Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Salma Mohamed Mwassa

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme ardhi toka dunia iumbwe haiongezeki, lakini watu wanaongezeka, shughuli za binadamu zinaongezeka, kwa hiyo angalia adha wanayoipata wafanyakazi wa ardhi au wasimamizi wa ardhi kwamba unapewa usimamie jukumu ambalo demand yake ipo juu lakini ongezeko lake haliongezeki, kwa hiyo wanapata tabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kabisa tusiwaangalie wafanyakazi wa sekta ya ardhi kwa negative way kama tunavyowaangalia sasa hivi, kwamba wanaonekana ni majambazi, ni wanyang’anyi na kila kitu siyo kweli, tuwaangalie kwa mtazamo ambao wanafanya kazi kwa juhudi kabisa na ndiyo maana wanamwezesha Mheshimiwa Waziri ku–perfom katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri amefanya mambo mazuri kabisa lakini kwa kusaidiwa na timu ambayo ni kali, anayo timu nzuri sana. Kwanza kabisa tukianza na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Moses Mpogole, huyo ni Mwalimu wangu sina tatizo na utalaam wake, yupo vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile analo gwiji wa Uthamini, Dada yangu Ndugu Evelyn Mgasha yupo vizuri. Pia anaye Kamishna ambaye ni makini Mary Makondo Mheshimiwa Waziri ana timu nzuri akianzisha kipenga mpira anaupiga huku hadi huku, hakuna mgogoro wowote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri arasimishe, apime na kupanga amalize mgogoro hakuna kitu kingine hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la maslahi duni ya Wafanyakazi wa Umma. Wafanyakazi wa Umma kwa kweli wana maslahi ambayo hayaeleweki, hawapandishwi madaraja, maslahi yao duni, kwanza kabisa ukiangalia hasa hawa wafanyakazi wa ardhi mnawasakama hapa bure, wafanyakazi hawa wana mazingira magumu sana. Ukiangalia vitendea kazi hawana, unakuta Idara nzima ina gari moja, huyo Afisa Ardhi ataendaje kukagua kiwanja ili aweze kuthibitisha kwamba hiki kiwanja mchoro huu ni sahihi au la!

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hawana hata kompyuta wala nini ya kuweza kusema kwamba hii itawasaidia wao katika kazi zao. Kwa hiyo mazingira yao ni duni, hakuna mbadala, mishahara yao ni midogo. Ukiangalia sekta ya ardhi, hivi mtu unampa akutunzie bilioni moja, kitu cha thamani halafu unamwambia mshahara wake laki mbili, laki tatu, huyu mtu si unamtia kwenye majaribu. Kwa hiyo, hapa ndiyo maana mnawaangalia kwenye mazingira ambayo ni wanyang’anyi, siyo kweli. Waandalieni mazingira wafanye kazi, watumishi wa ardhi wana mazingira mabovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye uhaba wa fedha, Wizara hii pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri amejipamba hapa, anayo hela sijui nini, lakini nikisoma kwamba bajeti ya 2016/2017 aliidhinishiwa bilioni 61 lakini zilizomfikia mpaka Januari ni bilioni 28 tu. Sasa nashindwa kuelewa kwamba je, wamtengee fedha kwa sababu anakusanya sana kwenye kodi, kwenye nini, makusanyo yake siyo mabaya, lakini mbona haletewi hela kwa wakati, yaani hana hela hapa zinazoeleweka. Shilingi bilioni 28 kati ya 61 anafanyaje kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya maendeleo kutegemea fedha za nje, kwanza twende kwenye ule mradi wa Land Tenure Support Program uliopo kwenye Wilaya za Malinyi na Ulanga. Mradi ule umetengewa bilioni tatu hela za ndani, bilioni 10 hela za nje, mpaka tunaenda kukagua ule mradi tunakuta kabisa hela za ndani kati ya bilioni tatu zimepelekwa milioni 400 tu na fedha za nje kati ya bilioni 10 zimepelekwa bilioni 3.4, sasa kama kweli urasimishaji ni tatizo la kuondoa migogoro, kama hiyo miradi haipelekewi fedha kwa wakati na uhaba wa fedha unaoikumba, tunamalizaje hiyo migogoro? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwenye Mabaraza ya Ardhi. Mabaraza ya Ardhi haya sheria yake imepitwa na wakati, tunaomba Mheshimiwa Waziri alete hapa sheria tena kwa sababu mabaraza haya yanasema kwamba yasiongelee mali ambayo inapita milioni hamsini, kwa Mabaraza ya Wilaya lakini Mabaraza ya Kata wanasema yasiongelee kitu chenye thamani inayozidi milioni tatu, sasa eneo kama la Dar es Salaam, nyumba ya milioni 50 unaipata wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, hali hii inasababisha mlundikano mkubwa kwenye Mahakama hizi za Ardhi, Mahakama Kuu tu, haya Mabaraza yamekuwa kama mapambo kwa sasa, hii sheria yake imepitwa na wakati, tunaomba Mheshimiwa Waziri ailete hapa Bungeni tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niongelee kwenye miradi ya