati za Halmashauri za Wilaya za Kugawa Ardhi, maeneo mengi amesema hazijateuliwa, kuna tatizo gani Mheshimiwa Waziri? Kuziteua hizo Kamati zigawe ardhi kuna tatizo gani? Hebu walifanyie kazi, wateue hizo Kamati zifanye kazi, ardhi yote igawanywe, itengwe, itumike kwa jinsi tutakavyokuwa tumeipangilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme, ukichukua hii sekta ya ardhi, sekta ya nyumba, duniani kote ina mchango mkubwa sana na isipokuwa properly managed ndiyo huwa inasababisha hata financial crisis dunia nzima. Sasa hebu naomba tuichanganue vizuri, tuifanyie kazi vizuri ili mambo yawe mazuri na maendeleo ya nchi hii yapatikane. Wananchi wale wanahitaji hizo hati ili waweze kuendelea na nina uhakika, Mheshimiwa Waziri na namkaribisha kule kwenye Jimbo langu la Vwawa, hebu aje atutembelee kidogo. Alikuja Mheshimiwa Naibu Waziri nakumbuka, lakini alikuwa na haraka hatukuweza kuzungumza mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi pale yanatakiwa yapangiliwe. Mkoa wa Songwe ni mpya, ufanane na mambo mapya. Sasa mkoa ni mpya tena uanze kujengwa hovyo hovyo, kila mahali kuwe hovyo hovyo, hiyo kwa kweli inatuchelewesha, inaturudisha nyuma. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu aje atutembelee, aje tupange, atuelekeze ili tufanye kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vifaa alivyosema Mheshimiwa Waziri vya kupima ardhi, vile alivyosema atavinunua, najua atakuwa labda hajanunua kwa sababu ya bajeti ndogo, hebu waharakishe vinunuliwe hivyo, vigawiwe kwenye halmashauri zetu vikafanye kazi ya kupima na sisi tutasaidia kusimamia kule ili kazi iwe nzuri, nadhani maendeleo yatapatikana katika nchi hii na kila kitu kitawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sipendi kupoteza muda mwingi, naomba kuunga mkono hoja na naomba kuwapongeza kwa kazi nzuri. Ahsanteni sana.