Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hii. Nichangie hoja hii katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Wizara. Nioneshe masikitiko makubwa sana kuona kuwa bajeti ya Wizara hii muhimu na inayomgusa kila Mtanzania badala ya kuongezeka, imepungua. Ni ukweli usiofichika kila Mheshimiwa Mbunge hapa ana shida ya maji katika jimbo lake. Kwa mfano mdogo tu bajeti ya Halmashauri yangu ya Kilindi ya mwaka wa fedha 2016/2017 ilikuwa shilingi bilioni 3.7 lakini mwaka huu imeshuka hadi shilingi bilioni 1.6. Hivi Wilaya hii yenye ukame mkubwa na yenye vijiji 102, kata 21 na vitongoji 650 bajeti hii itatosha kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inao Mfuko wa Maji, nasikitika kiasi kilichokusanywa ni kidogo sana. Ushauri wangu; badala ya kutoza sh.50/= katika lita ya mafuta ya dizeli na petrol tozo hii ipande iwe sh.100/=. Hii itasaidia kupunguza kero ya maji. Vile vile naamini tusipopunguza kero hii wananchi watakata tamaa na Serikali yao. Ikumbukwe wanaopata shida sana ni mama zetu na hasa waishio vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukaguzi wa Miradi. Katika maeneo ambayo Serikali imetoa fedha nyingi hakuna utaratibu ulio rasmi kati ya Wilaya hii na TAMISEMI na hii imepelekea miradi mingi kutekekelezwa chini ya kiwango. Nishauri sasa miradi yote ya maji ifanyiwe “Perfomance Auditing” kupitia ofisi ya CAG.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litaimarisha uwajibikaji na miradi mingi iwe na tija. Mfano mzuri ni mradi wa maji kutoka Wami kwenda Vijiji vya Chalinze, mkaguzi alibainisha namna ambavyo wakandarasi wanavyoisababishia Serikali hasara. Ni imani yangu Serikali itaona umuhimu wa kufanya ukaguzi wa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Visima vya Maji Makao Makuu ya Wilaya. Niipongeze Wizara kwa kunichimbia visima vinne katika halmashauri yangu kwa msaada mkubwa kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ambaye kwa sasa ni mstaafu. Visima hivyo vimeainishwa katika jedwali Na. 13.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Vijiji vya Sanje, Vilindwa, Nkama na Mafisa vimechimbwa lakini bado miundombinu ya kukamilisha miradi hii iweze kufanya kazi bado. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, maeneo haya yote yana shida kubwa sana ya maji. Miradi hii ikikamilika itasaidia mamlaka ya maji ya Songe iweze kufanya kazi kwa kujitegemea na ni takribani miezi sita sasa imepita toka wakala wa visima alipochimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ushiriki wa Sekta binafsi katika Sekta ya Maji na Umwagiliaji. Nipongeze juu ya wazo hili, ni wazo sahihi na pengine limechelewa. Naamini kabisa kwa changamoto hii ya tatizo la maji bila kushirikisha sekta binafsi kwa mpango wa PPP hatutaweza kufika mbali. Niishauri Serikali ifanye hima kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi jambo hili lianze haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni kubwa na yenye wananchi wengi. Kwa kushirikisha sekta binafsi ni wazi kutakuwa na gharama katika kuleta huduma hii ya maji, lakini vyema wananchi wetu wachangie katika kupata huduma ya maji kuliko kusubiri huduma ya bure kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Uchimbaji wa Mabwawa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeona ametaja bwawa moja tu la Kwamaligwa, wakati katika Jimbo langu tunalo bwawa lingine la Jungu ambalo lipo katika hatua za umaliziaji, lakini sijaona mahali popote tulipotengewa fedha. Nitaomba sana majibu ya Mheshimiwa Waziri, kwa nini bwawa hili halijatengewa fedha, lakini pia Wilaya yote? Njia bora ya kuwapatia wananchi hawa huduma ya maji ni kuchimba mabwawa mengi ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo bwawa moja tu la Kwamaligwa. Niombe Mheshimiwa Waziri tupatiwe mabwawa ya kutosha katika Jimbo langu lenye jamii ya wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi kuomba Mradi wa Maji. Wilaya ya Kilindi hatuna mto hata mmoja wala ziwa, nashangaa Wizara imeweza kutenga fedha katika maeneo yenye changamoto kama zetu wamepewa au kutengewa fedha nyingi za miradi ya maji lakini maskini Wilaya yangu haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri amtume Mheshimiwa Naibu Waziri au watumishi waliopo chini yake waje Jimboni kwangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupata mradi mkubwa kama vile HTM ambao umefika Handeni kwa kutoa maji Mto Ruvu. Kwa nini Wizara imeshindwa kufikisha mradi huu Kilindi?

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri afike na kutazama Wilaya ya Kilindi kwamba nao ni miongoni mwa maeneo yenye ukame na wanahitaji sana kupatiwa mradi wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.