ujasiriamali; kuondoa hii migogoro ya ardhi Mheshimiwa Waziri lazima apime na kupanga ardhi. Kwa ufinyu wa bajeti kama ninavyouona hapa ina maana kupima kama kupima Mheshimiwa Waziri hataweza gharama ni kubwa, kurasimisha pia itakuwa ni jibu lake sahihi. Kwa hiyo, kama ndiyo hivyo basi, huu urasimishaji kwenye hii miradi iliyoanza usiende kwa kusuasua kama ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameutaja hapa mradi wa Kimara, lakini mradi ule unaenda kwa kusuasua sana. Mimi mwenyewe natembelea pale mara kadhaa, mradi ule watu wale hawana magari ya kwenda site, hawana mafuta, hawana beacons, wale wafanyakazi hawajalipwa, wengine hata vibarua wameshasusa kwenda hata site. Mheshimiwa Waziri ananiambia kwamba mradi huu unaendelea vizuri, naomba tu autembelee au kama vipi tuongozane twende tukautembelee, kwa sababu naona anaupamba bure wakati mradi huu umekwama, naomba twende tukatembelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee, Tume ya umiliki wa ardhi, ile Tume ya kupanga ardhi. Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi ni Tume ambayo nayo inatakiwa iwekwe kipaumbele lakini mpaka sasa toka mwaka jana Tume hii inapangiwa pesa ndogo sana, sielewi kama hawaitaki, kama hawaitaki basi waifute tuelewe. Sasa mbona wanaipangia bilioni mbili, bilioni mbili watafanya nini hawa? Kama hii Tume ingeshirikiana na Wizara hii vizuri, ungekuwa ni mwarobaini wa hili tatizo, migogoro yote ingekwisha na tungeelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia mambo ya kodi ya ardhi, kodi ya ardhi inavyoonekana kwenye Wizara hii ndiyo uti wa mgongo wa maduhuli yote, lakini hiyo kodi ya ardhi inapatikana wapi kama eneo halijapimwa na kupangwa? Naomba kabisa Mheshimiwa Waziri urasimishaji huo apange hela nyingi apeleke huko ili aweze kupata kodi ya ardhi, asing’ang’anie kutoza kwenye maeneo yasiyopimwa, anakiuka Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 Na. (5) na (4), huwezi kutoza kodi kwenye maeneo ambayo hayajapimwa, atakuwa anatoza kwa kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atueleze kabisa akihitimisha kwamba anavyotuambia kwamba anatoza kodi kwenye maeneo yasiyopimwa kivipi? Wale watu hawana nyaraka kwanza anajuaje, kwa sababu kodi ya ardhi ni Mthamini anathamini lile eneo, akishathamini ndiyo anakwambia kwamba hili eneo kulingana na location yake basi inatakiwa itozwe kodi kiasi fulani. Sasa hapo ananiambia kwamba anatoza kodi kwenye maeneo ambayo hayajapimwa kwa vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri asikwepe jukumu lake, apime, apange, arasimishe akiona vipi mambo yamemwendea vibaya aombe hela hata huko nje, kama hivi anavyotegemea hela za nje halafu yeye mwenyewe za ndani amebana, sasa sijui itakuwaje! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee mambo ya uthamini, kuna Mbunge mmoja hapa alikuwa anasema kabisa mambo ya uthamini, ooh, Valuers ni wadanganyifu, sijui kwenye mali ya bilioni moja anasema milioni mbili. Hao siyo Wathamini waliosoma Chuo cha Ardhi, hao watakuwa ni Valuers wa mtaani anawajua yeye huyo Mbunge, Valuers makanjanja na Valuers ambao wamesoma Chuo cha Ardhi hawawezi kuongea udanganyifu, wao wanatumia opinion yao wanatumia kanuni, sheria na taratibu walizofundishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Valuers ni watu waliosoma muda mrefu, hawawezi kufanya cheating za hovyo, yeye aangalie vizuri huyo aliyethamini mali ya bilioni moja kuja kuirudisha milioni mbili, amuulize vizuri alitoka wapi, inawezekana hao ndiyo vishoka kwenye hiyo taaluma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siamini kabisa kwamba Valuers aliyefundishwa na Walimu makini na Walimu wenyewe mnawaona walivyo makini mpaka wameenda kumteua Naibu Katibu Mkuu kule na wameona umakini wake anaouonesha leo aende akamfundishe Valuer anaye-cheat haiwezekani! Huyo siyo Valuer aliyefundishwa Chuo cha Ardhi ni kanjanja sijui alipotoka ni wapi mpaka akakutana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niendelee kusema ukosefu wa wataalam au upungufu wa wafanyakazi kwenye hii Wizara ya Ardhi au kwenye sekta ya ardhi. Kwa kweli mpaka sasa kuna upungufu mkubwa wa wafanyakazi kwenye sekta ya ardhi, zaidi ya asilimia 70 kuna upungufu, wafanyakazi waliopo ni wachache sana, sasa hivi unakuta Afisa Ardhi mmoja anafanya kazi za Maafisa Ardhi 10 mpaka 20, mtu mmoja, halafu bado mnamsonga na maneno, bado sijui mwizi, siju nini, bado mshahara wake mdogo, hana over time, naomba mtoe kibali cha kuajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.