Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza hotuba ya bajeti ya Wizara hii na naunga mkono. Sote tunajua upatikanaji wa fedha na kazi nzuri iliyofanyika kwa kipindi hiki kinachoisha cha mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii wamejitahidi kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Wizara hii iongezwe ili kutoa nafasi shughuli nyingi za upatikanaji na usambazaji wa maji safi na salama ziweze kufanyika. Hivyo, nashauri kuwepo na tozo ya Sh.50 kwa bidhaa ya mafuta ili kuchangia kutunisha Mfuko wa Maji. Wizara na Kamati husika wawasilishe ombi kupitia Kamati ya Bajeti ili hoja ya kutoza kiasi hicho iingizwe kwenye hotuba ya Waziri wa Fedha kama tozo/kodi mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kuwepo mkakati wa kutunza vyanzo vya maji ambalo ndiyo suala la msingi zaidi ili maji kwa matumizi ya wananchi yapatikane. Wizara kupitia bajeti hii iwe na mikakati itakayopelekea suala la uhifadhi wa vyanzo vya maji kutekelezwa nchi nzima na kila Halmashauri iweze kutenga fedha za kutekeleza mkakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lambo la maji Lutubiga – Busega. Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea Wilaya ya Busega na kujionea bwawa la maji ambalo liligharimu fedha nyingi ambalo lilichimbwa na Serikali kupitia Wizara hii lakini halina wala halijawahi kutoa maji kwa matumizi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa hili limekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Kijiji cha Lutubiga, Kata ya Lutubiga, Wilaya ya Busega ambao wana uhitaji mkubwa sana wa maji na kwamba hawajapata maji licha ya bwawa hilo kuchimbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia bajeti hii, naiomba Wizara kwanza itume wataalam ili kutathmini hali hiyo na urekebishaji wa bwawa hili uweze kufanyika mara moja. Hii itasaidia kuwapatia wananchi ambao wamekuwa wakiteseka kwa kukosa maji ilhali tayari Serikali imekwishalipa fedha nyingi ambazo makosa tu kidogo ya kitaalam yamepelekea kukosekana kwa maji, hivyo basi, Wizara ichukue hatua stahiki mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.